CUF kusherehekea ushindi
Wakati hali ya kisiasa Visiwani ikiingia katika historia mpya, taarifa zilizopatikana mjini hapa zimedai kuwa Chama cha CUF kinafanya maandalizi ya kusherehekea ushindi baada ya kufanikiwa kuwashawishi baadhi ya vigogo wa CCM Zanzibar kukubali kuundwa kwa Serikali ya mseto kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu uliopangwa kufanyika mwezi Oktoba.
Katika maandalizi hayo ambayo inasemekana yanafanyika kwa usiri mkubwa, viongozi wa CUF wanaelezwa kukubaliana na mapendekezo ya Baraza la Mawaziri ambalo litajumuisha na wenzao wa CCM katika Serikali ya muda itakayoongozwa na Rais wa sasa wa Zanzibar, Amani Abeid Karume.
Chanzo cha habari hizi kimedai kuwa chini ya mapendekezo hayo, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad atakuwa Waziri Kiongozi nafasi ambayo kwa sasa inashikiliwa na Shamsi Vuai Nahodha ambaye anakusudiwa kutupwa nje ya Baraza jipya la Mawaziri.
Wengine waliopendekezwa na Wizara zao zikiwa kwenye mabano ni Mansoor Yussuf Himid–CCM (Mafuta na Nishati), Samia Suluhu Hassan-CCM (Afya), Juma Dui Haji – CUF (Biashara Utalii na Uwekezaji), Nassor Mazrui-CUF (Fedha), Dk. Mwinyihaji Makame Mwadini-CCM( Kilimo, Ardhi na Maji).
Wengine ni Fatma Abdulhabib Ferej-CUF (Wanawake, Watoto Maendeleo ya Vijana), Burhan Saadat Haji-CCM (Mawasiliano), Machano Othman Said-CCM (Waziri wa Tawala za Mikoa na Vikosi Maalum), Asha Abdulla Juma-CCM (Elimu), Abbas Juma Muhunzi-CUF( Ofisi ya Waziri Kiongozi), Ali Juma Shamuhuna – CCM (Ofisi ya Rais).
Kiongozi wa Upinzani katika Baraza la Wawakilishi, Abubakar Khamis Bakar amependekezwa kuwa Waziri wa Katiba na Utawala Bora.
Chanzo hicho kimedai kuwa mapendekezo hayo ya Baraza la Serikali ya muda yamekuwa yakisambazwa kwa vigogo wa CUF tu ikiwa ni ishara kwao ya ushindi wa suala walilokuwa wakilitaka la kuwepo ndani ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Pamoja na hali hiyo, kundi la wajumbe ambao wanapinga harakati hizo ni kubwa na ambalo linaundwa na wanasiasa wenye ushawishi mkubwa wa siasa za Tanzania na kwa namna hali inavyokwenda kikao hicho cha Kamati Maalum kitatawaliwa na vijembe vingi na upinzani mkali kwa watu waliopachikwa jina la ‘Uhafidhina’.
Tayari Kiongozi wa Upinzani katika Baraza la Wawakilishi Abubakar Khamis Bakar ameshawasilisha hoja binafsi kwa Katibu wa Baraza akitaka kufanyike marekebisho ya katiba yatakayoruhusu kubadilisha mfumo wa utawala wa SMZ kwa kuwa na Serikali ya mseto.
Idadi kubwa ya wafuasi wa CCM na viongozi wamekuwa wakipinga suala la kuongezwa muda kwa Rais Karume pamoja na kuwepo kwa Serikali ya mseto Zanzibar wakidai kuwa mazingira hayaruhusu kwa uundwaji wa serikali hiyo na kusisitiza msimamo wa utekelezaji wa azimio la CCM Butiama.