Monday, 3 September 2007

Zenj Watatoa Lini Miss Tz......?



Mshindi wa Miss Tz mwaka huu amewasha moto mkubwa kwa wadau wa urembo wa huko bara, ikiwa ni pamoja na mamiss kadhaa waliopita. Moto huo ambao kuzimika kwake ni songombindo unatokana na madai kuwa miss huyo hana asili ya Utz bara, ukinondoni n.k Usishangae sana kusema Utz bara, kwani huko visiwani hakuna mambo ya Umiss, na nina shangaa huyo mdosi...sori huyo miss kuitwa Miss Tz wakati Warembo wa Zenj hawakushiriki mashindano hayo...

Mara ya mwisho kwa kumbukumbu zangu, warembo wa marashi ya karafuu walishiriki mashindano hayo wakati yakidhaminiwa na fegi za aspen.. sijui bado zipo au la! manake fegi hizo zimeadimika sana mitaani.

Awali ya yote inaonekana kuwa Watz wameshindwa kabisa kuficha makucha yao ya kibaguzi kwa kupiga kelele kwa mdosi huyo mzalendo kutwaa taji hilo. Mimi binafsi sishangai sana, kwani ile dhambi ambayo ipo visiwani huku, imeweza kuvuka bahari na kutua huko Bongo...Tz bara.

Iwapo kungekuwpo na Miss Zenj basi yoyote yule ambae angebahatika kutwaa taji hilo, angechunguzwa kuwa ana asili ya wapi...! Kama ni kutoka kisiwa cha pili basi angeitwa ni mpemba, na iwapo angekuwa anakaa Ng'ambo iliyo karibu na Mji mkongwe basi wangesema ni Mngazija, zaidi iwapo angekuwa na chongo basi moja kwa moja angeitwa ni mnyamwezi( mtu yoyote toka bara).

Utamaduni wa kuangalia mtu ana asili ya wapi upo muda mrefu katika visiwa hivi, kiasi kwamba umeleta kujitenga kimakaazi kwa watu... Tabia hii huko bara haikuwepo huko zamani, lakini sasa naona inaingia kwa kasi kubwa. Sijui inaashiria kitu gani, kwani, huko bara waasia wamekuwa wakishika dhamana kubwa kubwa katika kuongoza nchi pasipo mashaka wala malalamiko yoyote. Leo hii kupatikana kwa miss mdosi wa kitz imekuwa nongwa!

Iwapo tulikuwa tukitembea vifua mbele kupinga ubaguzi wa rangi miaka ile, iweje leo tutoe machozi kwa mtz wa kiasia kutwaa taji la Utz? Au ile dhambi toka Zenj tayali imeshaanza kuingia huko bara? Tuliwahi kuonywa kuwa dhambi ya ubaguzi ni mbaya sana, eti ni sawa na kula nyama ya binadamu, kwani hutoishia kuionja tu, bali utaendelea kuila tu!... Mwakani Watz watahoji ni kwanini Mass wanatoka Kinondoni, au kwa nini wamiss wanatoka katika kabila fulani kila mara... Dhambi hiyo itaendelea tu!

Wazenj mara nyingi wamekuwa wakisoma mifano imara ya Tz bara katika suala zima la kuishi bila kujali huyu anatoka wapi au ana asili ya wapi... Iwapo leo hii mmefikia hatua hii, basi mnapoelekea sio kuzuri kabisa. Mfano wa karibu upo huku visiwani!

3 comments:

Egidio Ndabagoye said...

Inasikitisha sana hii.Tukianza kuchunguzana asili yetu kutakuuwa hakukaliki kabisa.Watanzania sasa tuelewe hizi sio zama za ujima tuko katika kizazi cha dijitali.

Simon Kitururu said...

Hii kitu mbaya sana!Niliwahi kufanya kazi kwenye Zanzibar Film festival kama MC .Basi ilikuwa nikiongea kiswahili tu , nasikia kutoka katika ukumbi, mtu wa bara huyo!

Kilichosaidia, nilikuwa natumia Kiingereza na Kiswahili ikawa inapunguza makali. Ila kuna wakati nilikuwa nahisi nikikosea kitu, kuzomewa kwa sababu ni mbara kungeweza kufikia.

Kulikuwa na MC mwingine ambaye alikuwa anajua Kiarabu, halafu kwa madoido yake alikuwa anatangaza kwa kiswahili na Kiarabu, ingawa na uhakika watu wengi walikuwa hawaelewi anaongea nini kwa Kiarabu. Walikuwa wanafurahia si mchezo akifungua mdomo tu!

Huku bongo ubaguzi wa rangi umekuwepo muda mrefu.Nakumbuka tokea hata shule ya vidudu tulikuwa tunaimba nyimbo za kupinga makaburu Afrika kusini lakini kulikuwa na nyimbo nyingine zilizokuwa zinalenga rangi yao na sio Uasi wao.

Wahindi ni muda mrefu tu wamekuwa wakiitwa majina ya ajabu na pia ilikuwa ni alama ya kutokuwa na nguvu.Yoyote mlegevu ilikuwa rahisi kumuita Mdosi. Wengi tu washavutwa sana nywele na mambo kibao, kitu ambacho siwezi kushangaa baadhi yao wakikitumia kama sababu ya kujitenga.

Kikubwa ni kwamba, inabidi tutambue kuwa ubaguzi ukopande zote. Na ukweli ni kwamba advantage tuzitumiazo kudai kuwa wanatuzidi mahesabu , tunawapa sisi wenyewe. Kwa ujumla siwezi kuelewa kwanini Waafrika washindwe kuushika uchumi Wa Tanzania na kusingizia kuwa ni kwasababu Wahindi wanatuzidi ujanja.

Kibunango said...

Egidio na Simon:
Ni kweli sasa inaonekana wazi kuwa tuna tatizo la ubaguzi miongoni mwetu. Sasa sijui litakuwa limechangiwa na nini hasa! Je ni uchumi, Elimu au Maendeleo?
Tunachoweza kusoma kutokana na miss 2007 ni kuwa bado hatukuweza kuondoa ubaguzi miongoni mwetu. Na ili tuweze kuondoa tabia hii, ni muhimu kukumbushana juu ya athari za kibaguzi. Tusichoke kukemea tabia hii ili historia isije kutuhukumu.

Simon pale shule ya Majimaji Songea, Darasani mwangu kulikuwa na wahindi wawili... zaidi ya utani wa kawaida tulisoma nao vizuri hadi kumaliza darasa la saba!.

zaidi leo nimepita Mawazoni katika kuchangia mada ya Afrika na Taka toka China mtambo wangu ukazima... Sasa sijui pale kwako wamekuwekea nini?