Monday 25 December 2006
Saturday 9 December 2006
Athari za Wizara kung'ang'ania madaraka....
Wakati mamilioni ya Watanzania leo hii wanasherekea siku ya uhuru wa Tanganyika, Huko Zanzibar, suala la uchafuzi wa Mazingira limechukua sura mpya. Hii ni baada ya wizara ya maji, ujenzi, nishati na ardhi kutangaza kuwa hapatakuwa na ruhusa kwa mwekezaji kujenga hoteli pasipo kuwa na water treatment plant na sehemu ya kuchomea taka ngumu ( incinerator).
Tatizo la utupaji wa taka ngumu na taka maji katika ukanda wa hoteli za kitalii na hasa maeneo ya mashariki na kaskazini ya kisiwa hicho yapo kwa muda mrefu sasa. Hoteli nyingi kubwa na ndogo zimekua zikitupa taka zao kwa njia wanazojua wao wenyewe. Kuna hoteli ambazo zimekuwa zikitupa taka ngumu moja kwa moja baharini, wengine kuzichimbia ardhini na wapo waliokuwa wanazichoma sehemu ya mbali toka katika maeneo yao. Hali kadhalika taka maji zimekuwa zikitupwa moja kwa moja baharini na kwenye maeneo ya karibu na bahari.
Matatizo ya kukosekana kwa mfumo wa utupaji wa taka na hasa nje ya halmashauri ya manispaa ua zanzibar, yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na baadhi ya wizara kung'ang'ania madaraka na hasa kwenye maeneo nyeti ya ardhi na uwekezaji. Kimsingi Mamlaka ya Maji huko visiwani inashughulika na usambazaji wa maji safi tu katika visiwa hivyo, huku jukumu la maji taka likiwa chini ya halimashuri ya manispaa ya zanzibar..ambayo ina eneo dogo tu la utawala. Zaidi hata katika eneo hilo dogo la kiutawala, haina sauti kisheria juu ya usimamiaji wa maji taka katika hoteli ambazo zimejengwa ndani ya Manispaa hiyo. Vyombo vinavyohusika hapo ni ZIPA na Idara ya Upimaji na Mipango Miji. Cha kushangaza hata Idara ya Mazingira imekuwa ikiwekwa pembeni mno kuhusu shughuli nyingi za uendelezaji wa ardhi katika visiwa hivyo.
Baada ya Miaka kumi na sita ya uendelezaji wa Mahoteli ya kitalii katika fukwe za visiwa hivyo pasipo na mfumo wowote wa utunzaji wa mazingira, athari zake sasa zimeanza kuoneka wazi. Hoteli hizo hazina mfumo wowote wa kusafisha maji taka kabla ya kuyamwaga baharini na hakuna sehemu maalumu ya utupaji wa taka ngumu katika maeneo ya hoteli hizo. Kila mwenye hoteli anafanya chochote atakachoweza katika kutupa taka zake.
Haya yote yametokana na baadhi ya wizara kung'ang'ania kila kazi, Kwa mfano jukumu la Idara ya Mazingira katika uwekezaji na katika suala zima la maendeleo hasa katika sekta ya ujenzi halijulikani. ZIPA ikishirikiana na Idara ya Mipango Miji/Vijiji wameshindwa kuonyesha ni kwa nanma gani taka zinazozalishwa kila siku katika mahoteli hayo zitakavyoweza kuhifadhiwa, kutupwa au kutumika tena, na mbaya zaidi haijulikani ni mamlaka ipi inayoshughulikia maji taka nje ya Manispaa ya zanzibar.
Iwapo ZIPA na Idara ya Mipango Miji/Vijiji ndio wanaochukua kodi za uanzishwaji wa mahoteli ya kitalii inawapasa wawajibike na kupanga mfumo unaoeleweka ukusanyaji na utupaji wa wa taka katika Maeneo ya hoteli. Ushirikishwaji wa mamlaka za serikali za mitaa katika maeneo hayo pamoja na idara ya mazingira lazima utazamwe upya.
Posted by Kibunango at 15:50 0 comments
Monday 20 November 2006
SMZ na Vilabu vya Pombe...
Pengine ni Zanzibar pekee katika Afrika Mashariki ambako unaweza kukuta Mahakama ya Vileo. Mahakama hii hufanya kazi chini ya Waziri wa Tawala za Mikoa, ikiwahusisha Wafanyakazi toka katika Mahakama ya wilaya, Baraza la Manispaa na Waombaji wa leseni ya kuuza vileo katika kisiwa cha Zanzibar.
Mahakama hii ipo siku nyingi zaidi ya uhai wa SMZ yenyewe, aidha imekuwa ikizidi kupata umaarufu siku za karibuni, ambako kumekuwepo na pingamizi za wazi kuhusu uhanzishwaji wa vilabu vya pombe na suala zima la unywaji pombe visiwani humo.
Pingamizi kubwa toka kwa wananchi ni kwamba vibalu vingi vimekuwa vikianzishwa karibu na nyumba za ibada na sehemu za maakazi ya watu. Hivyo kuwepo na kero kwa wananchi kutokana na kelele za wanywaji au pilikapilika za kwenye vilabu hivyo.
Hata hivyo sio wananchi wengi ambao wanajua shughuli za Mahakama hii, hivyo wengi wao huishia kutupa lawama zao kwa Baraza la Manispaa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa. Kwa ufupi Mahakama hii hukutana mara moja kwa mwaka kupitisha maombi yote ya uanzishaji wa biashara ya ulevi, kuongeza muda kwa lesini za biashara ya ulevi, kufuta lesini zilizoshindwa kufuata utaratibu n.k Mahakama hii haiusiki na utoaji wa vibali vya ujenzi wa nyumba za ulevi.
Hivi karibuni Mh. Waziri wa Tawala za Mikoa Visiwani humo aliitaka mahakama hiyo kutotoa leseni kwa vilabu vya ulevi vilivyopo karibu na Maakazi ya watu na nyumba za ibada, na ni baada ya kuwepo kwa malalamiko mengi toka kwa wananchi.
Pengine ni wakati ambao tunapaswa kujiuliza kuwa ni sehemu zipi za maakazi ya watu, ni sehemu zipi za biashara ni sehemu zipi za elimu ni sehemu zipi za viwanda na ni sehemu zipi za kilimo ndani ya kisiwa hicho. Kwa haraka haraka sio rahisi kujua hilo na hasa ikizingatiwa hali halisi ya mpango wa mji wa kisiwa hicho. Hata ukiangalia master plan ya Mwaka 1982 chini ya Sheria ya Ardhi ya mwaka 1985, haikuweza kuweka bayana sehemu maalumu kwa ujenzi na uendeshaji wa biashara ya ulevi. Masterplan hiyo ilitenga maaeneo ya Maakazi, Viwanda na Elimu tu. Hivyo basi leo hii kusema kudai kuwa Vilabu visiwe katika maaneo ya wakaazi sio sahihi.
Zaidi wenye vilabu na wanywaji wa ulevi katika kisiwa hicho, ni wastaraabu sana na ni watu ambao wanajua kuheshimu uhumimu wa kuheshimu Majirani zao, iwe ni sehemu ya Ibada au Maakazi ya watu.
Kwa mfano, kila inapokaribia adhana, basi redio au muziki ndani ya kilabu huzimwa hadi adhana inapokwisha. Kwa maelewano mazuri kati ya wenye baa na baadhi ya misikiti iliyokaribu na baa hizo huweza kusaidiana huduma ya maji, na hasa kwa waumini kwenda kutawadha katika baa pasipo usumbufu wowote. Hivyo ni vema kuendelea kuheshimu uungwana wa walevi wa visiwa hivyo ambao ulevi wao ni wa kistaarabu kuliko walevi wa nchi nyiongi dinuani
Posted by Kibunango at 00:08 5 comments
Sunday 19 November 2006
eka Tatu
Kuna kauli moja iliwahi kutolewa na rais wa awamu ya nne katika SMZ kuwa Zanzibar ni "Njema na kila atakae kuja basi anakaribishwa" Kutokana na kauli hiyo Zanzibar ilishuhudia mabadiliko ya nguvu katika sekta zote kuanzia ya kibiashara,kijamii na kadhalika. Mamia ya watu walianza kufanya biashara wageni wakiongezeka na kuufanya mji wa zanzibar kuwa mdogo kutokana na msongamano wa watu.
Kuingia kwa awamu ya tano kulishuhudiwa na mabadiliko makubwa zaidi,mabadiliko haya zaidi yalikuwa katika kuendeleza ardhi ya zanzibar. Hapa inabidi tukumbuke kuwa ardhi yote ya Visiwa vya Zanzibar ni mali ya serikali. Hivyo ili uweze kuendeleza ardhi hiyo ni shurti uwe na hati ya kumiliki ardhi hiyo toka serikalini. Katika awamu ya tano kulikuwa na wimbi kubwa la ujenzi wa nyumba za kuishi na mahoteli, kutokana na kuwa serikali ndio mmiliki wa ardhi kwa kiasi kikubwa ilishindwa kukidhi maombi mengi ya viwanja. Hili likawa ni tatizo kubwa na tena kubwa sana. Hadi mwaka huo tayali mji wa zanzibar ulikuwa unafuata mapendekezo ya mastertplan ya wachina ya mwaka 1982 iliyotiliwa nguvu na sheria ya upimaji miji na ardhi ya mwaka 1985. Master plan hiyo iliongeza ukubwa wa mji wa zanzibar na ilikuwa imeshatenga maeneo ambayo serikali ilitakiwa kuyaendeleza aidha kwa kujenga nyumba au kugawa ardhi hiyo kwa wananchi wanaotaka kujenga nyumba. Hilo halikufanyika na kama lilifanyika basi ni kwa kiwango kidogo sana. Maeneo hayo yaliyopimwa na kuonyeshwa kwenye master plan ni pamoja na eka tatu ambazo zilitolewa na serikali ya awamu ya kwanza na ya pili kwa lengo la kuwapatia wananchi wa visiwa hivyo sehemu za kulima. Katika awamu hizo wananchi wengi walikuwa wanaishi katika maeno ya umbali wa maili tano kuzunguka mji. Eka tatu karinu zote zilikuwa nje ya mji na ziliguswa na master plan.
Kutokana na mabadiliko ya kiuchumi na mahitaji makubwa ya ardhi kwa ajili ya ujenzi, eka tatu taratibu zilianza kujengwa. Ilikuwa ni kazi ya ziada kujenga katika eka hizo ukizingatia kuwa ardhi ni mali ya serikali. Hata kupitia Mambo msige ambao wao pia wanatoa hati ya kumiliki mali, wananchi waliona huko ndiko kwepesi kwa kupata hati ya kumiliki ardhi.Hivyo wananchi walianza kujenga misingi ya nyumba katika heka hizo na baadae kuziuza na serikali kupitia idara yake ya mambo msige kuidhinisha na kuthibitisha uuzaji na uendelezaji wa ardhi hiyo ambayo awali ilikusudiwa kuwa ni ya kilimo. Vita kati ya idara za serikali ukaanza taratibu kati ya idara ya Ardhi na Idara ya Mambo msige, huku serikali kuu ikikaa kimya.
Leo katika kusoma gazeti nimekutana na kauli ya Waziri wa Waziri wa Maji, Ujenzi na Ardhi Bw. Mansour Yussuf Himid akisema kuwa smz itabomoa nyumba zote zilizojengwa kwenye eka tatu. Kauli hii kwa kweli imenitisha mno. Na ni kauli nzito sana kwa waelfu ya wakaazi wa Visiwa hivyo. Kwani kwa namna moja ama nyingine watakaoadhirika na bomoabomoa hiyo ni wengi, na ni kuanzia kwenye mahoteli yote ya kitalii yaliyojengwa baada ya mwaka 1985, viwanda na maelfu ya nyumba za kuishi.
quote:
--------------------------------------------------------------------------------
’’Tutabomoa nyumba zilizojengwa kwenye ardhi za ekari tatu zilizotolewa kwa wananchi baada ya Mapinduzi,’’ alisisitiza Waziri.
--------------------------------------------------------------------------------
Posted by Kibunango at 15:32 0 comments