Tuesday 15 February 2011

Ni katika kusherehekea miaka 50 ya uhuru wa Tanzania na miaka 100 ya siku ya mwanamke duniani


Ni onyesho la wazi, bure na la aina yake mara ya Kwanza nchini.

Itakuwa ni kampeni ya utu mwanamke na uzazi salama

Wadhamini waombwa kujitokeza kusapoti uzazi salama Tanzania



Katika kusherehekea miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania, na miaka mia moja ya siku ya mwanamke kimataifa, mbunifu nguli wa mavazi Tanzania, Mustafa Hassanali aliyebobea katika ubunifu wa mavazi ya jioni na Harusi, kwa kushirikiana na wabunifu waalikwa wa kimataifa toka Uingereza watafanya maonyesho ya mavazi tarehe 4-5 mwezi Machi mwaka huu, kwa lengo la kusaidia suala zima la uzazi salama nchini.

Akizungumzia maonyesho hayo, Mustafa Hassanali, ambae anaamini katika kuitumia mitindo kama njia mbadala ya kuchangia, kuhamasisha na kueneza taarifa kwa jamii zinazohusiana na masuala ya afya amesema”kwa kushirikiana na shirika la utepe mweupe la Tanzania kwa pamoja tumeamua kufanya maonyesho ya mavazi kwa siku mbili, lengo si tu kuonyesha mavazi ya Mustafa Hassanali kwa mwaka 2011, na utu mwanamke, bali pia kuhamasisha uzazi salama nchini”.

‘Kila dakika moja dunia inapoteza mwanamke mmoja kwa matatizo ya uzazi, tunahitaji kufanya mabadiliko hususani katika kipindi hiki ambacho dunia inasherehekea miaka mia moja ya siku ya mwanamke, na taifa pia la Tanzania likitimiza miaka 50 toka uhuru, hivyo hatuna budi kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha tunampa mchango mwanamke katika suala zima la afya ya uzazi” alisema Mustafaa Hassanali.

Mustafa Hassanali, mwenye elimu na uelewa mzuri wa udaktari, ambae ndie alieanzisha mpango wa ‘Fashion 4 Health’, mpango ambao umefanya maonyesho ya mavazi katika kusaidia masuala mbalimbali yahusuyo afya toka mwaka 2008, na moja kati ya harakati zake, ni pamoja na ile ya kuchangia hospitali ya wenye matatizo ya akili huko Zanzibar, ambapo kiasi cha shilingi milioni 23 zilipatikana kutokana na mradi huo.


Akiwa kama nguli wa mitindo Afrika Mashariki na kati, na mwenye nia ya kuiweka fani hii ya mitindo mbele, Mustafa Hassanali alisema”tunatarajia kufanya onyesho la wazi kwa tarehe tano ya mwezi wa tatu, hii itasaidia kuipa nafasi jamii yote bila kujali uwezo wa mtu, kupata taarifa kamili na sahihi kuhusu uzazi salama hapa nchini”.

Akichangia katika hilo, meneja mauzo na masoko wa Mustafa Hassanali, ndugu Hamis Omari alisema kuwa “maonyesho haya yataenda sambamba na utoaji elimu bure kuhusu afya ya uzazi salama, tekinolojia husika na haki ya kila raia katika hili”

Meneja Masoko huyo aliwaomba wadau na makampuni mbalimbali kujitokeza ili kudhamini onyesho hilo lenye nia njema, ili kutoa mchango wao katika kumsaidia mwanamke wa Tanzania na uzazi salama.

‘Mamma Mia’ ni jina lililotokana na wimbo uliovuma sana katika miaka ya 80 na kundi la ‘ABBA’, ambapo onyesho hilo litajumuisha mitindo mipya na ya nguvu toka kwa Mustafa Hassanali, pamoja na wabunifu waalikwa toka wiki ya mitindo ya Uingereza.

Nukuu kwa Mhariri:

KUHUSU MUSTAFA HASSANALI
Mustafa Hassanali ni mbunifu mjasiriamali anaeamini katika ‘daima sitashindwa’ huku akitumia kipaji chake na ubunifu wake wa mavazi katika kuleta maisha bora ya sasa na ya baadae.

Kazi za mbunifu Mustafa zimekuwa zikithaminika na kuonyeshwa kimataifa, ambapo Mustafa alifanikiwa kuonyesha ubunifu wake katika nchi kama Angola ‘Angola Fashion Business’, FAFA (Festival of African Fashion and Arts in Kenya), Kameruni, Wiki ya Mitindo India 2009, Naomi Campbell’s fashion for relief 2009, Arise Africa Fashion Week 2009, Wiki ya mavazi Durban & Cape town, Vukani Fashion Awards Pretoria, Miss Ethiopia Beauty Pageant, Mediterranean Fashion Festival, Sicily, Italia, M’net Face of Africa, Msumbiji, Uganda, na Wiki ya Mitindo Kenya, ambayo kwa pamoja yamemletea heshima kubwa, ndani na nje ya nchi.

KUHUSU SHIRIKA LA UTEPE MWEUPE
Ni shirika la kimataifa lisilo la kiserikali, lenye nia ya kuleta mabadiliko katika suala zima la uzazi salama, kati ya mama na mtoto duniani kote.

Katika jamii nyingine, rangi nyeupe ina maana ya majonzi, na jamii nyingine, nyeupe in maana ya matumaini na uhai, hivyo basi utepe mweupe umetwaliwa kama kumbukumbu kwa wanawake wote waliofariki kwa mimba , na katika harakati za kujifungua.
Toka ilipoanzishwa mwaka 1999, shirika la utepe mweupe limekuwa likikuwa kwa kasi duniani kote, hadi kufikia kuwa na nchi wanachama 148 ambao wanapaza sauti zao kwa ajili ya wanawake na jamii zao kwa ujumla. Ambapo kwa sasa linaongoza katika kuyakabili majanga yanayotokana na vifo vya uzazi.

KUHUSU MUSTAFA HASSANALI NA SHIRIKA LA UTEPE MWEUPE.

Mustafa Hassanali, ni mbunifu wa mavazi anayeshirikiana kwa karibu sana na shirika hili, ambapo kwa pamoja waliwahi kufanya onyesho na Naomi Campbell lililofahamika kama ‘Naomi Cambpell’s fashion for Relief’ mwaka 2009, ambapo zilokusanywa kiasi cha dola 65,000.

Mustafa Hassanali, mwenye shahada ya udaktari, anaamini kwa moyo mkunjufu kabisa katika kutumia mitindo kama njia yakusaidia kuchangisha fedha, na kusambaza ujumbe wa masuala ya afya kwa jamii yote.

Kwa maelezo zaidi tembelea www.mustafahassanali.net

No comments: