SMZ Imejichokea....
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Waziri wa kazi na maendeleo ya watoto katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar(SMZ) alinukuliwa akisema kuwa nusu ya wanzibari milioni wenye uwezo wa kufanya kazi hawana kazi. Hii ni kusema asilimia 50 ya watu wenye uwezo wa kufanya kazi hawana kazi. Ni idadi kubwa sana na yenye kutakiwa kufanyiwa kazi. Hesabu hii inajumuisha sekta rasmi na sekta zisizo rasmi visiwani humo.
Kama kawaida wimbo ukawa ni ule ule wa kushaauri kuwa wote wasio na kazi waande makondeni(mashambani) kwa ajili ya kulima, au kwa ufupi wawe wakulima, ila safari hii wimbo huo uliongezewa vionyo vingine kuwa wawe wakulima wa mazao ya biashara. Lakini kila nikijaribu kuangalia idadi ya watu hao na konde zilizopo sasa huko visiwani napata mashaka kama bado hili ni wazo madhubuti la kuondokana na ukosefu wa ajila visiwani humo.
Ikumbukwe kuwa wananchi wengi wa visiwa hivyo walishawahi kugaiwa ardhi kwa ajili ya kilimo, maarufu kama eka tatu. Wakati SMZ ikitoa eka hizo kwa wananchi wake ilikuwa na lengo la kuwafanya wengi wawe wakulima. Hata hivyo ugawaji wake haukuweza au kulenga wale wasio na ajila. Eka tatu hizo kwa sasa ni wachache mno ambao wamendelea kuzitumia kwa shughuli za kilimo, wengi wao walishaziuza kupisha ujenzi wa nyumba za kuishi na biashara.
Zanzibar ni nchi ambayo imekulia katika sekta kubwa ya kibiashara zaidi ya kilimo. Ingawa iliwahi kuvuma sana kwa kilimo cha karafuu, nchi hiyo haijawahi hata mara moja kujitoshereza kwa kilimo cha mazao mengine, pamoja na kuwa mbele sana kwa vifaa na taaluma katika sekta hiyo ya kilimo. Ukiondoa mazao ya Nazi na karafuu na matunda kuna mazao mengi yanalimwa huko kama mpunga ambapo bado kufikia nafasi ya kutosheleza mahitaji ya nchi nzima. Karafuu sasa imeanguka katika soko la dunia, Zao la nazi nalo lipo katika mashaka kutokana na kuongezeka kwa ujenzi wa nyumba. Viwanda ambavyo hapo awali vikitoa ajila kwa wakaazi wengi vingi vimekwisha vungwa na kufutika kabisa katika ramani ya utengenezaji wa ajila visiwani humo.
Kuanguka kwa zao la karufuu kulifungua milango kwa utalii, na serikali hiyo ikaona njia nyingine ya kuongeza pato lake ni kupitia utalii. Kuja kwa utalii kulileta sekta isiyo rasmi ya kutembeza watalii maarufu ka upapasi. Awali ilikuwa ni vita kati ya serikali na mapapasi, hii ilitokana na serikali kukataa kuwatambua hao au kukataa ukweli wa kuwepo na sekta isiyo rasmi visiwani humo. Ilichukuwa muda mrefu kwa mapapasi kuweza kutambuliwa na wizara ya utalii kama ni sehemu mojawapo ya utalii aidha inatoa ajila kwa vijana wa hapo zenj.
Kupanuka kwa utalii Zanzibar kulienda sambamba na ujenzi wa hoteli nyingi za kitalii, hii ilitoa picha kuwepo kwa ajila nyingi visiwani humo. Hata hivyo sio serikali au wananchi wa visiwa hivyo ambao walikuwa wamejiandaa na mabadiliko hayo. Kwani kuanzia kazi za ujenzi ziliwezwa kushika na wageni toka Kenya na baadhi ya watanzania Bara...hii iliianza kutoa malalamiko ya chini chini kuhusu ajila kuchukuliwa na wageni.
SMZ ina hotel zake za kitalii chini ya wizara ya utalii, na ina chuo chake cha utalii hapo Maruhubi,wafanyakazi wachache waliosoma hapo Maruhubi uajiliwa moja kwa moja katika hizo hoteli chache za SMZ Sijui ni kwanini SMZ kupitia wizara na chuo hicho walishindwa kuwavuta wananchi wengi kujiunga na chuo hicho ili kuweza kujipatia ajila katika hoteli lukuki zilizokuwa zikijengwa. mkakati wa kitaifa wa kuona kuwa wananchi wananufaika na hoteli hizo. Hata katikati ya miaka ya tisini wakati SMZ ilipokuwa ikipeleka wanafunzi kusoma nje ya nchi kwa mafungu, idadi ya waliokuwa wakienda huko kwa ajili ya masomo ya utalii ilikuwa ni ndogo mmno kulinganisha na wanafunzi wengine ambao kozi zao zinapatikana kwa wingi katika vyuo kibao Tanzania bara.
Mwishoni mwa miaka ya tisini Zenj iliweza kunufaika na mradi wa miji endelevu, ambao pamoja na mambo mengine ulikuwa na lengo la kutatua kero za wananchi, kwa kuwashirikisha wananchi hao katika kuzitatua. Moja ya mradi ambao uliweza kutengeneza ajila ni ule wa ukusanyaji na utupaji wa taka katika wadi ya Mkele. Ingawa idadi ya walioajiliwa mwanzo wa mradi huu walikuwa kidogo, mradi huu ulilenga kutengeneza ajila kwa wananchi, aidha ukiwa kama mradi kiongozi ulitakiwa kupata kila aina ya msaada ili kuendelea na kupanuka ili wadi na asasi zingine ziweze kuiga mfano na kuweza kutoa ajila kwa wengi. Pamajo na kushirikisha asasi zote tokea Wizara ya Kazi na Maendeleo ya watoto, Tawala za mikoa, Ofisi ya Waziri Kiongozi, ILO na Manispaa ya Mji, mradi huu ulikufa kutokana na baadhi ya Wadau katika asasi hizo kutuupa nafasi ya kuendelea.
Miaka ya elfu mbili, ILO walikuja na wazo jingine la kutoa ajila kwa vijana katika Mji Mkongwe na kama kawaida utashi binafsi wa watendaji wa SMZ mradi huo ulishindwa kufanyika.
SMZ imekuwa kama inawaweka wananchi wake kama rasilimali ya kushinda chaguzi tu, kwani kila ukaribiapo uchaguzi asasi za ulinzi visiwani humo hutangaza ajila lukuki kwa vijana. Ni vema sasa kuangalia sehemu nyingine ambazo zinaweza kutoa ajila kwa utaratibu mzuri na wa kuvutia kama vile uvuvi
Sekta ya uvuvi kwa miaka mingi sijapata kusikia kuwavuta wavuvi wapya kujiunga nao, kama ilivyo kwa sekta ya kilimo. Nina imani kama sekta hii nayo itaweza kupew msukumo kama kilimo ambacho vijana wengi hawapo tayali kujiunga nayo licha ya uchache wa konde zilizopo inaweza kutatua kwa kiasi kibubwa tatizo la ajila visiwani humo. Cha msingi ni namna gani ya kuwashirikisha vijana katika shughuli za uvuvi, kwani soko lake ni kubwa na bado uvuvi unahitaji watu wengi zaidi.
Kwa upande wa utalii ni vema kwa SMZ kutilia mkazo kwa wananchi wake na hasa vijana kusomea fani hiyo, ipo haya ya kupanua chuo kilichopo cha utalii sambamba na mahitaji ya hoteli zilizopo. Nina hakika wenye hoteli hizo watapenda kuajili wazaliwa wa hapo kwani wigo wao wa ufahamu wa visiwa hivyo ni mkubwa kuliko wageni na hili ni moja ya chachundu katika biashara ya utalii. Hili linawezekana kwani bado wazenj wengi hasa wazazi wanamtazamo tofauti sana na utalii.
No comments:
Post a Comment