Masheha kuwa na Makarani....
ZANZIBAR: SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema inatarajia kuwawekea makarani Masheha ili kuweza kufanya kazi zao vizuri na kwa ufanisi zaidi.
Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Idara Maalumu za SMZ, Haji Omar Kheri aliwaambia wajumbe wa baraza la wawakilishi jana katika kikao kinachoendelea Chukwani Mjini Zanzibar wakati akijibu masuali ya nyongeza ya wajumbe hao.
“Katika bajeti ya fedha mwaka ujao wanatarajia kuwawekea makarani angalau wawili kwa kila sheha ili waweze kuwasaidia katika shughuli zao za kila siku kwani wameonekana wamekuwa na kazi nyingi zinazohitaji usaidizi” Alisema Waziri huyo.
Akijibu suali kuhusiana na kutunzwa kumbukumbu Waziri huyo alisema utunzaji wa kumbukumbu upo salama na haijawahi kupata taarifa ya kupotea kwa kumbukumbu licha ya kuwa baadhi ya Ofisi za Masheha kuwepo katika makaazi ya watu.
Alisema serikali imeandaa daftari maalumu la taarifa ambalo kila sheha atalazimika kujaza taarifa zake, ili kuiainisha mfumo wa taarifa zake.
Hatua hiyo imeelezwa kuwa itasaidia kwa kiasi kikubwa kutofautiana kwa mfumo wa mtunzaji wa taarifa ambao unafanywa kwa ushirikiano na Tume ya Mipango.
Waziri huyo alisema kuwa utaratibu wa kuweka kumbukumbu unafanyika na taarifa hizo ndizo zinazowawezesha masheha kutekeleza majukumu yao ya kila siku ambapo alisema kila Sheha ana jukumu hilo.
“Mheshimiwa Spika naomba nisema kwamba ili kuoainisha mfumo huo wa taarifa Ofisi yangu kwa kushirikiana na Tume ya Mipango tumeandaa daftari la taarifa ambalo kila sheha atatakiwa kulijaza na litaondowa kutofautiana kwa mfumo wa mtunzaji wa taarifa zake”, alisema Waziri huyo.
Hata hivyo alisema kuwa baada ya kujazwa katika daftari taarifa hizo zitawekwa katika mfumo wa kompyuta ili kuhifadhi kumbukumbu hizo.
Kheri alisema kuwa mfumo huo upo salama na hawajawahi kupata taarifa ya kupotea kwa kumbukumbu licha ya kuwa baadhi ya ofisi za masheha ziko katika makaazi ya wananchi.
Awali katika suali lake la msingi Mwakilishi wa nafasi za wanawake (CUF) Mwanajuma Faki Mdachi alisema kwa kuwa Masheha hufanya kazi zao kwa niaba ya serikali na ili Masheha wafanye kazi zao vizuri wanatakiwa waweke kumbukumbu mbali mbali katika maeneo yao ili kuondoa utatanishi baina ya Masheha na wananchi wlaiomo katika shehia zao, Je utaratibu wa kuweka kumbukumbu unafanyika.
Aidha Mwakilishi huyo alitaka kujua iwapo utaratibu huo unafanya kazi na ni masheha wangapi wenye kufanya hivyo na kwa kiasi gani utunzaji wa kumbukumbu hizo unakuwa salama wakati ofisi za Masheha zipo majumbani mwao.
No comments:
Post a Comment