Friday, 22 May 2009
Monday, 4 May 2009
Avumae Baharini ni Papa.....
Kwa mara ya kwanza vidagaa baharini vimeanza kujiuliza ni nani mkubwa kati ya Papa na Nyangumi, huku wakiwa wamesahau kuwa avumae bahari ni Papa lakini kubwa lao ni Nyangumi..!
Papa ndie anaye aminika kutamba baharini, kwa mwendo wake wa kasi na mashambulizi ya ghafla tena ya kutisha, kiasi ya kumfanya awe ni maarufu sana baharini.
Hivi karibuni katika vita vya mafahali wawili wa baharini, imeonekana kuwa pamoja na ukubwa wa Nyangumi, Papa bado ni maarufu sana kwa ukubwa katika bahari ya maharamia wa meli hadi kule kwa prez asie tumia ndomu. Hata hivyo wataalumu wa mambo wanasema ni nadra sana kwa vidagaa, vibua, ngisi, pweza, changu,tasi na aina nyingine ya visamaki katika eneo hilo kumwona Nyangumi, hivyo kwao Papa bado ndio samaki/mnyama mkubwa kabisa licha ya kuwepo kwa Nyangumi.
Kama vile haitoshi vidagaa hivyo, ambavyo mara nyingi hukaa mbali na Papa, wameendelea kuhoji ni kwa nini Papa ametumia televisheni ya taifa la wanyama wa baharini,kujinadi kama yeye sio mkubwa kama Nyangumi, wakisahau kuwa Papa hana ubavu kama wa Nyangumi ambae ametumia televisheni yake yenye uwezo wa kuonekana live katika eneo lote avumalo Papa!
Kuna taarifa ambazo sio rasmi kuwa Nyangumi atajaa tena kwenye televisheni yake akipinga madai kuwa yenye ndie mtafunaji wa kwanza wa vidagaa na aina nyingine ya visamaki katika eneo hilo la bahari, huku vidagaa vingine vikifanya mpango wa kwenda kwenye maeneo ambayo Nyangumi amekuwa akivuliwa kwa wingi ili kuweza kujionea samaki hilo lipo la aina gani, na kama inawezekana kuliondoa katika eneo lao la bahari, licha ya madai yake kuwa yupo katika kuwatetea vidagaa na umaarufu wa Papa.
__________________
Posted by Kibunango at 18:32 1 comments
Sunday, 26 April 2009
Muungano unazidi kukua, miaka 45 sio mchezo...
Katika kusherehekea miaka 45 ya Muungano nimejikuta nikikumbuka sana shoki shoki, matunda yenye radha ya aina yake ni maarufu sana hapo Zenj. Anyway lengo ni kusherekea muungano, miaka 45 sio mchezo! Muungano huu ambao ulizaliwa na mambo kumi na moja, sasa una mambo 38 na bado una kero ambazo kuchwa zinapigiwa kelele! Sasa cha kujiuliza muungano huu unakua au unapolomoka. Ukiangalia idadi ya mambo yanayounganisha nchi mbili hizi utaona kama unakua na kama unakuwa unaelekea upande gani? Kuunganisha kila jambo na kuwa na serikali moja?
Hata hivyo dalili zinaonyesha kuwa mengi kati ya hayo 38 yameingizwa kwa upande mmoja kuburuzwa na upande mwingine, ndio maana kumezaliwa neno kero za muungano! Kwa hali ya sasa dalili za kukua kwa muungano huu ni kidogo kuliko kukua kwa kero zake! Nini kifanyike? yarudishwe yale 11 ya mwanzo au haya ya sasa yajadiliwe kwa kina na kuondoa hizo kero. Je ni upande mmoja tu wa muungano ambao unaona kuna kero? na kama ni hivyo upande mwingine wa muungano unajisikia vipi kukaa kimya na kutosikiliza kero za upande mwingine? Ni kiburi ama dharau? Au kuna ajenda ya siri?
Nawatakiwa kila heri watanzania wote katika siku hii muhimu ya kuzaliwa kwa Tanzania.
Posted by Kibunango at 17:59 1 comments
Saturday, 18 April 2009
Kisauni Airport kuongezwa kwa mita 560
Zanzibar International Airport maarufu duniani kama Kisauni Airport inatazamiwa kuongezwa urefu wa njia yake kwa mita 560. Ni katika mradi uliopatiwa fedha na Benki ya Dunia.
Uwanja wa Kisauni umekuwa ukifanyiwa matengenezo mara kwa mara, ili kukidhi ongezeko la matumizi ya uwanja huo na hasa baada ya kukua kwa sekta ya utalii visiwani humo.
Matengenezo haya yatajumuisha ukarabati wa jengo la uwanja pamoja na utiaji wa uzio katika baadhi ya maeneo ya uwanja huo ambayo yapo hatarini kuvamiwa kwa ujenzi wa nyumba za kuishi. Aidha kampuni itakayofanyia matengezeno uwanja huo Sogea Satom ya Ufaransa imenukuliwa ikisema kazi hiyo itachukua muda wa mwaka mmoja na miezi mitatu kukamilika.
Posted by Kibunango at 22:17 4 comments