Zenj Majaribuni tena....
Mwezi ujao tarehe 24, kisiwa cha Zanzibar kitawakaribisha visura wa Afrika kuweka kambi yao kabla ya kuanza safari ya kumtafuta kisura wa Afika(M-Net, Face Of Africa) visiwani humo. Jumla ya visura 24 watakuwepo kwenye kambi hiyo ambayo itaisha kwa kumchagua kisura wa Afrika katika kisiwa hicho. Aidha kwa Visura wa Tanzania watachujwa mapema wiki ijayo kabla ya kujiunga na wenzao 12 kutoka kona nchi kadhaa barani Afrika.
Zanzibar mara nyingi imekuwa ikipinga aina hii ya mashindano, ingawa kwa nyakati tofauti wazenj wamewahi kushiriki katika mashindano ya kutafuta mrembo wa zenj wa kushiriki Miss World. Nakumbuka niliwahi kuona Miss Aspen katika miaka ya tisini huko Zenj ambapo alikuwa akisakwa Miss Zenj, aidha ilikuwa ni vituko tupu, tofauti na jinsi warembo wanavyotafutwa huko Bara.
Wananchi wengi wa visiwani humo hupinga vikali aina yoyote ya ushindanishaji wa wasichana na hasa namna ya ushiriki katika mashindano kama hayo kwa kuwa yanaenda tofauti na maadili ya visiwa hivyo. Kuna wakati Miss Zenj aliwahi kutafutiwa katika mkoa wa Dar baada yakuwepo na upinzani wa hali ya juu kwa mashindano ya aina hii.
Wengi bado wanakumbuka jinsi washichana/wanawake toka Bara na Kenya walivyokuwa wakichezea fimbo huko Zenj na hasa katika mtaa wa Darajani na kundi moja la watoto wa simba. Pamoja na kundi hilo kujulikana hakuna hatua zozote zilizowahi kuchukuliwa dhidi yao na vyombo vinavyohusika kwa mashumbulio yao kwa wanawake ambao walivaa suruali ama sketi au kutovaa hijabu.
Nina mategemeo kuwa kambi hii ya kutafuta kisura wa Afrika haitopata kadhia za kupigwa bakora, kwani nina imani kuwa kambi yao itawekwa nje ya eneo la mji. Aidha ninategemea kuwa waandaji wa mashindano hayo watawapa kanuni za uvaaji kwa wasichana hao iwapo watatembelea huko mjini. Kwa upande mwingine hii ni mojawapo ya nafasi nzuri ya kisiwa hicho kuendelea kujitangaza ndani ya Afrika. Mshindi atakaepatikana hapo nategemea ataondoka na sifa nzuri za Tanzania na hasa Zanzibar kama hatochezea bakora....