Tuesday, 4 August 2009

Mwakilishi adai wizi wa watoto umekithiri Zanzibar


WAJUMBE wa Baraza wameishauri Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kufuatilia kwa kina upoteaji wa watoto katika maeneo mbalimbali pamoja na kushughulikia suala la utumiaji wa dawa za kulevya nchini.

Walitoa ushauri huo jana walipokuwa wakichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Kazi Maendeleo ya Vijana, Wanawake na watoto kwa mwaka wa fedha 2009/10 katika kikao cha baraza la wawakilishi kinachoendelea Mjini Unguja.

Mwakilishi kupitia Wanawake (CCM), Raya Suleiman Hamad, alisema kuna haja kwa serikali kuanzisha uchunguzi huo kwani watoto wengi wanapotea ovyo katika mitaa yao, huku wazazi wao wakiwa wanahangaika kuwatafuta bila ya mafanikio.

Alisema kwamba inavyonekana wapo baadhi ya watu wanaoendesha biashara ya kuiba watoto jambo ambalo tayari limeanza kuwatia hofu baadhi ya wazazi nchini.

Mwakilishi huyo alisema kwamba watu wanaoendesha vitendo hivyo hutumia njia za kuwahadaa kwa kuwafuata watoto na kuwapa fedha kisha wanawasihi wawafuate ili wakawanunulie nguo.

Mwakilishi huyo alitoa mfano katika mtaa wa Nyerere kwamba kuna kesi za kupotea watoto wanne na kwamba hadi sasa hawajapatikana pia hawajulikani walipotea katika mazingira gani.

Aliitaka serikali ichukue hatua za kufanya utafiti juu ya suala hilo kwa vile tayari limeanza kuwatisha wananchi na linaweza kusababisha madhara makubwa baadaye

Alisema wakati serikali ikilitafakari hilo, ni vyema hivi sasa kuangaliwa uwezekano katika bandari na Viwanja vya Ndege watu wanaoonekana kubeba watoto wakahojiwa uhalali wao.

Mwakilishi huo pia alizungumzia suala ubakaji wa watoto kuendelea ikiwa pamoja na wagonjwa wa akili na kutaka vyombo vya sheria kutekeleza majukumu yao bila ya upendeleo kwani matendo kama hayo yakiachwa yanaweza kuhatarisha usalama kwa watoto .

Akitoa mifano Mwakilishi huyo alisema iliyowahi kujitokeza kisiwani Pemba baada ya mtoto mmoja kubakwa lakini kesi yake ilipopelekwa Polisi wamekuwa wakishindana na Polisi kwa kuwaeleza wahusika hawana la kufanya na waende wakamkamate mhusika wampeleke kituoni hapo.

Mwakilishi huyo pia alisema ni lazima serikali iandae mkakati maalum wa kukabiliana na tatizo hilo kwani suala la madawa ya kulevya linaonekana kama vile limeshindikana kutokana waletaji na wauzaji wa dawa hizo kuwa wanafahamika lakini hawachukuliwi hatua zozote za kisheria wakati vijana wengi wanazidi kuharibika na utumiaji wa madawa hayo.

No comments: