Wednesday, 8 October 2008

Mbolea ya Mboji katika mjadala


Waalimu wawili wakuu wa shule ya Msingi za Kahama na Kirumba pamoja na Mwalimu toka shule ya msingi Isenga, wakifuatana na Mratibu wa Mradi wa Tampere - Mwanza wametembelea chuo cha TAMK Tampere kujadili maendeleo ya mradi wa utengenezaji wa mbolea katika shule zao jioni ya leo. Pichani Waalimu hao wakitoa maelezo juu ya mradi huo ambao kwa ufupi umekuwa ni wa mafanikio makubwa.

Aidha wanafunzi wa TAMK walipata kutoa shukrani zao juu ya ushirikiano mkubwa wakati wa uanzishaji wa mradi huo wa aina yake wenye lengo la kuwashirikisha wanafunzi katika utengenezaji wa mboji.



Hadi sasa shule zote tano ambazo zipo kwemye mradi huu zimefanikiwa kuzalisha mbolea hiyo, huku shule ya msingi ya Isenga ikiwa tayali imeanza kutumia mbolea hiyo kwa upandaji wa miti katika shule yao. Mwalimu toka Isenga alisema kuwa mafanikio hayo yameanza kuvuka mipaka ya shule hiyo kwa baadhi ya wakaazi wa karibu na shule hiyo kuanza kutengeneza mbolea ya mboji.

Mipango ya baadae ni kuendelea kutoa elimu ya utengenezaji wa mboji kwa shule nyingi zaidi katika Jiji la Mwanza. Aidha kutoa nafasi kwa wanafunzi na wananchi wa jiji hilo kupitia vikundi kazi kutembelea jiji la Tampere ili kutoa ujuzi wao wa kutengeneza mbolea kwa wakaazi wa jiji la Tampere. Hii itakuwa ni nafasi nzuri zaidi kwao, kwani matumizi ya artificial fertilizer yanategemewa kupungua kwa kasi katika nchi ya Finland kutokana na kuongezeka kwa bei yake kwa kiwango cha asilimia 300.

Kwa upande wa TAMK wanafunzi wameonyesha kulidhika sana na mradi huo kiasi kwamba idadi ya wanafunzi wanaotegemewa kwenda kwenye awamu ya pili ya mradi huo imeongezeka. Hii ni changamoto kwa Jiji la Mwanza kuandaa shughuli nyingi kadili ya idadi ya wanafunzi hao ili kuweza kunufaika vema na utaalamu wao.

Tuesday, 30 September 2008

Idd Mubaraka


Napenda kuwapa mkono wa idd wadau wote wa blog hii. Sikukuu njema

Monday, 29 September 2008

Wanafunzi na Mazingira...Case: Mwanza





Mazingira ya shule ya Msingi Igoma. Shule hii ina klabu ya mazingira ya wanafunzi na moja ya kazi zake ni kutunza mazingira ya shule hiyo.




Wanafunzi wa shule ya Msingi Kirumba wakiandaa shimo kwa ajili ya utengenezaji wa mbolea kwa taka za jikoni. Klabu ya Mazingira katika shule hiyo hujishughulisha na usafishaji wa mazingira katika kata yao ya Kirumba.


Uandaji wa mashimo kwa ajili ya kutengeneza mboji kutokana na taka za jikoni, katika shule ya Msingi Isenga

Wednesday, 24 September 2008

Chumbe...Na sifa zake





Chumbe ni kisiwa chenye ukubwa wa hekta 20 na kipo umbali wa kilomita 6 toka Mji Mkongwe - Zanzibar. Ni rahisi sana kukiona kisiwa hiki ukiwa unaingia ama kutoka Zanzibar kwa njia ya bahari... aidha iwapo unaingia kwa njia ya anga unaweza kukiona kisiwa hiki kilichojaliwa utajili wa mazingira ya baharini.

Umaarufu wa Chumbe kwa wakaazi wengi wa Zenj hautokani na umaarufu unaojulikana duniani kote katika mazingira ya kisiwa hicho, bali ni kutokana na kauli za viongozi wa kisiasa wa visiwa hivyo wakitumia kisiwa hicho kama mpaka wa mambo mengi ya kisiasa baina ya Zanzibar na Tanzania Bara. Viongozi wengi kuanzia Marehemu A.Karume, rais wa kwanza wa visiwa hivyo amehawi kunukuliwa akisema baadhi ya mambo ya Tanzania Bara mwisho wake ni Chumbe.... na wengi kwa wakati tofauti wamekuwa wakiendelea kutumia kisiwa hicho kutenganisha mambo ya SMZ na JMT.... Pengine hata sasa kwenye sakata la mgao wa mafuta wengi watadai kuwa JMT mwisho wao ni Chumbe...

Zaidi ya mambo ya kisiasa kisiwa hicho kinajulikana duniani kama ni kisiwa cha kwanza duniani kuwa na "Coral Park" inayomilikiwa kibinafsi, kisiwa cha kwanza katika Tanzania kuwa na "Marine Park" aidha ina hoteli ambayo ipo kwenye hoteli 20 bora duniani kimazingira "Eco Hotel". Zaidi, kisiwani humo unaweza kuwaona kobe kadhaa, na kuna kobe mwenye miaka zaidi ya 125 ndani ya kisiwa hicho.. Zaidi kisiwa hicho kimewahi kushinda tuzo ya British Airways- Tourism for Tomorrow, mwaka 2000