Wednesday 11 April 2007

Safarini Uingereza

Wapenzi wa kona hii ya Vituko vya Zenj, napenda kuwataarifu kuwa nitakuwa safarini Uingereza kuanzia mwishoni mwa wiki hii..

Kwa miezi kadhaa ijayo nitakuwa na blog tokea jiji la London. Zaidi itakuwa jambo la msingi iwapo nitaweza kukutana na wanablog wa Uingereza...na watanzania wengine ambao ni wapenzi wa blog..

Tuesday 6 March 2007

Uchovu wa SMZ kwenye masuala ya Umiliki wa Ardhi...

Moja ya matatizo makubwa ya SMZ yapo kwenye masuala ya umiliki wa ardhi. Serikali hiyo ina migogoro mingi kuhusu umiliki na uendelezaji wa ardhi licha ya kuwa na sheria ya Mipango miji/vijiji na Ardhi ya mwaka 1985, Baraza la Manispaa ya mwaka 1995 na Mamlaka ya Hifadhi na Uendelezaji wa Mji Mkongwe ya mwaka 1994.

Sheria hizo zote hapo juu zinasimamia uendelezaji na umiliki wa ardhi, aidha Halmashauri za wilaya nazo kwa upande mwingine zimekuwa zikisimamia uendelezaji wa ardhi. Serikali kuu kupitia kwa Masheha wao nao wamekuwa wakijishughulisha katika masuala ya ardhi.

Katika Mahakama zote visiwani humo kumejaa kesi nyingi za madai ambazo zinahusiana na matatizo ya ardhi.

Leo kanisa la Anglikana huko Zanzibar limekumbushia kadhia yao ya kunyang'anywa ardhi yao na kufanyia mabadiliko ya matumizi. Kimsingi eneo ambalo lina mgogoro ni shule ya msingi Mkunazini ambayo kabla ya mwaka 1964 ilikuwa inamilikiwa na kanisa hilo.

Kinachoshangaza ni hatua ya SMZ kupitia wizara zake kuendelea kubadilisha kinyamela matumizi ya eneo hilo toka eneo la shule na Ibada kuwa eneo la biashara, kwa kuruhusu ujenzi wa maduka katika eneo hilo.

Miaka ya tisini kanisa hilo liliwahi kuomba ruhusa ya kukarabati uzio wa eneo hilo ambao ulikuwa unazama taratibu. Uzio huo unaanzia upande wa mbele ya shule hiyo mkabala na barabara ya Benjamini Mkapa. Kibali cha ujenzi wa uzio huo kilichukua muda mrefu hadi kupatikana. Na kiliweza kupatikana baada ya kanisa hilo kutoa malalamiko mengi kuhusu urasimu wa vyombo vya SMZ.

Ucheleweshaji wa upatikanaji wa Kibali cha Matengenezo ya Ukuta wakati ule sasa ninaweza kuuelewa vizuri. Inaoneka Watendaji wa SMZ walishaona kuwa eneo hilo linafaa kwa kujengwa kwa Vibanda na Viduka vya biashara hivyo walikuwa wanasita kutoa ruhusa ya matengenezo ya ukuta. Na hata walipotoa ruhusa hiyo eneo lilikuwa karibu na shule hiyo halikupewa ruhusa ya ukarabati.

Sasa eneo hilo limejengwa Vibanda vya biashara, na litaendelea kujengwa licha ya maombi ya kanisa hilo kurejeshewa umiliki wa shule hiyo.

Hivi ni nini nafasi ya kuwa na mamlaka ya hifadhi na uendelezaji wa mji mkongwe, iwapo sehemu ambazo zinahitaji kupatiwa hifadhi kutokana na umuhimu wake wa kihistoria, zinashindwa kuhifadhiwa? Kanisa la Anglikana ni muhimu kabisa katika historia ya Zanzibar. Hivyo linatakiwa lipewe nafasi ya ya kuhifadhiwa chini ya Sheria za Mamlaka ya Hifadhi na Uendelezaji Mji Mkongwe.

Thursday 15 February 2007

Sasa ni Disco...!

Katikati ya mwaka jana(2006)SMZ ilipigia marufuku matumizi ya simu za mkononi kwa wanafunzi wote wa shule za Msingi na Sekondari kwa madai kuwa, simu hizo zinachangia kwa kiasi kikubwa kwa wanafunzi kushiriki katika vitendo vya ngono, aidha wanafunzi hao wamekuwa wakipoteza muda mrefu kuandika meseji na kupokea simu wawapo darasani na katika maeneo ya shule.

Sasa SMZ imenyoshea mkono Disco kuwa imesababisha kwa wanafunzi wengi kufeli mtihani wa kidato nne wa mwaka jana. Hivyo ni marufuku kwa mwanafunzi yoyote wa shule ya msingi na sekondari kwenda Disco!

Hatua ya kupiga marufuku kwa wanafunzi kwenda kwenye madisco na kumbi za starehe zimepokelewa kwa mitazamo tofauti na waakazi wa visiwa hivyo, ambapo Disco na mojawapo ya sehemu ndogo tu ya Starehe zinazopatina kwenye visiwa hivyo.

Wanafunzi wengi wanakwenda katika madisco wakati wa sikukuu za Idd ambazo huwa ni mara mbili kwa mwaka, Madisco mengine yanayovuta wanafunzi wengi ni kama tamasha la Mwaka Kogwa ambalo hufanyika mara moja kwa mwaka na Tamasha la nchi za Majahazi. Zaidi wanafunzi huonekana kwenye maonyesho ya Muziki wa Kizazi Kipya. Madisco yote haya hufanyika kuanzia saa za maghalibi hadi usiku wa saa nne.

Katika kuona kuwa wanafunzi wa Visiwa hivyo wanafanya vizuri SMZ imo katika mipango ya kutenganisha wanafunzi kwa kuweka shule za jinsia moja tu. Mpango huu umeshaanzishwa kwa baadhi ya shule visiwani humo kwa lengo la kuwafanya wanafunzi hao wasome na kufaulu na sio kutongozana.

Mwaka jana Visiwa hivyo vilishuhudia amri ya kuwataka wanafunzi wa chuo cha "Zanzibar University College" kutochanganyikana(wanaume na wanawake) wakati wa kujisomea usiku, kwa madai kuwa chuo kimezagaa na kondomu zilizotumika!

Hatua za SMZ kutaka kuona kunakuwepo na matokeo mazuri ya mitihani kwa wanafunzi wake zichukuliwe kufuatana na mapendekezo kadhaa yaliyokwisha kutolewa huko nyuma. Kwanza SMZ imekwisha shauriwa mara kadhaa kuhusu kubadilisha mitaala yake ili iendane na ya Tanzania bara. Hata hivyo hadi sasa SMZ wanaonekana kuwa bado kuwa tayali kufuta pendekezo hilo, licha ya kujua manufaa yake kwa wanafunzi na wanakisiwa hicho kwa ujumla. Kinacho zuia kutofuatwa kwa pendekezo hilo hadi leo hakijulikani. Zaidi ni kwa serikali hiyo kuibuka na viamri vya ajabu ajabu kila kukicha! Kitendo cha kupiga marufuku marufuku hizi husababisha kuwafanya wanafunzi kuwa watukutu zaidi.

Kwa upande mwingine Wazazi nao wanapaswa kushirikishwa katika kila hatua ya maendeleo ya wanafunzi wanapokuwa shuleni na majumbani. SMZ inapaswa kushirikiana na wazazi kuona ni kwa kiwango gani wataweza kuongeza bidii ya wanafunzi katika masomo yao. Malezi bora kwa mwanafunzi husaidia kwa kiasi kikubwa kwa mwanafunzi kuwa na bidii katika masomo yake.

UNCEF wanathibitisha hilo kwa kuwa hata nchi zenye utajili mkubwa iwapo wanafunzi wake wanakosa malezi bora matokeo ni kufanya vibaya shuleni.

http://news.bbc.co.uk/2/hi/uk_news/6359363.stm

Tuesday 23 January 2007

Nungwi : Ukahaba, Nguo fupi na Ulevi hauna nafasi..

Linapokuja suala la ukahaba, Kijiji cha Nungwi huko Zanzibar kimekuwa mbele kukanya tabia hizo wazi wazi. Wamejaribu kutumia njia mbalimbali ikimemo maandamano, risala na kutimia viongozi wao katika kukemea tabia hiyo, hali hiyo ni tofauti kidogo na mjini Zanzibar ambapo makundi ya vijana hujichukulia sheria mkononi kuwahadhibu makahaba na wale wavao nguo fupi.
Hatua iliyochukuliwa mwanzoni mwa wiki hii na Kamati ya Maadili na Maendeleo katika kijiji cha Nungwi ya kutunga sheria ndogo ya kudhibithi uvaaji nguo fupi, ukahaba na ulevi inathibitisha ni kwa jinsi gani wanakijiji hicho hupenda kupita katika njia zinazokubalika katika kutoa kero zao.
Nikirudi nyuma na kuangalia kile kinachodaiwa kuwa ni ukahaba na mambo mengine yanayokwenda tofauti na maadili ya wakaazi wa Nungwi, yalianza mara baada ya kijiji hicho kukaribisha hoteli za kitalii. Kabla ya kuja kwa hoteli za kitalii kijiji hicho kilikuwa ni maarufu kwa uundaji wa majahazi na shughuli za uvuvi.
Miaka ya tisini ambayo ilikuwa ni ya mabadiliko makubwa katika sekta ya utalii visiwani huko, Waakazi wa Nungwi walishuhudia maandamo ya kinamama kupinga kuwepo kwa wanawake na wasichana toka mkoani Tanga ambao walidaiwa kuwepo huko kwa lengo la kufanya ukahaba. Wakinamama hao walidai wadada hao toka Tanga wamekuwa wakiwarubuni waume zao na kufanya nao mapenzi kwa pesa na kusababisha hali ngumu katika nyumba zao. Waliendelea kwa kusema uwepo wao hapo kutasababisha kuongezeka kwa ukimwi na kupolomoka kwa maadili. Hivyo waliwataka akinadada hao kuondoka mara moja kijijini mwao. Hatua yao hiyo ambayo iliungwa mkono na Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini, ilizusha mjadala mrefu kuhusu nafasi ya Wabara katika visiwa hivyo. Zaidi ilionekana kuwa Watz bara wanazuiwa kutumia haki yao ya msingi ya kwenda popote pale ndani ya Tanzania pasipo bughuza. Hata hivyo maandamano hayo yalishuhudia kuongezeka kwa Watanga ambao sasa walihamia mjini na vijiji vingine vyenye hoteli za kitalii.
Nungwi hawakuishia hapo, wakanyosha vidole kwa wageni wengine ambao ni wafanyakazi wa mahoteli kwamba wanavaa nguo fupi na suruali za kubana. Kipindi hicho wafanyakazi wengi katika hoteli za kitalii huko walikuwa ni wananchi toka Kenya.
Hatua za Kamati hiyo ya kutunga sheria ndogo ndogo za kudhibiti uvaaji wa nguo fupi na ukahaba, ni hatua nzuri katika kulinda maadili yao. Hata hivyo kuna vitu kadhaa vya kujiuliza juu ya uhalali wa sheria hizo ndogo ndogo na hasa katika kuzisimamia na utekelezaji wake. Kimsingi kuhusu uvaaji wa nguo fupi, kamati hiyo inawataka wale wote wavaao nguo fupi kuvaa vazi la Kizanzibari. Vazi la kizanzibari kwa ufahamu wangu ni kuvaa kanga zaidi ya mbili, huku ukiwa umefunika sehemu zote za mwili na kuachia sura tu. Sheria hii inaweza isikubalike kwa wengi wa wafanyakazi katika hoteli hizo ambao sio wenyeji wa zanzibar.
Na iwapo vazi la kizanzibari ni kama lile la kuvaa baibui na hijabu yake, basi sheria hiyo itakuwa inalenga zaidi maadili ya kidini kuliko maadili ya kizanzibari, na itakuwa sio kosa kuhoji kauli ya serikali ya kusema kuwa nchi hiyo si ya kidini. Na kwanini wananchi ambao sio wa dini fulani washurutishwe kuvaa baibui?
Ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Kaskazini ambayo ndio imepelekewa sheria hizo ili izibaliki, kabla ya Sheha na Wajumbe wake kuanza kucharaza viboko hadharani kwa dada zetu, itabidi iipitie vizuri sheria hizo kabla ya kuziruhusu kutumika. Lengo ni kuona haki sawa kwa waakazi wa kijiji hicho na kisiwa cha zanzibar kwa ujumla, inazingatiwa.