Zanzibar Yaongoza Kwa Ukatili Wa Kijinsia Kwa Watoto.
Hii sio habari njema hata kidogo kwa kisiwa chenye kujitambukisha duniani kama ni kitovu cha ustaarabu na furaha katika mwambao wa Afrika ya Mashariki. Aidha unapozungumzia udhalilishaji wa kijinsia au ukatili kwa watoto kwa hapa Tanzania mara nyingi mikoa ya Tanzania Bara imekuwa ikishika nafasi za juu kulinganisha na Visiwani. Ukatili wa kijinsia unalenga zaidi katika jinsia ya kike, ambapo kumekuwepo na ndoa nyingi chini ya umri, mimba kwa watoto walipo skuli na hata ajila kwa watoto.
Vitendo vya ndoa, ubakaji, ulawiti, ukeketaji na ajila kwa watoto kwa mapana ndio unajenga kuwepo kwa ukatili kwa watoto kwa jinsia zote, hapa nchini.
Taarifa ya kitafiti iliyotolewa na TAMWA hapo siku ya Jumatano tarehe 19.02.2014, imebaini kuwa Zanzibar kuna matukio mengi ya ukatili wa kijinsia ukilinganisha na Tanzania Bara. Hii sio mara ya kwanzakwa TAMWA kufanya tafiti za aina hii hapa nchini, ila kinachosikitisha ni kwa Zanzibar sasa kuongoza katika jedwali la ukatili tofauti na hapo miaka ya nyuma ambapo mikoa kama ya Singida na Mara ilivyokuwa ikishika nafasi za juu katika ukatili huu.
Katika tafiti zilizopita zilitafiti zaidi vitendo vya ubakaji na ulawiti wa watoto huku ukeketaji ukitafitiwa zaidi katika mikoa ya bara. Tatizo la ubakaji na ulawiti kwa Zanzibar linaonekana kupungua kwa mjibu wa Kitengo Cha Uhifadhi Mtoto (Child Protection Unit). Kitengo hiki kilianzishwa mwaka 2010 ambapo kwa mwaka huo jumla ya kesi 141 za ubakaji zikiwemo 30 za ulawiti ziliripotiwa kituoni hapo, kulinganisha na mwaka 2011 ambapo kesi 8 za ubakaji na 2 za ulawiti zilifunguliwa kiyuani hapo, huku mwaka 2012 kesi zikishuka zaidi hadi 6 za ubakaji na moja ya ulawiti, hii ni katika kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Mei.
Wakati tatizo la ubakaji likishuka, tatizo la ndoa na mimba kwa watoto waliopo skuli limeongezeka na kusababisha kuwa kikwazo cha maendeleo kwa mamia ya watoto wa kike visiwani humu.
Katika tafiti ya TAMWA kwa Wilaya ya Kati Unguja na Kusini Pemba kulikuwepo na jumla ya matukio 288 ya mimba za umri mdogo na matukio 42 ya ndoa za umri mdogo. Hali hii inatisha na inatoa pi ha kubwa juu ya ukatili huu kwa watoto wa kike visiwani na inapaswa kutazamwa kwa ukaribu kabisa ili kuondoa tatizo hili Visiwani.
Moja ya sababu ambayo inaweza kuchangia ukatili huu, ni sheria ya sasa inayotoza faini ya Shs 15,000 kwa mzazi/mlezi atakaye muozesha mtoto wake aliyeopo skuli. Zaidihakuna sheria yoyote ambayo inamzuia mzazi/mlezi kumwozesha mtoto ambaye hasomi skuli. Ukiangalia kwa sheria ya ndoa ya mwaka 1971 kifungu cha 13(1) kimeelezea umri wa kuolewa ni mika 15, umri ambao kwa watoto wengi wanakuwa bado wapo skuli. Sheria hii inaweza kutoa mwanya mkubwa kwa ndoa za aina hii na kukatiza maendeleo ya mtoto wa kike.
Kwa upande mwingine wazazi/walezi wamekuwa katika nafasi ya mbele ya kuendeleza kuwepo kwa ndoa aina hii, na vitendo vingine ambavyo vinasababisha kuwepo kwa mimba nyingikwa watoto wa skuli. Malezi duni, uchumi mbovu na tamaa ya wazazi wengi inatajwa kuwa ni moja ya sababu ya kuendelea kuwepo na ukatili huu kwa watoto wao. Hata baadhi ya sheria kama ile ya kuruhusu kwa watoto walipata mimba kuendelea na masomo inaweza kuwa kichecheo kwa watoto hawa kupata mimba kiholel holela. Sheria hii hata hivyo aina sio wengi wameweza kuitumia kwa kurudi skuli baada ya kujifungua.
Pengine ukatili huu unaweza kupunguzwa kwa kiasi kikubwa kupitia Katiba Mpya ya Tanzania inayoendelea kujadiliwa huko Dodoma. Hii imetokana na TAMWA kupendekeza kuwepo na vipengele vya kuzuia ukatiliwa kijinsia katika rasimu ya pili ya Katiba.
Meneja Programu wa kuelimisha demokrasia na KATIBA wa TAMWA, Bi Shufaa Faisal Ubuni, ametaja kipengele kilichoingizwa kwenye rasimu ya pili ya Katiba ibara ya 43, ibara ndogo ya 3 ambacho kinasisitiza wajibu wa kila mzazi/mlezi pamoja na mamlaka ya nchi kuhakikisha kuwa watoto wanalelewa kwa maadili sawa na umri wao.
No comments:
Post a Comment