Mwezi wa gharama wakaribia huko Zenj...
Unapokaribia mwezi mtukufu wa Ramadhani, Jiji la zenj hujaa pilikapilika nyingi mno, ni rahisi sana kutofautisha jinsi watu wanavyoishi kabla ya mwezi huo kwani kila mtu huwa kwenye pilika za hali ya juu, tofauti kabisa na miezi mengine yoyote katika mwaka.
Kijana mmoja aliwahi kunilalamikia kuwa ingependeza kama kufunga mwezi Mtukufu wa Ramadhani ikawa kama fainali za kombe la dunia kutokea mara moja kwa miaka minne tena katika nchi tofauti. Akiwa na maana iwapo itakuwa zamu ya Tanzania kufunga mwaka huu nchi zingine hazitofunga mpaka zamu yao ikifika....! Sikupata picha kamili ingekuaje kwa nchi zaidi ya mia mbili duniani humu.. Mawazo kama haya uzaliwa kichwani mwa mtu kutokana na majukumu mengi katika mwezi huo.
Kabla ya mwezi kufika wengi hupata mialiko ya kuhudhuria shughuli za arusi, hii yote ni katika kujiandaa na mfungo, kwani wengi hupenda kufuturu majumbani mwao, hivyo vijana wengi hupenda kufunga ndoa katika kipindi kama hichi ili mradi tu awe na uhakika wa kupata futari murua akiwa kwake.
Hali halisi ya Zenj na hasa katika kuandaa futari husababisha ugumu mkubwa katika mwezi huu. Bei za bidhaa hupanda maradufu hivyo kuwa usumbufu mkubwa kwa waakazi wengi wa kipato cha kati visiwani hapo. Ikiwa bado siku kadhaa kabla mwezi huo kuanza bei ya nyama kwa kilo sasa ni zaidi ya sh. 5,000 huu ni mzigo mkubwa. Ikumbukwe bidhaa za vyakula kisiwani humo nyingi hutoka Bara na Pemba, hata hivyo uonekana kama havitoshi pamoja na ukubwa wa gharama.
Sina hakika kama kisiwa cha pili bado wataendeleza mgomo wao wa kutopeleka vyakula huko Zenj, baada ya muafaka kurudishwa tena mezani, na sina hakika hali itakuaje baada ya kasheshe za karibu miezi mitatu kuhusu Zenj kama nchi zitaathiri vipi mfungo wa mwaka huu. Kawaida pamoja na rais wa Zenj kutembelea kwenye markiti akiwaomba wauzaji kupunguza bei, bei hubaki palepale. Safari hii rais atavuka hatua ya kwenda markiti, kwani itabidi kuwashawishi waletaji bidhaa kufanya hivyo na kuweka siasa kando katika mwezi huu.
Ikumbukwe kuwa wananchi hao hujiandaa kwa muda wa miezi kumi kuja kufunga kwa mwezi mmoja, kwani bila ya kujiandaa na kujiwekea akiba unaweza kuja kuumbuka katika kutafuta futari hivyo kuufanya mfungo kuwa mgumu zaidi. Zaidi ya wao wenyewe kujiandaa, ndugu wengi waishio nje ya Zenj na hasa nje ya Afrika wamekuwa mstari wa mbele kusaidia kupunguza makali ya mwezi huu, kwa kujaza wazenj wengi katika ofisi za west union. Kwani pamoja na kujiandaa na futari pia ni mwanzo wa maandalizi ya sikukuu ya Idd ambayo usheherekewa kwa muda wa siku nne mfululizo. Sherehe hizo ni kubwa sana hasa kwa watoto ambao uwakera wazazi wao kwa kudai nguo mpya na maridadi, toys na kadhia zingine ziendanazo na sherehe hizo.
Mie binafsi napenda kuwatakia Wafungaji wote Mfungo mwema....
No comments:
Post a Comment