Leo ni Sikukuu Zenj (15/10/07)
Wananchi wa Zanzibar leo watendelea kuwepo mapumzikoni, katika kusherekea sikukuu ya Idd El Fitri. Hayo yalitangazwa na Mkurugenzi wa Idara ya Utumishi visiwani humo. Kwa kawaida sikukuu hii huwa na mapumziko ya siku mbili rasmi, hata hivyo mwaka huu iliangukia siku ya mapumziko, hivyo pengine SMZ wakaona ni vema na siku ya Jumatatu wananchi wake waendelee kufaidi kusherekea sikukuu.
Visiwani sikukuu za Idd husherekewa kwa muda wa siku nne mfululizo,ambapo siku mbili kati ya hizo huwa ni mapumziko rasmi, na zingine mbili husherekewa baada ya saa za kazi kwisha. Viwanja rasmi hutengwa na Halmashauri za miji kwa ajili ya watu kwenda huko kushereheka, karibu kila aina ya burudani huwepo katika viwanja hivyo. katika viwanja hivyo huwepo na maduka ya kuuza toys,vibanda vya vyakula, vibanda vya kupiga picha, vibanda vya tombola, vibanda vya taarabu, disco na uchekeshaji na vibanda vingine. Kwa Halmashauri hizo ni wakati mzuri wa kukusanya kodi kubwa katika kipindi kifupi zaidi cha ukusanyaji wa kodi. Aidha kwa wananchi ni wakati wa kutumia kwa nguvu katika kipindi kifupi.
Kwa wafanyakazi wa SMZ sherehe hizi hufana zaidi iwapo zitaangukia mwisho wa mwezi, kwani wengi wao hua na uhakika wa kupeleka familia zao katika viwanja hivyo kwa muda wote. Iwapo una familia, mke/wake na watoto, basi hupenda kuwa na nguo mpya kwa siku zote za sikukuu, pesa ya kwenda na kurudi na za kujichana wawepo viwanjani humo.. huku watoto ukiwa ndio wakati wao wa pekee kununua toys wazipendazo. Hivyo kwa mfanyakazi wa SMZ inabidi awe amejinyima sana ili kuweza kufurahisha familia yake.
Kujinyima kwa wafanyakazi hao si kitu rahisi sana kutokana na viwango vya mishahara na hali halisi ya maisha visiwani humo, hii husababisha wasiwe na mipango ya muda mrefu ya kujiandaa na sherehe hizo, zaidi ya kuomba Mungu sherehe hizo ziangukie karibu na mwisho wa mwezi.
Katika ile awamu ambayo wafanyakazi walikuwa wakilipwa mishahara yao katika siku ya arobaini, kulikuwepo na tabia ya wafanyakazi kulipwa nusu msharaha iwapo sikukuu itaangukia katikati ya mwezi. Hii iliwapunguzia machungu ya kusubiri mshahara wa siku ya arobaini na kuweza angalu kuvinjali na familia zao katika viwanja vya sikukuu. Hata hivyo wakati huu nusu mshahara haikutoka na zaidi leo wameambiwa kuwa wapumzike. Kwa upande wa wengi hii ni kero kwao. Iweje upumzike wakati huna hata senti mfukoni. Wengi wanaona bora wangeenda huko kwenye maofisi yao kufanya kazi kuliko kukaa nyumbani pasipo kuwa na kitu. Mbaya zaidi iwapo mfanyakazi ana akaunti ya katika Benki ya Watu wa Zanzibar(PBZ), ina maana kuwa leo hatoweza kutoa fedha zozote, kwani benki itakuwa imefungwa na PBZ hawana ATM...
Hivyo nina imani kuwa pamoja na nia nzuri ya SMZ, kuwapa wafanyakazi siku ya leo kuwa ya mapumziko, sio wengi ambao wamefurahia tangazo hilo. Zaidi limewaweka katika wakati mgumu wa kujibu maswali mengi toka kwenye familia zao.