Tuesday 10 February 2009

Kichekesho kingine toka kwa Shamsi Vuai Nahodha



Mwishoni mwa mwezi Januari mwaka huu, Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi alinifanya nicheke kwa kauli yake ya kuamua kushika fagio na kuanza kufagia barabara za Zenj kutokana na barabara hizo kujaa michanga na vumbi kiasi cha kutojulikana kama ni za kiwango cha lami au la. Hii si mara ya kwanza kwa Mh. Nahodha kujitolea kusafisha Halmashauri ya Manispaa ya Zanzibar. Hata hivyo pamoja na juhudi zake hizo kwa Halmashauri hiyo ambayo kipindi fulani kupitia kwa Mkurugenzi wake Mr Mabrouk Makame Jabu ilikuwa ikidai kupewa hadhi ya Jiji(Sina hakika kama tayali ombi hili limeshakubaliwa)bado mji huo umeendelea kuwa mchafu.

Juhudi zote za Waziri Kiongozi zimekuwa na mafanikio ya muda mfupi, kwani huwa zinafanyika katika mtindo wa Operation ambao siku zote huwa hauna uendelevu wa aina yoyote, kwani operation inapokwisha shughuli nzima uwekwa kando na watu wakaendelea na shughuli zao zingine, huku wakisubiri kutokea kwa operation mpya. Watendaji wengi na hasa wa kimacha chini upenda aina hii ya utendaji kwani ndio wakati wao wa kuwa na kipato zaidi kutokana na overtime. Kwa Waziri Kiongozi ambae mara kwa mara amekuwa akisisitiza kuwepo na utendaji wa uendelevu katika shughuli za serikali, kilimo na biashara huku akiongoza kufanya operation za usafi ni kichekesho kitupu. Inakuaje unahutubia kila siku mambo ya uendelevu huku kazi unafanya za kizima moto kama sio vituko vitupu!

Moja ya barabara ambao siku zote huwa inajaa michanga na kusababisha vumbi la kuweza kusababisha chafya kila baada ya sekunde kadhaa, na hatari ya kupata kikohozi kikali ni barabara ya Benjamin Mkapa(zamani creek road). Barabara hii ndio inatenganisha Mji Mkongwe na Ng'ambo, ni moja ya barabara yenye pilika kubwa kabisa katika Zenj ikipitiwa na magari mengi zaidi, itumiwayo na wapanda baiskeli wengi zaidi na wapanda vespa,huku wakipigana vikumbo na mamia ya watembeao kwa miguu. Ndio barabara pekee visiwani humo yenye taa za kuongozea magari, kwa ufupi ndio barabara maarufu kabisa visiwani humo.

Kwa miaka nenda rudi barabara hiyo imekuwa ikifagiliwa pasipo kutakata na sasa naona imeshakuwa sugu, na kama hakuna mipango ya kuweza kujua ni kwa nini barabara hiyo haikosi vumbi licha ya kuwa ndio picha ya mji wa Zenj, kamwe haitokuja kuwa safi na ni wazi kuwa vumbi litaendelea kuwepo tu, licha ya ombi la watendaji wa Halmshauri hiyo kununuliwa gari la kufagia barabara hivi karibuni.


Barabara hiyo pamoja na kupita katika bustani za Mnazi Mmoja, Jamhuri, Donge na viwanja vya Malindi, haikupaswa kabisa kuwa na vumbi. Lakini kutokana na sababu za kutokuwa na mipangilio mizuri vumbi limeendelea kuwepo licha ya ufagiaji wa kila siku. Kitu cha kwanza ambacho kina kasoro kubwa katika barabara hiyo ni kukosekana kwa njia ya watembeao kwa miguu. Kama kungekuwa na njia hiyo ingetumika vile vile kama buffer ya kutenganisha barabara na sehemu zinazoingiza michanga barabarani na kusababisha vumbi. Aidha aina za kuegesha magari na hasa teski katika barabara hiyo unachangia kuingia kwa michanga barabarani, kuna maegesho ya magari ya mizigo na haya uegeshwa karibu kabisa na barabara hiyo, hivyo uchangia kuingia kwa michanga barabarani.Kwa upande mwingine Feeder road zinazo ingia katika barabara hiyo vile vile uchangia kuingiza michanga.

Ili kumfanya Waziri Kiongozi aendelee kufanya kazi zake za kawaida, badala ya kutafuta fagio, upo umuhimu wa lazima kuona kuwa barabara ya Benjamin Mkapa inafanyiwa mabadiliko makubwa ili kukidhi mahitaji ya watumiao barabara hiyo ambao ni maelfu. Kuna umuhimu wa kuweka njia kwa watembeao kwa miguu ambayo iwe inafanya kazi ya kuzuia kuingia kwa michanga katika barabara hiyo. Kuboresha maegesho ya teski na magari ya mizigo kama kituo cha daladala kilivyoboreshwa, kufanyia matengenezo feeder roads ambazo huingiza michanga kwa wingi na hasa wakati wa masika. Kuangalia tena eneo la Darajani kwani nalo linachangia sana katika uchafuzi wa barabara hiyo. Maeneo mengine kama Mkunazi,Donge, Ben Bella na Ofisi za Zec zinatakiwa kuangaliwa kwa vizuri zaidi.

Kwa utengenezaji wa njia ya wapita kwa miguu, Halmashauri ya Manispaa ya Zenj, inaweza kufanya kazi hiyo kwa kutumia mitambo yake mikubwa ya kutengeneza vigae, kwa kuweka vigae pembeni ya barabara hiyo. Hizo milioni 135,000,000 ambazo Manispaa wanahitaji kwa ununuzi wa mashine ya kusafisha barabara mnaweza kuwapa japo nusu yake ili waweze kutumia kwa utengenezaji wa vigae.

No comments: