Monday, 15 September 2008

Ngoma Afrika Band na Ziara yao Ulaya...









Bendi ya mziki wa dansi ya The Ngoma Africa inayoongozwa na mwanamziki nguli Ebrahim Makunja alimaarufu Ras Makunja hilifanikiwa kuufunga mtaa mrefu katikati ya jiji la mji mashuhuri wa Hamburg,katikati ya eneo maarufu hamburg-Haltona,
kulikuwa pata shika ya Nguo Kuchanika wakati bendi hiyo mashuhuri kwa kuwadatisha washabiki hakili na mziki wao wa dansi "Bongo dansi" kutoka Tanzania ukiwa unarindima
Live katikati ya mji katika tamasha kubwa la aina yake Afrika-Festival.

Hilikuwa majira ya saa 2.30 usiku wakali wa mziki wa dansi barani ulaya "The Ngoma Africa band walipanda jukwaani na kuanza kuporomosha nyimbo zao za kiswahili zilizo sindikizwa na mdundo mkali wa dansi ! mziki ambao uliweza kuwazoa mashabiki kwa kasi
ya aina yake na kuwatia kiwewe maelfu ya washabiki katika tamasha hilo.

*Ni Ras Makunja na Bendi ya The Ngoma Africa !
siku hiliyofuatia 30-08-2008 wakali wetu hawa walipanda jukwaa kubwa katikati ya
mji wa Krefeld,katika onyesho kubwa la wiki ya mwafrika (Africa Week) huko nako kuwa
patashika washabiki wamataifa mbali mbali wakiwa wamechanganyikiwa na mdundo wa
dansi wa Tanzania,jukwaa lilikuwa limezungukwa na walinzi wenye suti na miwani meusi,
Ras Makunja na kikosi chake wakiwa jukwaani na kuhakikisha mdundo huo unawamtingisha kila mtu.

Bendi hiyo ambayo imefanikiwa kuwanasa washabiki wa ulaya na mziki wao wa dansi
kutoka bongo Tanzania,inasemekana ndio bendi pekee ya mziki wa dansi iliyoweza kugusa hisia za kila mshabiki,si watoto wala wakubwa,vijana kwa wazee,wake kwa waume,wazungu na weusi hili mradi dansi lao linatingisha.

Taarifa hii imeletwa kwa hisani kubwa na Msema Kweli

Sunday, 14 September 2008

Madawa ya kulevya na Zenj...Watoto matatani!




Matumizi ya madawa ya kulevya huko Zanzibar sasa yamechukua sura mpya ambayo ni mbaya sana na ya kutisha katika historia ya matumizi ya madawa hayo Visiwani humo. Athari za mwanzo kwa jamii ya visiwa hivyo ilikuwa ni pamoja na kuvunjika kwa ndoa, umalaya na wizi. Hatua ya sasa ni kuambukiza watoto wadogo virusi vya ukimwi kwa kuwachoma sindano zenye damu isiyo salama. Huu ni unyama wa aina yake kutokea huko visiwani.

Hadi kufikia mwaka 2001, Zanzibar ilikuwa tayali imepata umaarufu mkubwa wa kuwa bandari ya kupitishia madawa ya kulevya. Umaarufu huu ulisadikiwa kufunika hata umaarufu wa soko la watumwa uliotokea miaka mia mbili iliyopita. Ukuuaji wa biashara ya ya madawa ya kulevya katika Zanzibar ulikwenda sambamba na uporomokaji wa bei ya karufuu katika soko la dunia na kupanda chati kwa biashara ya utalii.

Awali, Zanzibar ilikuwa ni pepo ya wasafiri watumiao Bangi. Hii ilitokana na urahisi mkubwa wa kupatikana kwa bangi visiwani humo. Taratibu madawa mengine ya kulevya yalianza kuingia visiwani na kufikia kilele katika miaka ya tisini.

Zanzibar kuwa pitisho kubwa la madawa ya kulevya katika ukanda wa Afrika ya Mashariki, kunahusishwa sana na mabadiliko ya ya kiutawala huko Afrika ya Kusini, ambapo utawala wa kibaguzi ulifikia kikomo. Ulinzi mkali katika bandari ya Mombasa baada ya ulipuaji wa balozi za USA huko Nairobi na Dar es Salaam ni sababu nyingine inayotajwa ya Zanzibar kuwa kimbilio la kupitishwa kwa madawa hayo. Aidha ubinafishwaji wa Uwanja wa ndege wa Zanzibar katika miaka ya mwishoni ya tisini umetajwa kuchangia kwa kiasi kikubwa kukua kwa upitishaji wa madawa hayo katika Zanzibar.

Matumizi ya madawa ya kulevya yamekuwa yakienda pamoja na uongezekaji wa maambukizi ya virusi vya ukimwi. Hii hasa kwa wale wanaojidunga sindano. Uchunguzi unaonyesha kuwa asilimia 46 ya watumiaji wa madawa hayo hushare sindano, huku zaidi ya asilimia 50 wakifanya ngono (group sex na anal sex) ili kupata madawa hayo. Baadhi ya vijana huweza kutumia hadi US$ 240 kwa mwezi kupta madawa hayo.

Matumizi ya sindano yaliweza kuingia katika sura mpya katika miaka ya hivi karibuni, baada ya kuongezeka kwa watumiaji wasio kuwa na uweo wa kununua madawa hayo. Njia maarufu ya "flash blood" iligunduliwa ambapo mtumiaji wenye nazo mfukoni, hujidunga sindano yenye heroin, na akimaliza kijidunga ufyonza damu yake kutumia sindano hiyohiyo na kumpatia asie na uwezo damu yake ilichanganyika na heroin(diluted). Mchanganyiko huu uweza kumpatia nishai asiye kuwa na uwezo wa kununua herion.

Hali ya sasa ni mbaya mno kama si ya kutisha. Kwani watumiaji wa madawa hayo sasa hupita mitaani na kuwachoma sindano watoto wadogo, sindano hizo ni zile ambazo wanatoka kuzitumia kwa madawa yao ya kulevya, hivyo kuwepo na uwezekano mkubwa wa kuwapatia watoto hao maambukizi ya virusi vya ukimwi. Huu ni unyama mkubwa kabisa katika historia ya matumizi ya madawa hayo pamoja na ugonjwa wa ukimwi visiwani hapo. Kwa ufupi wazazi wengi wapo katika hali ya hofu na hasa wale wanoishi katika mitaa yanye vijana wengi wa kubembea, aidha kwa watoto ni adha kubwa mno kwao kwani inabidi kukaa ndani tu kwa usalama wao...

Saturday, 13 September 2008

Weekend Njema...




Forodhani bado inaendelea kufanyiwa mabadiliko makubwa ambayo yatawezesha kupatikana kwa huduma bora kwa wadau wote watumiao eneo hilo maarufu sana hapo Zenj... Zaidi hata umiliki wa eneo hilo la historia utabadilika na kuwa chini ya Agha Khan Foundation. Kiutawala kuna mengi ndani ya eneo hilo, kuna migongano kati ya Mamlaka ya Mji Mkongwe, Baraza la Manispaa, Idara ya Mipango Miji, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi na Ofisi ya Waziri Kiongozi.. Hata NGO nazo kwa wakati mmoja au mwingine zimeweza kulitaka eneo hilo, mojawapo ni ZAYADESA...Upande mwingine wafanyabiashara hasa wale wauza vyakula usiku nao udai kuwa hilo ni eneo lao.

Lakini cha msingi eneo hilo linafanyiwa ukarabati katika muda muafaka, na ni ukarabati mkubwa kabisa kufanyika katika eneo hilo. Cha msingi ili eneo hilo liendelee kuwa katika mvuto na kupunguza uharibifu baada ya kufunguliwa tena, ni vema kwa sasa wadau wa eneo hilo wakapatiwa mafunzo juu ya kutunza mazingira ya eneo hilo. Hii isisubiri mpaka uchakavu mwingine utakapotokea. Wote tunajua kuwa "Samaki mkunje angali mbichi" Hivyo hatua za makusudi zinapaswa kuchukuliwa sasa kwa kutoa elimu ya utunzaji na matumizi ya eneo hilo kwa wadau wote watumiao eneo hilo kwa njia moja ama nyingine.

Wednesday, 10 September 2008

SMZ Imejichokea....

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Waziri wa kazi na maendeleo ya watoto katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar(SMZ) alinukuliwa akisema kuwa nusu ya wanzibari milioni wenye uwezo wa kufanya kazi hawana kazi. Hii ni kusema asilimia 50 ya watu wenye uwezo wa kufanya kazi hawana kazi. Ni idadi kubwa sana na yenye kutakiwa kufanyiwa kazi. Hesabu hii inajumuisha sekta rasmi na sekta zisizo rasmi visiwani humo.

Kama kawaida wimbo ukawa ni ule ule wa kushaauri kuwa wote wasio na kazi waande makondeni(mashambani) kwa ajili ya kulima, au kwa ufupi wawe wakulima, ila safari hii wimbo huo uliongezewa vionyo vingine kuwa wawe wakulima wa mazao ya biashara. Lakini kila nikijaribu kuangalia idadi ya watu hao na konde zilizopo sasa huko visiwani napata mashaka kama bado hili ni wazo madhubuti la kuondokana na ukosefu wa ajila visiwani humo.

Ikumbukwe kuwa wananchi wengi wa visiwa hivyo walishawahi kugaiwa ardhi kwa ajili ya kilimo, maarufu kama eka tatu. Wakati SMZ ikitoa eka hizo kwa wananchi wake ilikuwa na lengo la kuwafanya wengi wawe wakulima. Hata hivyo ugawaji wake haukuweza au kulenga wale wasio na ajila. Eka tatu hizo kwa sasa ni wachache mno ambao wamendelea kuzitumia kwa shughuli za kilimo, wengi wao walishaziuza kupisha ujenzi wa nyumba za kuishi na biashara.

Zanzibar ni nchi ambayo imekulia katika sekta kubwa ya kibiashara zaidi ya kilimo. Ingawa iliwahi kuvuma sana kwa kilimo cha karafuu, nchi hiyo haijawahi hata mara moja kujitoshereza kwa kilimo cha mazao mengine, pamoja na kuwa mbele sana kwa vifaa na taaluma katika sekta hiyo ya kilimo. Ukiondoa mazao ya Nazi na karafuu na matunda kuna mazao mengi yanalimwa huko kama mpunga ambapo bado kufikia nafasi ya kutosheleza mahitaji ya nchi nzima. Karafuu sasa imeanguka katika soko la dunia, Zao la nazi nalo lipo katika mashaka kutokana na kuongezeka kwa ujenzi wa nyumba. Viwanda ambavyo hapo awali vikitoa ajila kwa wakaazi wengi vingi vimekwisha vungwa na kufutika kabisa katika ramani ya utengenezaji wa ajila visiwani humo.

Kuanguka kwa zao la karufuu kulifungua milango kwa utalii, na serikali hiyo ikaona njia nyingine ya kuongeza pato lake ni kupitia utalii. Kuja kwa utalii kulileta sekta isiyo rasmi ya kutembeza watalii maarufu ka upapasi. Awali ilikuwa ni vita kati ya serikali na mapapasi, hii ilitokana na serikali kukataa kuwatambua hao au kukataa ukweli wa kuwepo na sekta isiyo rasmi visiwani humo. Ilichukuwa muda mrefu kwa mapapasi kuweza kutambuliwa na wizara ya utalii kama ni sehemu mojawapo ya utalii aidha inatoa ajila kwa vijana wa hapo zenj.

Kupanuka kwa utalii Zanzibar kulienda sambamba na ujenzi wa hoteli nyingi za kitalii, hii ilitoa picha kuwepo kwa ajila nyingi visiwani humo. Hata hivyo sio serikali au wananchi wa visiwa hivyo ambao walikuwa wamejiandaa na mabadiliko hayo. Kwani kuanzia kazi za ujenzi ziliwezwa kushika na wageni toka Kenya na baadhi ya watanzania Bara...hii iliianza kutoa malalamiko ya chini chini kuhusu ajila kuchukuliwa na wageni.
SMZ ina hotel zake za kitalii chini ya wizara ya utalii, na ina chuo chake cha utalii hapo Maruhubi,wafanyakazi wachache waliosoma hapo Maruhubi uajiliwa moja kwa moja katika hizo hoteli chache za SMZ Sijui ni kwanini SMZ kupitia wizara na chuo hicho walishindwa kuwavuta wananchi wengi kujiunga na chuo hicho ili kuweza kujipatia ajila katika hoteli lukuki zilizokuwa zikijengwa. mkakati wa kitaifa wa kuona kuwa wananchi wananufaika na hoteli hizo. Hata katikati ya miaka ya tisini wakati SMZ ilipokuwa ikipeleka wanafunzi kusoma nje ya nchi kwa mafungu, idadi ya waliokuwa wakienda huko kwa ajili ya masomo ya utalii ilikuwa ni ndogo mmno kulinganisha na wanafunzi wengine ambao kozi zao zinapatikana kwa wingi katika vyuo kibao Tanzania bara.

Mwishoni mwa miaka ya tisini Zenj iliweza kunufaika na mradi wa miji endelevu, ambao pamoja na mambo mengine ulikuwa na lengo la kutatua kero za wananchi, kwa kuwashirikisha wananchi hao katika kuzitatua. Moja ya mradi ambao uliweza kutengeneza ajila ni ule wa ukusanyaji na utupaji wa taka katika wadi ya Mkele. Ingawa idadi ya walioajiliwa mwanzo wa mradi huu walikuwa kidogo, mradi huu ulilenga kutengeneza ajila kwa wananchi, aidha ukiwa kama mradi kiongozi ulitakiwa kupata kila aina ya msaada ili kuendelea na kupanuka ili wadi na asasi zingine ziweze kuiga mfano na kuweza kutoa ajila kwa wengi. Pamajo na kushirikisha asasi zote tokea Wizara ya Kazi na Maendeleo ya watoto, Tawala za mikoa, Ofisi ya Waziri Kiongozi, ILO na Manispaa ya Mji, mradi huu ulikufa kutokana na baadhi ya Wadau katika asasi hizo kutuupa nafasi ya kuendelea.

Miaka ya elfu mbili, ILO walikuja na wazo jingine la kutoa ajila kwa vijana katika Mji Mkongwe na kama kawaida utashi binafsi wa watendaji wa SMZ mradi huo ulishindwa kufanyika.

SMZ imekuwa kama inawaweka wananchi wake kama rasilimali ya kushinda chaguzi tu, kwani kila ukaribiapo uchaguzi asasi za ulinzi visiwani humo hutangaza ajila lukuki kwa vijana. Ni vema sasa kuangalia sehemu nyingine ambazo zinaweza kutoa ajila kwa utaratibu mzuri na wa kuvutia kama vile uvuvi

Sekta ya uvuvi kwa miaka mingi sijapata kusikia kuwavuta wavuvi wapya kujiunga nao, kama ilivyo kwa sekta ya kilimo. Nina imani kama sekta hii nayo itaweza kupew msukumo kama kilimo ambacho vijana wengi hawapo tayali kujiunga nayo licha ya uchache wa konde zilizopo inaweza kutatua kwa kiasi kibubwa tatizo la ajila visiwani humo. Cha msingi ni namna gani ya kuwashirikisha vijana katika shughuli za uvuvi, kwani soko lake ni kubwa na bado uvuvi unahitaji watu wengi zaidi.

Kwa upande wa utalii ni vema kwa SMZ kutilia mkazo kwa wananchi wake na hasa vijana kusomea fani hiyo, ipo haya ya kupanua chuo kilichopo cha utalii sambamba na mahitaji ya hoteli zilizopo. Nina hakika wenye hoteli hizo watapenda kuajili wazaliwa wa hapo kwani wigo wao wa ufahamu wa visiwa hivyo ni mkubwa kuliko wageni na hili ni moja ya chachundu katika biashara ya utalii. Hili linawezekana kwani bado wazenj wengi hasa wazazi wanamtazamo tofauti sana na utalii.