Friday, 6 February 2009

Athari za Utalii kwa Mazingira ya Zanzibar




Moja ya masharti wanayopewa watalii mara waingiapo Zenj, ni juu ya uvaaji wa nguo ambazo hazistiri mwili mzima, yaani uvaaji wa suruali kipande, vichupi, ama kutembea vifua wazi ni sawa na kwenda uchi ndani ya Zenj. Hivyo watalii uambiwa wavae nguo zinazofunika mwili wote wakati wao wote watakapo kuwepo visiwani humo. Kwa watalii sharti hili ulipokea kwa shingo upande kwani wanapotoka ni sehemu za baridi na kwa muda mrefu wanakuwa wakivaa nuo nyingi kujikinga na baridi, na hivyo wanapotalii katika nchi za joto hupenda kuipa nafasi miili yao kufaidi joto hilo ambalo kwao ni adimu.

Hata hivyo linapokuja suala la ujenzi wa hoteli za kitalii Masharti na Taratibu zake hazijulikana kabisa, kwani vyombo vinavyosimamia ujenzi huo havina ushirikiano wa moja kwa moja na Idara ya Mazingira ambayo ipo kisheria kusimamia mazingira ya Visiwa hivyo chini ya sheria ya mwaka 1996.

Utalii katika visiwa vya Zanzibar sasa umeshapanuka sana na visiwa hivyo vimeshashuhudia mambo mengi yaliyokuja na utalii, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa hoteli nyingi za kitalii karibu kwa fukwe zote visiwani humo pamoja na visiwa vidogo dogo, ongezeko la wageni wahamiaji kwa ajili ya kazi za kitalii, ongezeko la uvuvi kwa ajili ya vyakula vya watalii, ongezeko la safari za anga na ardhini, ongezeko la maduka rasmi kwa ajili ya watalii na mambo mengine mengi yanayoendana na utalii kwa ujumla.

Mengi katika haya yalikuja pasipo kwa wenyeji wengi kujiandaa na sasa inakaribia miaka ishirini tokea mfumuko wa utalii visiwani kuanza, na kumekuwepo na malalamiko mengi toka ndani ya visiwa hivyo na nje ya visiwa hivyo kwa jinsi suala zima la utalii lilivyobadili mambo mengi visiwani humo. Wenyeji wengi wanalalamikia sehemu kubwa ya ajila kushikwa na wageni, ongezeko la bei kwa vyakula vya baharini, kupigwa marufuku kutembea ama kuvua katika baadhi ya hoteli hizo. Huku asasi za kimataifa zikipigia kelele uharibifu wa mazingira kutokana na aina za ujenzi wa baadhi za hoteli visiwani humo, uharibifu wa coral reef kutokana na uvuvi uliokithiri, kutokuwepo na miundo mbinu ya kutosha kwa ajili ya kuhifadhi maji taka na utupaji holela wa taka toka mahotelini humo.

Hadi kufikia mwaka 2003 takwimu za ZIPA zinaonyesha kuwa, jumla ya miradi 242 ilidhinishwa yenye thamani ya jumla ya dola za kimarekani milioni 403. Mwaka 2001 Zanzibar iliingiza dola za kimarekani milioni 46 kutokana na utalii pekee ikiwa ni asilimia 15 ya GDP. Makisio yanaonyesha kuwa kutakuwa na ongezeko la asilimia 21 la GDP kufikia mwaka 2012 na kufanya mgawanyo wa mapato kufikia million 116(makadirio haya yalifanyika kabla ya Global recessionya mwaka huu).

Ripoti ya maendeleo ya utalii ya Zanzibar iliyoandaliwa na na UNDP inaonyesha kuwa katika mwaka 1983 kulikuwa na sehemu kumi tu za malazi visiwani humo zenye vyumba 215 na jumla ya vitanda 467 ambazo hazikuwa kwenye daraja la aina yoyote(utalii au malazi ya wageni wa kawaida). Leo hii sekta ya utalii visiwani humo ina sehemu zaidi ya 180 za malazi, zenye zaidi ya vyumba 3160 na zaidi ya vitanda 6490.

Kufikia mwishoni mwa mwaka 2006, ripoti ya Umoja wa Mataifa(UN) ilionya kuwa Zanzibar imekuwa mojawapo ya nchi duniani inayoongoza kwa uchafuzi wa mazingira ya baharini kutokana na umwagaji wa maji taka katika bahari ya Hindi pamoja na uharibifu wa vyanzo vya maji. Mtafiti Stefan Gossling toka Sweden, yeye alionya kuwepo na uharibifu mkubwa wa coral reef kwa lengo la uuzaji wa viumbe vyake kwa watalii. Maeneo yenye uharibifu mkubwa wa mazingira kutokana na utalii visiwani humo ni ya Kaskazini na yale ya Mashariki.

Ukuaji wa utalii, licha ya kuendelea kuharibu mazingira umesababisha kuwepo na ushirikiano mdogo kati ya serikali na wananchi wake. Kwa upande wa mazingira wananchi wengi wanalalamikia hatua kadhaa za wenye hotel kuwanyima sehemu zao za uvuvi, ulimaji(seaweeds), minazi na hata kutembea karibu na hotel hizo. Mwaka 2002 wananchi wenye hasira katika kijiji cha Kendwa walichoma moto hoteli ya kitalii kwa madai ya hoteli hiyo kuharibu coral reef, tabia hii ilisambaa kwa baaadhi ya vijiji vya Nungwi.

Baadhi ya hotel( Fundu lagoon, Matemwe Bungalow, Blue Bay, Mnemba Island na Chumbe) zimeonyesha kujali athari ambazo zinatokana na ujenzi wa hoteli zao kwa mazingira. Wamejitahidi kufuata aina za ujenzi usio tumia resources kwa wingi, aidha wamejitahidi kufuata aina ya ujenzi wa nyumba za vijiji zinavyowazunguka. Hivyo kupunguza uharibifu wa maji safi na bahari.

Serikali kwa upande wake imeendelea kutoa vibali vya ujenzi pasi kuzingatia uharibifu wa mazingira au namna ya kujenga pasipo kuwepo na uharibifu wa mazingira. Hoteli zinaendelea kujengwa pasipo kuwepo na mfumo unaotambulika wa ukusanyaji na usafishaji wa maji taka, ukusanyaji na utupaji wa taka ngumu na utunzaji wa vyanzo vya maji. Aidha hakuna taratibu zozote ambazo zinatolewa kwa kutumia materials ambazo zinaendana na mazingira ya fukwe zinazojengwa.

Na kama kawaida yao, mambo yanapokwenda kombo, viongozi huja na amri kede kede. Nakumbuka miaka miwili iliyopita Mh. Mansour Yussuf Himid alinukuliwa akisema;
“Serikali imegundua ukiukwaji wa taratibu za utunzaji wa mazingira katika ukanda wa fukwe”
Aidha alikubali kuwa sekta ya utalii ndio inaongoza katika uchafuzi wa mazingira visiwani humo na kuzitaka Idara zinazohusika kujipanga kukabiliana na tatizo hilo hilo, huku Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ikisema kuwa yeyote ambae atakiuka taratibu za Mazingira ataburuzwa mahakamani na kupigwa faini ya Sh million 2 ama kwenda Chuo cha Mafunzo kwa kipindi cha miezi sita.

1 comment:

EDWIN NDAKI (EDO) said...

Nimekusoma kamanda.

Nakumbuka msemo mmoja kwenye kipindi likuwa kinarushwa RTD(sijui kama bado kipo hewani) walikuwa wanachagiza kwa maneno "MAZINGIRA NI UHAI"

Hakika "mazingira" yasipolindwa tunaweza kufikiri tumeingiliwa na MAZINGARA!

Tutafika tu..