TANZANIA Food and Culture
Na Mwandishi Wetu
TANZANIA imepata fursa pekee miongoni mwa nchi za bara la Afrika, kushiriki Tamasha la Chakula litakalofanyika mwisho wa mwezi huu mjini Conwy, Wales.
Katika taarifa ya mratibu wa tamasha hilo la chakula, Gloria Mutahanamilwa, hiyo itakuwa fursa kwa Tanzania kujitangaza katika nyanja mbalimbali za utali, utamaduni, biashara, uchumi, kilimo, uvuvi na nyinginezo.
"Hili ni tamasha la chakula ambacho ni kitu kinachopewa umuhimu zaidi, lakini tutajumuisha mambo mengine mbalimbali kupitia tamasha hilo, kuna uwezekano wa kufungua njia kwa Tanzania katika kushirikiana na nchi nyingine kupitia nyanja tofauti" alisema mratibu huyo.
Katika tamasha hilo, ujumbe wa Tanzania wa watu takriban 25 pia utahusisha wacheza ngoma, wapiga muziki na wapishi.
Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Mwanaidi Maajar anaunga mkono jitihada hizi na amethibitisha kuhudhuria tamasha litakaloonyesha vyakula, mapishi, utamaduni na vivutio pamoja na kutoa malelezo kuhusu Tanzania.
Tamasha hilo litafanyika katika mji wa kihistoria wa Conwy uliopo Wales kwa siku mbili yaani Oktoba 27 na 28, mwaka huu na inakadiriwa watu 20,000 toka kona mbalimbali za dunia watahudhuria kwani Conwy ni miongoni mwa miji mikuu ya kihistoria na kitalii.
"Ushiriki wa Tanzania ni wa kujitolea, wajumbe wote wanajitolea lakini bado kuna gharama nyingi ili Tanzania tuwakilishwe ipasavyo," alisema mratibu na kuhimiza watu binafsi na taasisi mbalimbali kuchangia na pia kushiriki.
Taarifa zaidi kuhusu TANZANIA Food and Culture zinapatikana kwenye tovuti yao kwa kubonyeza hapa au kwa kuwasiliana na wandaaji,
Tanzania Centre UK kwa barua pepe tanzaniacentre@hotmail.co.uk au
simu +447745891595.
No comments:
Post a Comment