Thursday 13 September 2007

Wajane waweka rekodi mpya huko zenj....!

Wajane wa kisiwa cha Zanzibar wameweka rekodi mpya katika fani ya mavazi. Ni baaada ya kuwa wabunifu wa kwanza kupaka/kuchora hinna kwenye vitambaa ambavyo hutumika kutengenezea nguo mbalimbali. Ubunifu huu waliupata kutokana na kuhudhulia kozi ya muda mfupi juu ya kuchora hinna kwenye vitambaa.

Ili lengo la mafunzo hayo liweze kufanikiwa ambalo ni kuongeza kipato kwa Wajane hao, ni muhimu kuona kuwa wanakuwa na sehemu rasmi ya kufanyia biashara zao. Kwa upande huu wa fani zisizo rasmi kuwekuwepo na usumbufu mkubwa wa sehemu za kufanyia shughuli zao, pengine ni kutokana na serikali kutowajali, hivyo kuwasumbu sumbua kila kila.

Sehemu ambayo Wajane hawa na wafanyabiashara wengine katika fani hiyo wamekuwa wakiitumia ni Eneo la mji mkongwe na sehemu ya Uwanja wa Forodhani na baadhi ya mitaa ambayo hutokea katika uwanja wa forodhani kama vile mtaa wa gizenga. Halmashauri ya Mji kupitia maelekezo ya Mamlaka ya Mji Mkongwe, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mjini Maghalibi na ofisi ya Waziri Kiongozi wamekuwa mara kwa mara wakiwaondoa wafanyabiashara hao kwa madai mengi, ambayo mengine uhusisha mambo ya dini.

Kwa kuweza kuweka rekodi ya Dunia, ambapo sasa wataweza kujiongezea mapato yao maradufu, Ni vema kwa serikali kutowasumbua sumbua Wajane hao. Soko lao hilo linawalenga watalii ambao hupatikana katika maeneo ya forodhani ambako kuwa vivutio kadhaa vya Utalii. Na zaidi SMZ sasa iweke mikakati ya kuweza kutambua fani zisizo rasmi, kwani zaidi ya kutoa ajila kwa wahusika zitaweza vilevile kuingiza mapato ndani ya serikali na kusaidia juhudi za serikali kupunguza umaskini kwa wananchi wake.

Ni Msimu wa Beer za Mafichoni...Zanzibar


Mwezi wa Ramadhan huko Zanzibar, hubadilisha sura ya kawaida ya visiwa hivyo, aidha pilikapilika nyingi za kawaida huenda likizo ya muda, huku pilika nyingine huchukua nafasi katika kipindi hiki.

Kwa wanywaji wa bia ambao hawafungi, uungana na wananchi wengine ambao wana imani zingine kuendelea kunywa bia, kwa staili ya kujifungia ndani ya nyumba za ulevi....Kwa ufupi katika kipindi hiki cha mfungo, migahawa, hoteli, baa na majumba mengine yote ya starehe hufungwa. Hakuna sheria rasmi ya kufanya hivyo, ila kwa kuwa imekuwa ikifanyika kwa miaka nenda rudi sasa inaonekana ni kama sheria. Na iwapo ukishikwa unakula mchana katika mfungo huu, basi utasekwa rumande na kuachiwa baada ya siku moja au kushitakiwa kabisa!

Miaka kadhaa huko nyuma Beer ilikuwa ikiuzwa katika hotel za serikali tu wakati wa mfungo huu. Tena waliokuwa wanakusudiwa hapo ni watalii tu...! labda na wageni wa serikali ambao wana imani tofauti. Zaidi ya kuuza bia, hoteli hizo pia ndio zilikuwa zikiuza msosi. Hata hivyo mambo sasa yamechukua sura mpya. Baa nyingi huendelea kufanya kazi katika kipindi hiki, zikiuza bia na misosi. Tofauti ya mwezi huu na miezi mingine ni kuwa unywaji ufanyika kwa kujificha, na katika mazingira ya ukimya kabisa, huku wengi wakisubiri king'ora cha kufuturu...!

King'ora kikisharia, kumbi hizo ufunguliwa milango, redio hufunguliwa na kelele za kawaida za kwenye baa huanza kusikika! Hali hii uwepo kwa muda wa mwezi mzima.

Sunday 9 September 2007

Karibu Kahawa...



Kwa wale waliofika Zenj na kunywa kahawa na kashata mitaani, kahawa hiyo sasa inapatikana kwenye makopo kwa matumizi ya nyumbani.

Friday 7 September 2007

Karume Boys hamna aibu?

Karume Boys imepewa jina hilo baada ya rais wa Zenj kujitosa katika kudhamini mchezo wa mpira wa miguu huko visiwani na hata katika ngazi ya afrika ya mashariki na kati. Rais huyo amekuwa mstari wa mbele kusimamia mchezo huo kwa kuhakikisha kuwa timu za Taifa kama hii ya vijiana wa umri chini ya miaka 17 wanashiriki katika mashindano makubwa.
Kwa kufanya hivyo nina imani kuwa lengo la rais ni kuwajenga vijana hao kimchezo tokea wakiwa vijana ili waje kuingia kwenye timu za wakubwa wakiwa na uzoefu mkubwa katika mchezo huo.

Kilichotokea hivi karibuni huko Burundi, kinatia shaka na kinyaa katika medani ya soka visiwani humo. Kuna tuhuma kuwa vijana hao waliuza mechi kwa jirani zao wa Kenya, ili timu hiyo ya Kenya iweze kuingia hatua ya nusu fainali. Kuuza mechi za kitaifa kwa kweli kunatia shaka sana na kama ni kweli basi itakuwa ni hujuma mbaya kabisa kutokea katika fani hii ya kusakata kabumbu katika visiwa hivyo na hata kwa Tanzania kwa ujumla.

Nikirudi nyuma kuangalia maandalizi ya timu hiyo na safari yake ya Burundi yalikuwa ni ya kusuasua na hasa katika suala zima la gharama za timu hiyo kuanzia kambini kwao hadi nauli ya kwenda huko.

Kuanzia timu za Taifa, hadi kwenye vilabu vya Zenj vimekuwa na tatizo la udhamini, hivyo kufanya kuitegemea zaidi serikali katika kushiriki mashindano ya kimataifa. Rais huyo wa Zenj nina hakika alikubali kuanza kudhamini timu hiyo kutokana na kukosekana kwa wafadhili wenye ridhaa ya SMZ. Kwani sio kila mfadhili hukubalika huko Zenj. Hali ya sasa ya udhamini wa soka, na hata uwezo wa vilabu vya soka huko visiwani ni wa kutia shaka, na hii inadhibitishwa na klabu bingwa ya visiwa hivyo timu ya Miembeni kutaka kujitoa au kuuza nafasi yao ya kushiriki mashindano ya klabu bingwa afrika, kutokana na kukosa fedha za kugharamia maandalizi na ushiriki wa mashindano hayo. Hata yule mfadhili wao ambae aliweza kuwaingiza wapenzi wa Miembeni na watu wengine bure kujaza uwanja wa Amani amejitoa kuidhamini timu hiyo katika mashindano hayo muhimu.

Tatizo kubwa la soka visiwani huko ni kukosekana kwa wafadhili. Kipindi kile cha Mzee Ruska, timu za Zenj zilikuwa zikitamba sana, na ilitokana na kuwa na wafadhili. Kwa mfano timu ya Malindi iliweza kununua wachezaji nyota wa timu ya Taifa ya Zambia, kuchezea timu yao, zaidi waliweza hata kuleta wachezaji toka Ulaya ya Mashariki. Mlandege nayo haikuwa nyuma katika kuwakilisha vizuri visiwa hivyo, ambao wachezaji walikuwa wakilipwa kama ni wachezaji wa kulipwa.

Kuanguka kwa ufadhili wa mtu mmoja mmoja kulifungua ukurasa kwa makampuni makubwa kama ya Bia kuingia katika anga za soka. Hata hivyo SMZ ilipinga vikali udhamini wa makampuni ya Ulevi... Kwa kudai kuwa unakwenda kinyume na maadili ya Nchi. Taratibu vilabu vilianza kudorola na hata kufikia kwa timu ya Taifa.

Kilichotokea huko Burundi kinawezekana kutokana na hali halisi ya maandalizi ya timu hiyo. Inaonekana kuwa timu hiyo haikuwa na motisha wa aina yoyote zaidi ya kushiriki mashindano hayo ili siku ipite na warudi makwao. Timu hiyo inawezekana ilikuwa katika hali ngumu kimaisha huko, kiasi ikiwa ni rahisi kurubuniwa ili kudhibiti njaa zao.

Waziri kiongozi nae aliona hali ngumu ya ufadhili kwa timu hiyo, na kabla ya timu hiyo kwenda huko Burundi alinukuliwa akisikitishwa na wafadhili kutojitokeza kuidhamini timu hiyo. Hayo, pamoja na mengine itakuwa ni busara kusubiri uchunguzi wa ZFA dhidi ya timu hiyo. Aidha itakuwa ni jambo la mbolea kwa ZFA kutujulisha matokeo ya uchunguzi wao. Ambao utatuwezesha kujua kipigo cha magoli matano kilikuwa ni kuzidiwa kimchezo au hujuma!