Karume Boys hamna aibu?
Karume Boys imepewa jina hilo baada ya rais wa Zenj kujitosa katika kudhamini mchezo wa mpira wa miguu huko visiwani na hata katika ngazi ya afrika ya mashariki na kati. Rais huyo amekuwa mstari wa mbele kusimamia mchezo huo kwa kuhakikisha kuwa timu za Taifa kama hii ya vijiana wa umri chini ya miaka 17 wanashiriki katika mashindano makubwa.
Kwa kufanya hivyo nina imani kuwa lengo la rais ni kuwajenga vijana hao kimchezo tokea wakiwa vijana ili waje kuingia kwenye timu za wakubwa wakiwa na uzoefu mkubwa katika mchezo huo.
Kilichotokea hivi karibuni huko Burundi, kinatia shaka na kinyaa katika medani ya soka visiwani humo. Kuna tuhuma kuwa vijana hao waliuza mechi kwa jirani zao wa Kenya, ili timu hiyo ya Kenya iweze kuingia hatua ya nusu fainali. Kuuza mechi za kitaifa kwa kweli kunatia shaka sana na kama ni kweli basi itakuwa ni hujuma mbaya kabisa kutokea katika fani hii ya kusakata kabumbu katika visiwa hivyo na hata kwa Tanzania kwa ujumla.
Nikirudi nyuma kuangalia maandalizi ya timu hiyo na safari yake ya Burundi yalikuwa ni ya kusuasua na hasa katika suala zima la gharama za timu hiyo kuanzia kambini kwao hadi nauli ya kwenda huko.
Kuanzia timu za Taifa, hadi kwenye vilabu vya Zenj vimekuwa na tatizo la udhamini, hivyo kufanya kuitegemea zaidi serikali katika kushiriki mashindano ya kimataifa. Rais huyo wa Zenj nina hakika alikubali kuanza kudhamini timu hiyo kutokana na kukosekana kwa wafadhili wenye ridhaa ya SMZ. Kwani sio kila mfadhili hukubalika huko Zenj. Hali ya sasa ya udhamini wa soka, na hata uwezo wa vilabu vya soka huko visiwani ni wa kutia shaka, na hii inadhibitishwa na klabu bingwa ya visiwa hivyo timu ya Miembeni kutaka kujitoa au kuuza nafasi yao ya kushiriki mashindano ya klabu bingwa afrika, kutokana na kukosa fedha za kugharamia maandalizi na ushiriki wa mashindano hayo. Hata yule mfadhili wao ambae aliweza kuwaingiza wapenzi wa Miembeni na watu wengine bure kujaza uwanja wa Amani amejitoa kuidhamini timu hiyo katika mashindano hayo muhimu.
Tatizo kubwa la soka visiwani huko ni kukosekana kwa wafadhili. Kipindi kile cha Mzee Ruska, timu za Zenj zilikuwa zikitamba sana, na ilitokana na kuwa na wafadhili. Kwa mfano timu ya Malindi iliweza kununua wachezaji nyota wa timu ya Taifa ya Zambia, kuchezea timu yao, zaidi waliweza hata kuleta wachezaji toka Ulaya ya Mashariki. Mlandege nayo haikuwa nyuma katika kuwakilisha vizuri visiwa hivyo, ambao wachezaji walikuwa wakilipwa kama ni wachezaji wa kulipwa.
Kuanguka kwa ufadhili wa mtu mmoja mmoja kulifungua ukurasa kwa makampuni makubwa kama ya Bia kuingia katika anga za soka. Hata hivyo SMZ ilipinga vikali udhamini wa makampuni ya Ulevi... Kwa kudai kuwa unakwenda kinyume na maadili ya Nchi. Taratibu vilabu vilianza kudorola na hata kufikia kwa timu ya Taifa.
Kilichotokea huko Burundi kinawezekana kutokana na hali halisi ya maandalizi ya timu hiyo. Inaonekana kuwa timu hiyo haikuwa na motisha wa aina yoyote zaidi ya kushiriki mashindano hayo ili siku ipite na warudi makwao. Timu hiyo inawezekana ilikuwa katika hali ngumu kimaisha huko, kiasi ikiwa ni rahisi kurubuniwa ili kudhibiti njaa zao.
Waziri kiongozi nae aliona hali ngumu ya ufadhili kwa timu hiyo, na kabla ya timu hiyo kwenda huko Burundi alinukuliwa akisikitishwa na wafadhili kutojitokeza kuidhamini timu hiyo. Hayo, pamoja na mengine itakuwa ni busara kusubiri uchunguzi wa ZFA dhidi ya timu hiyo. Aidha itakuwa ni jambo la mbolea kwa ZFA kutujulisha matokeo ya uchunguzi wao. Ambao utatuwezesha kujua kipigo cha magoli matano kilikuwa ni kuzidiwa kimchezo au hujuma!
No comments:
Post a Comment