Wednesday, 11 April 2007

Tindikali kwa wauza kilaji Zanzibar

Sijui kisiwa kitaendelea vipi katika sekta ya Utalii kama wauzaji vinywaji vikali wataendelea kuteswa namna hii haya mambo yakuchanganya maswala ya kidini na uchumi hayana maendeleo yoyote Somalia mfano.




Wakala mwingine wa pombe amwagiwa tindikali

2007-04-10 10:28:44
Na Mwinyi Sadallah,Zanzibar

Wakala mwingine wa kusambaza pombe Zanzibar, Bw. Chadalal Javed, amemwagiwa tindikali usoni, muda mfupi baada ya kufungua duka lake lililoko mtaa wa Empire mjini hapa.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Mjini Magharibi Bw. Bakar Khatib Shaaban alithibitisha kutokea kwa tukio hilo. Tukio hilo lilitokea jana saa 3:00 asubuhi.

Alisema kwamba mfanyabishara huyo mwenye asili ya Asia, alivamiwa na mtu asiyejulikana, muda mfupi baada ya kufungua duka lake.

``Ghafla mfanyabiashara huyo alimwagiwa kemikali na kumjeruhi sehemu za usoni na tayari amepelekwa jijini Dar es Salaam kwa matibabu zaidi,`` alisema Kamanda Bakari.

Alisema kuwa wakati tukio likitokea, mfanyabiashara huyo alikuwa dukani na mkwewe wakijiandaa kutoa huduma kwa wateja wao.

Alisema hata hivyo, polisi hawakufanikiwa kuchukua sampuli za kemikali iliyotumika, kwa vile baada ya tukio kutokea, wahusika waliharibu mabaki ya kemikali hiyo.

Kamanda Bakari alisema kwamba iwapo wangefanikiwa kupata mabaki ya kemikali hiyo, wangeweza kupeleka kwa Mkemia Mkuu kujua aina ya kemikali iliyotumika.

``Hatufahamu, aina ya kemikali iliyotumika,lakini tunaendelea na uchunguzi kwa kuwa mtu aliyefanya uhalifu huo alifanikiwa kukimbia baada ya tukio,`` alisema Kamanda Bakari.

Mfanyabiashara huyo anamiliki duka la Scorch Store, ambalo linatumika kusambaza pombe Zanzibar katika mahoteli ya kitali, baa na watumiaji wa rejareja Zanzibar.

Kamanda Khatib alisema hilo ni tukio la pili kutokea kwa wamiliki wa maduka ya pombe. Alisema mwezi uliopita mfanyabiashara mwenye asili ya Kiasia, Bw. Kirikti Mandala, alimwagiwa tindikali akiwa dukani kwake eneo la Michenzani.

Alisema kwamba katika tukio hilo watu wawili walihojiwa na polisi, lakini hadi sasa hakuna mtu aliyefikishwa Mahakamani kuhusiana na tukio hilo.

Hivi karibuni baadhi ya wanaharakati wa dini, wamekuwa wakilalamika kuongezeka kwa idadi ya baa katika manispaa ya Zanzibar, kitendo ambacho wanasema ni kinyume na mila na utamaduni wa Mzanzibari.

Mwezi uliopita wanaharakati hao, waliandamana kupinga ongezeko hilo la idadi ya baa katika mji wa Zanzibar, lakini hawakutoa takwimu za ongezeko hilo.

* SOURCE: Nipashe

kibunango

Asante kwa kunikaribisha katika blog hii matata yenye jicho katika vihoja vitokeavyo kisiwani Unguja , napenda kwanza kukutakia safari njema uingereza, na vilevile kutoa ahadi yakujitahidi kucompose as many articles as possible tuko pamoja.
Guidance

Safarini Uingereza

Wapenzi wa kona hii ya Vituko vya Zenj, napenda kuwataarifu kuwa nitakuwa safarini Uingereza kuanzia mwishoni mwa wiki hii..

Kwa miezi kadhaa ijayo nitakuwa na blog tokea jiji la London. Zaidi itakuwa jambo la msingi iwapo nitaweza kukutana na wanablog wa Uingereza...na watanzania wengine ambao ni wapenzi wa blog..

Tuesday, 6 March 2007

Uchovu wa SMZ kwenye masuala ya Umiliki wa Ardhi...

Moja ya matatizo makubwa ya SMZ yapo kwenye masuala ya umiliki wa ardhi. Serikali hiyo ina migogoro mingi kuhusu umiliki na uendelezaji wa ardhi licha ya kuwa na sheria ya Mipango miji/vijiji na Ardhi ya mwaka 1985, Baraza la Manispaa ya mwaka 1995 na Mamlaka ya Hifadhi na Uendelezaji wa Mji Mkongwe ya mwaka 1994.

Sheria hizo zote hapo juu zinasimamia uendelezaji na umiliki wa ardhi, aidha Halmashauri za wilaya nazo kwa upande mwingine zimekuwa zikisimamia uendelezaji wa ardhi. Serikali kuu kupitia kwa Masheha wao nao wamekuwa wakijishughulisha katika masuala ya ardhi.

Katika Mahakama zote visiwani humo kumejaa kesi nyingi za madai ambazo zinahusiana na matatizo ya ardhi.

Leo kanisa la Anglikana huko Zanzibar limekumbushia kadhia yao ya kunyang'anywa ardhi yao na kufanyia mabadiliko ya matumizi. Kimsingi eneo ambalo lina mgogoro ni shule ya msingi Mkunazini ambayo kabla ya mwaka 1964 ilikuwa inamilikiwa na kanisa hilo.

Kinachoshangaza ni hatua ya SMZ kupitia wizara zake kuendelea kubadilisha kinyamela matumizi ya eneo hilo toka eneo la shule na Ibada kuwa eneo la biashara, kwa kuruhusu ujenzi wa maduka katika eneo hilo.

Miaka ya tisini kanisa hilo liliwahi kuomba ruhusa ya kukarabati uzio wa eneo hilo ambao ulikuwa unazama taratibu. Uzio huo unaanzia upande wa mbele ya shule hiyo mkabala na barabara ya Benjamini Mkapa. Kibali cha ujenzi wa uzio huo kilichukua muda mrefu hadi kupatikana. Na kiliweza kupatikana baada ya kanisa hilo kutoa malalamiko mengi kuhusu urasimu wa vyombo vya SMZ.

Ucheleweshaji wa upatikanaji wa Kibali cha Matengenezo ya Ukuta wakati ule sasa ninaweza kuuelewa vizuri. Inaoneka Watendaji wa SMZ walishaona kuwa eneo hilo linafaa kwa kujengwa kwa Vibanda na Viduka vya biashara hivyo walikuwa wanasita kutoa ruhusa ya matengenezo ya ukuta. Na hata walipotoa ruhusa hiyo eneo lilikuwa karibu na shule hiyo halikupewa ruhusa ya ukarabati.

Sasa eneo hilo limejengwa Vibanda vya biashara, na litaendelea kujengwa licha ya maombi ya kanisa hilo kurejeshewa umiliki wa shule hiyo.

Hivi ni nini nafasi ya kuwa na mamlaka ya hifadhi na uendelezaji wa mji mkongwe, iwapo sehemu ambazo zinahitaji kupatiwa hifadhi kutokana na umuhimu wake wa kihistoria, zinashindwa kuhifadhiwa? Kanisa la Anglikana ni muhimu kabisa katika historia ya Zanzibar. Hivyo linatakiwa lipewe nafasi ya ya kuhifadhiwa chini ya Sheria za Mamlaka ya Hifadhi na Uendelezaji Mji Mkongwe.