Thursday, 21 January 2010

Maalim Seif ajibiwa....

Maalim Seif asiachwe kuizunguka historia ya Zanzibar


LIMEFANYIKA jaribio dhaifu la hadaa ya kisiasa; jaribio ambalo maelfu ya Wazanzibari wameliamini na kulikubali na bila ya kujali itikadi zao na mirengo yao ya kisiasa, wamelikumbatia kama ukweli na kuandamana kuliunga mkono.

Jaribio hilo ni lile la kupotosha historia ya Zanzibar ili kujipa alama bora za kisiasa. Jaribio hilo limefanywa na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Seif Sharrif Hamad katika hotuba yake ya kuelezea juu ya “maridhiano na mustakabali wa Zanzibar”.

Kwa mtu yeyote aliyesoma hotuba hiyo ya Maalim Seif, ukweli mmoja unajionyesha wazi kama mwili wa mbuni aliyejificha kichwa chake mchangani, na kama mwangaza wa radi, hotuba hiyo imefunua ulaghai wa kisiasa ambao mtu makini anaweza kuuona toka mbali na kuukwepa.

Nasikitika wananchi wa Zanzibar katika kile kinachodhaniwa kuwa ni umoja wao, wamekumbatia historia hii mpya ya Zanzibar; historia ambayo kiukweli ni mpya!

Historia isiyo na doa ya Zanzibar

Kitu cha kwanza ambacho tunakiona katika historia hii mpya ya Zanzibar kwa mujibu wa Maalim Seif, ni historia isiyo na “doa” ya Zanzibar. Katika historia yake, Maalim Seif anaielezea Zanzibar katika mwanga wa uzuri wa paradiso. Anadai kuwa Zanzibar, licha ya udogo wake kama kisiwa, ilikuwa na umuhimu mkubwa katika eneo la Afrika ya Mashariki, Uarabuni, Bahari ya Hindi na Mashariki ya Mbali. Anadai kuwa umuhimu huo “ulitokana na maendeleo makubwa yaliyokuwa yamepigwa Zanzibar katika nyanja mbali mbali za maisha.”

Katika ‘maendeleo haya’ utumwa hautajwi wala kuhusishwa! (nitaliangalia hili mbele zaidi kwa wakati huu yatosha kuliweka mawazoni kama utumwa ni sehemu ya maendeleo ambayo Maalim Seif anaisifia Zanzibar!).

Mojawapo ya vitu vingine vya kihistoria ambavyo Maalim Seif amevionyesha katika kutangaza utukufu wa Zanzibar ni madai kuwa “Zanzibar inaelezwa kutajwa kwa majina tofauti tangu miaka 500 kabla ya kuzaliwa Nabii Issa (Yesu Kristo). Uvumbuzi wa karibuni wa mapango ya watu wa kale katika ukanda wa Mashariki Kusini mwa kisiwa cha Unguja unaonyesha kuwepo kwa makazi ya watu tokea zama za mawe ziitwazo ‘Stone Age’.

Katika kitabu maarufu chenye kumbukumbu za wasafiri wa kale wa Ugiriki waliotembelea mwambao wa Afrika Mashariki kiitwacho Periplus of the Erythrean Sea, kilichoandikwa mwaka 100 A.D. (kabla ya Nabii Issa), Zanzibar imetajwa kwa jina la ‘Menouthias’ ikiwa tayari ni nchi yenye watu mchanganyiko tena walio na ustaarabu wakiwa wanavaa nguo za hariri.”

Sasa alivyozungumza kwa uhakika ni kana kwamba wasomi wote duniani wanatambua kuwa “menouthias” ndiyo Zanzibar! Bila ya shaka Wazanzibari waliomsikia na kumsoma hivyo walifurahia mioyoni mwao kuwa kweli Zanzibar inatajwa katika maandishi ya kale.

Sitoshangaa kama watu wa Bara ambao hawajui historia yao waliinamisha vichwa vyao kwa sababu hawajui kama eneo lao linatajwa mahali popote au historia yao ndiyo imeanza mwaka 1884 au wanafikiria Bagamoyo ndiyo sehemu ya kale zaidi!

Kama Maalim Seif angependa kuwaambia ukweli wa Zanzibar juu ya miji ya kale na jamii za kale zilizowahi kutajwa kwenye maandishi ya kale, angewaambia watu wake juu ya mji wa kale wa Rhapta! Najua wengine mnajiuliza “ze what?”!

Katika kitabu hicho hicho cha maelezo ya safari za majini za kale katika bahari ya Hindi, kunatajwa vile vile mji wa Rhapta ambao tunaambiwa ulikuwa ni mji pwani ya Azania umbali wa usafiri wa kama siku mbili toka visiwa vya Menouthias.

Mmoja wa wataalamu wetu wa mambo ya kale Prof. Felix Chami anaweza kulielezea hili kwa kina kuwa siyo Zanzibar peke yake ambayo ina historia ya kale na kuwa watu wake walikuwa wakiishi katika jamii na kufanya biashara vizuri tu.

Ujio wa utawala wa Sultani

Katika historia yake hii mpya ya Zanzibar, Maalim Seif anadai kuwa “Mwaka 1503 Wareno waliivamia Zanzibar kupitia Unguja Ukuu na wakaitawala kwa muda mrefu wakifanya vitimbi vya kila aina. Waomani, kwa maombi ya wenyeji, walikuja katika Dola ya Zinj na kupambana na Wareno na hatimaye wakafanikiwa kuwatimua.” Katika hili tunaona mambo mawili yanayotajwa kwanza ni uvamizi wa Wareno (ambao kwa yeyote aneyejua historia haukukoma kwa visiwa hivyo tu) na pili “maombi ya wenyeji kwa Waoman”.

Kwamba Wareno walikuwa na vitimbi ni maneno machache; kwani historia yao inajulikana hadi Mombasa na Lamu. Tunapoambiwa kuwa wenyeji waliomba Oman ije kuwasaidia kuwaondoa Wareno, hatuambiwi ni wenyeji gani hao? Lakini wakati huo huo ni lazima tukumbuke kuwa utumwa ulikuwepo!

Yawezekana wenyeji waliotaka Oman kuja kuwaondoa Wareno walikuwa ni watumwa? Je watumwa walifaidika vipi na ujio wa Wa-Oman?

Balozi za kigeni huko Zanzibar

Maalim Seif anatuelezea katika hii historia mpya ya Zanzibar kuwa “Katika kipindi hiki Zanzibar iliweza kujitambulisha na kutambuliwa kama Dola huru katika ulimwengu. Zanzibar ikawa kituo muhimu cha kisiasa, kiuchumi na kibiashara katika Afrika Mashariki na Bahari ya Hindi.. Kutokana na umuhimu wake, madola makubwa yalifungua Ofisi za Kibalozi mjini Zanzibar : Marekani (1837), Uingereza (1841), Ufaransa (1844), na baada ya hapo Ureno, Utaliana, Ubelgiji na Ujarumani zikafuata.”

Mzanzibar ambaye hajui historia ya Zanzibar na mtu wa bara ambaye anayasoma maneno haya anaamini kabisa kuwa balozi hizo zilifunguliwa kwa sababu ya Zanzibar “kujitambulisha na kutambuliwa kama dola huru katika ulimwengu”.

Bahati mbaya ni kuwa kuna historia ambayo Maalim Seif hakutaka kuikiri hadharani inayohusiana na kufunguliwa kwa balozi hizo Zanzibar na siyo sehemu nyingine katika eneo letu hili. Naomba ruhusa nimkumbushe sehemu hii ya historia yetu.

Mwaka 1822 Sultan wa Oman, Sayyid Said Bin Sultan aliingia mkataba ujulikanao kama Mkataba wa Moresby. Mkataba huu, pamoja na mambo mengine, ulipiga marufuku uuzaji wa watumwa kwa nchi za Kikristu kutoka katika himaya yote ya Sultani huyo. Ni kutokana na mkataba huo na mingine iliyofuatia ndio nchi za Marekani, Uingereza , Ufaransa n.k zilipoamua kuanzisha ofisi zao za ubalozi huko ili kuhakikisha mojawapo ya mambo mengi kuwa Sultani wa Zanzibar anaheshimu makubaliano ya Moresby, Hamilton n.k

Ukiangalia tarehe ya kuanza kwa balozi hizo kama Maalim alivyoonyesha (1837) unaweza ukafikiria ni kwa bahati nzuri tu kuwa ndani ya miaka kama saba nchi mbalimbali za Kimagharibi zimefungua balozi zao huko?

Ikumbukwe kuwa mwaka 1832 (wanahistoria wengine wanaweka tarehe ya mbele kidogo) Sultani wa Oman alihamishia maskani yake kutoka Omani na kuwa Zanzibar makao makuu. Kutokana na ukaribu wake na nchi hizo za Magharibi Zanzibar hatimaye ilifanikiwa pole pole kukomesha utumwa na utumishi wa kulazimisha (servitude).

Omani, hata hivyo, ambayo tunaambiwa ndio walikuwa watu wema kwetu, waliendelea na hali hiyo kwa namna moja au nyingine hadi mwaka 1870 kufuatia mapinduzi yaliyomuingiza Sultan Qabus na Saudi Arabia yenyewe chini ya Mfalme Faysal ilifanya hivyo mwaka 1869!

Hii ni muhimu kuelewa kwa sababu ni sehemu ya Historia ya Zanzibar, na ni historia yetu vile vile. Hatuwezi kuikana, kujificha kwa haya au hata kuitaja kwa jina.

‘Uhuru’ wa Zanzibar ni uhuru?

Jambo jingine ambalo Maalim analielezea ni kuwa “Uingereza ilikabidhi uhuru kwa Zanzibar tarehe 10 Desemba 1963 chini ya Sultani na Serikali ya ZNP/ZPPP. ASP hawakuukubali uhuru huo na tarehe 12 Januari, 1964 ilifanya Mapinduzi na Zanzibar ikatangazwa kuwa Jamhuri.”

Wapo watu wanaoamini kabisa kuwa huu kweli ulikuwa ni “uhuru wa Zanzibar”. Ndio hawa ambao bado wanapata shida kuyatambua Mapinduzi ya Zanzibar na ulazima wa kwanini yalitokea. Unaweza kuliona hilo katika hotuba hiyo ya Maalim Seif.

Utaona mambo makubwa matatu ambayo ni sehemu ya historia ya Zanzibar hayatajwi kabisa na kama hilo hapo juu yanatajwa kama kwa kupita. Kwanza ni suala la utumwa na pili ni utawala wa Sultani wa Zanzibar na kama wananchi waliokuwa watumwa au watu weusi walinufaika na utawala huo.

Ndugu zangu, tunapotaka kujenga Zanzibar mpya na Tanzania mpya tuipendayo, hatuna budi kuwa wakweli kwa historia yetu. Tusiikane au kuona ni vibaya kuikiri. Wamarekani walikuwa na utumwa, Wamarekani walipigana wenyewe kwa wenyewe na zaidi ya nusu milioni walikufa.

Wamarekani walikuwa na ubaguzi wa rangi licha ya Katiba yao kutangaza usawa wa binadamu wote na haki zao. Leo hii Wamarekani wameweza kumchagua mtu mweusi kuwa Rais wao miaka chini ya hamsini tu tangu vurumai za mwamko wa haki za watu weusi nchini humo!

Bila ya kura za watu weupe Obama asingeweza kuwa Rais wa Marekani! Watu weusi wa Marekani ni kama asilimia 12 tu ya Wamarekani wote! Kwa maneno mengine, watu weupe ambao wamekuwa wakiangaliwa vibaya na kubebeshwa lawama za utumwa na ubaguzi na watu weusi walikubali historia yao na kuikumbatia na kujitokeza kumchagua mtu mweusi.

Hii ni historia yetu!

Hii ina maana kwetu leo hii. Waarabu, Wahindi, Washirazi na watu weusi wa Zanzibar na Tanzania Bara, ni lazima watambue kuwa hata tukimbie vipi, hata tujifiche vipi na hata tukwepe vipi, historia yetu imefungamana milele. Hata kina Maalim wasipotaja utumwa wasidhanie kuwa basi utafutika katika historia!

Na pia ni lazima tutambue kuwa kama taifa hatuwezi kuwabebesha Waarabu na Waoman wa leo mzigo wa dhambi ya utumwa na kuwaona kuwa ni waonevu juu yetu.

Kama vile Marekani, natambua wapo watu ambao bado hawamuoni mtu mweusi kuwa ana haki sawa na kumheshimu. Wapo watu weupe Marekani ambao hadi leo hii hawamtambui Obama kama Rais wao! Sitoshangaa wapo kati yetu uzao wa Wa-Oman na Waarabu wengine ambao wanaona watu weusi bado ni duni!

Na katika upotofu Fulani, wapo watu weusi ambao wanaamini kabisa kuwa bila ya wao kukubaliwa na Waarabu hao au na Washirazi, basi siyo binadamu hasa. Na wengine wamefikia hata kujiita “Waarabu” ili waonekane kukubalika. Huu ni upumbavu.

Waarabu wa Tanzania ni wananchi wenzetu na wana haki zote kama Watanzania wengine. Hawana haki au utu zaidi kwa sababu ya Uarabu wao.

Watu wenye asili ya Omani ambao vizazi vyao vimegawanyika Zanzibar na Oman wasijione kuwa wao ndiyo Waarabu hasa kulinganisha na Waarabu waliochangia damu na Wamanyema na Wanyamwezi wa Bara!

Wahindi ambao hawajachangia damu yoyote na watu weusi na wana vizazi Tanzania na India wasijifikirie kuwa wao ni watu bora zaidi na kuwa watu weusi bado ni maboi wao!

Nayasema haya ili ijulikane kwamba Tanzania tunayoitaka ni Tanzania yetu sote - historia ya Zanzibar ni historia ya Tanzania. Huu upuuzi wa kutaka kufanya watu wa Bara ni duni kwa sababu hawana historia ya taa za barabarani na televisheni za rangi, ni lazima ukome hata ukitolewa na wanasiasa tunaowapenda.

Huu mtindo wa “Zanzibar ilikuwa pepo na mapinduzi yakaharibu”, ni mtindo tunaopaswa kuukataa kwa nguvu zetu zote!

Ndiyo maana ni muhimu kujua kama kina Maalim Seif wanatambua ulazima wa mapinduzi yale na kuyakubali si kwa ajili ya kupata pointi za kisiasa bali kifalsafa na kimaadili. Ni lazima tujue kama kina Seif wanaweza kusema kuwa waliona matatizo yoyote ya utawala wa Sultani huko Zanzibar au wao bado wanaamini kuwa Sultani alionewa tu.

Na ndiyo maana katika haya pia mimi ninaamini kabisa kuwa mojawapo ya mambo ya kupatana Zanzibar ni lazima suala la Sultani lizungumzwe siku moja na kuhitimishwa, kwa sababu tunajua hadi leo hii Sultani wa Zanzibar hajakikana kiti chake cha Usultani wa Zanzibar na watoto wao bado wanaendelea kujitambua kuwa ni wana wa Sultan (Prince na Princesses).

Wote hawa ndugu zangu ni sehemu ya historia yetu na wakati umefika tuache kujitenga kwa mambo ya kijinga tukifirikia kuwa tunachofanya ni hekima na busara na ni uzalendo. Zanzibar haiwezi kukaa katika kivuli cha Sultani anayesubiri siku moja arudi na kukalia kiti chake!

Wananchi wa Zanzibar wasikubali hadaa ya maneno ya kisiasa, wasikubali kuimbiwa zumari za uongo na wao wakacheza.

Zanzibar ina historia yake na historia hiyo ina mazuri na mabaya yake kama vile ilivyo historia ya Uingereza, Japani, na China!

Historia hiyo ya Zanzibar ni historia ya Azania! Ni historia ya Tanzania yetu leo hii. Katika hili hatuna sababu ya kuomba radhi na Wazanzibari wasifikirie kuwa tutawaonea wivu. Wao ni sehemu yetu, sehemu ya damu yetu; kwani hatuwezi kamwe kuandika historia ya Tanganyika au Mwambao wa Afrika ya Mashariki bila kuandika historia ya Zanzibar.

Wana CCM Zanzibar wameliabisha taifa

Kitendo cha uongozi wa CCM Zanzibar kukubali na kukumbatia uongo kwa kisingizio cha “Zanzibar moja” ni cha hatari kwa muafaka wa taifa; kwani kinalenga kudhoofisha muungano na Rais Kikwete na Watanzania wasipoangalia ni ujumbe mkubwa wa kisiasa ambao matokeo yake hata kichaa anaweza kuyatabiri.

Wana CCM wa Zanzibar na Watanzania wa Zanzibar watambue kuwa wao ni sehemu ya jamhuri yetu, historia yetu ni historia yao na historia yao ni yetu. Tofauti za kisiasa na kimtizamo ni tofauti zinazozungumzika (hata leo hii majimbo ya Marekani na hata Uingereza wanazungumzia tofauti zao za kisiasa na kiutawala)

Katika kutafuta sifa za kisiasa, Rais wa Zanzibar asilipeleke taifa kwenye uchaguzi mbaya kwa kukumbatia uongo.

Vinginevyo, Dk. Karume atajikuta anafifisha na kudunisha na kudharau damu ya wale waliokufa katika mapinduzi na kufanya mapinduzi yale kuwa hayana maana yoyote! Historia itamhukumu vibaya sana akiendelea na maamuzi anayofanya sasa.

Kina Maalim wasitugawe sasa kwa historia wakifikiri wanatutendea hisani. Na nimeudhika kuona wana CCM wameingia katika mtego huu huko Zanzibar kiasi cha kupepea uongo kwa kanga zao za kijani na njano!

Ninaona fahari kuwa Zanzibar ni sehemu ya Tanzania. Ninaona fahari ya kujua historia yetu kama taifa.

Naomba niishie hapa. Nitajibu hoja zake za kisiasa alizozitoa wiki ijayo, inshallah.

5 comments:

Anonymous said...

Kibs,

Majibu haya kayatoa nani?

Kibunango said...

Anoy:
kwenye headline ya bandiko nimeweka link ya huyo aliejibu! Hata hivyo ni Lula wa Ndali-Mwananzela

Anonymous said...

Mimi ningependa kujuelimishwa, jee haya mazuri yote aliyeandika Maalim Seif, yana ukweli wowote? Na kama ni kweli tupu, tatizo liko wapi?

Ikisha tukija kwenye suali la utumwa. Kwanza, Zanzibar imehusika na biashara hii ikiwa ni kama soko la watumwa tu, na pengine watu maarifu ni akina tipu-tibu ambaye ni muarabu kiasili na bwana liveingstone ambaye ni mzungu. Lakini cha ajaabu, kuwa biashara hii ikifanyika kwenye kanisa kuu la madhehebu ya catholic... sijuwi kuna siri gani.

Sasa kuna watu hupenda kuzungumzia mambo haya ya Utumwa kwa Zanzibar tu na kwa dhana zao kuwa wataweza kuupiga vita u-islamukwa kuonesha Zanzibar ni ksiwa cha wakazi ambao asilimia 99.0% ni Wa-Islamu. Lakini sijuwi kwanini utumwa huu hauzungumzwi ule wa bara, kama bagamoyo na kwengineko. Hazungumzwi ushenzi wa Wa-Jerumani ama Wa-Engereza kama vile wafaransa. Na waathirika wakubwa a mambo ya utumwa ni afrika bara na si visiwani. Kwa mfano Gambia, Ghana, Senegal hata Tanganyika imeathrika kiasi fulani.

Azeni nyinyi Watanganyika kuzungumzia kuhusu utumwa, kwa vile hawa watu ulaya ndio walio kukoseni nyinyi.

Anonymous said...

Mbona GNU imeundwa Zanzibar bila ya pingamizi yeyote ile...na Maalim Seif amekuwa Vice President of Zanzibar...

Kibwengo mkubwa we na spy wa kitanganyika....hufai kuwa na hata hii blog, fala tu we.....
ni kitu gani hasa munachokipigania katika Zanzibar yetu nyinyi watanganika.....
Sisi ni Wazanzibar mukitaka kuleta mambo mengi ya mizengo katika nchi yetu na sisi tunabadilika na kuungana kwa kuliokoa taifa letu kutoka katika koloni la mtanganyika...hamna cha CCM wala CUF sote ni wa ZANZIBAR.

Achaneni na nchi yetu nyie sio mnatufuatilia kama nyie ndio mumetupa uhuru.

Halafu na wewe Kibunango ujitayarishe kuhama Zanzibar urudi kwenu Tanganyika other wise vijana wa kizenji tutakufanyia...hatutaki wanafiki kama wewe katika Nchi yetu.

Anonymous said...

Kama kuna waathirika na biashara ya utumwa tena kwa wingi basi ni Mabara. Sasa ndugi zetu wa Tanganyika hebu anzeni huko Tanganyika kulaani na kutafuta hao walio fanya hiyo biashara ya Utumwa. Tena muanze na ma-chief wenu, utawala wa kijerumani na na huu Malkia wa UK ili tupate ukweli. Nyinyi wazuri wakuzugumzia utumwa lakini kwa Zanzibar tuuuuu. Wacheni choko choko na fitna zenu sisi tushajuwa makosa yetu na kwa uwezo wake Mwenye nguvu, mfalme wa Falme, Mungu wa Haki ambaye ni Allah subuhana wataa-Allah atatupa uwezo wa kuwa kitu kimoja,na kuishi salama salimin Amin Amin Amin