E-governance for African Municipalities...Ni Wizi Mtupu....!
Zenj mara nyingi imekuwa ikiingia kwenye rekodi mbalimbali barani Afrika na Duniani kutokana na matukio ya maisha maendeleo na teknologia. Rekodi kadhaa zimeandikwa ndani ya visiwa hivyo, hivyo kuongeza umaarufu wake na wakati huo huo kuboresha huduma mbalimbali kwa wananchi wake.
Zanzibar inaendelea kujivunia rekodi zake mbalimbali hadi wakati huu ingawa zingine zilishindwa kuendelezwa na hivyo kubakia kwenye kumbukumbu tu na kuwa hadithi kwa vijana kutambiana na hasa wanapokuwa katika ubishi na wenzao wa bara. Mapema mwaka huu Zenj iliibuka tena na kujiwekea rekodi nyingine mpya katika Afrika ya Mashariki, na iwapo rekodi hii itakuwa na mafanikio hapana shaka itaanza kusambaa taratibu kwa nchi zote za jirani. Safari hii rekodi hiyo haikupokelewa vizuri na nchi jirani, hata hivyo nina hakika baada ya muda wataifuata tu. Hii ni rekodi ya kuwa nchi ya kwanza katika Afrika ya Mashariki kutoa leseni ya udereva yenye kumbukumbu zote muhimu za mwenye leseni pamoja na namba yake ya ulipaji kodi. Hii ni hatua nzuri na kubwa kwa nchi zenye matatizo ya ukusanyaji wa kodi.
Mafanikio haya yote siku zote yanakuwa na lengo moja kubwa la urahisishaji wa utendaji na uongezaji wa ufanisi katika utoajo wa huduma, ambapo ni hatua muhimu ya kuondokana na ukiritimba ambao umekuwa ukichangia kwa asilimia kubwa kuwepo na rushwa na hatimae ufisadi.
Hata hivyo sio mambo yote ambayo yamekusudiwa kufanikisha na kurahisisha utoaji huduma katika Zanzibar yamefanikiwa. Ni watu wachache ambao watakumbuka kuwepo na mradi wa E-governance for African Municipalities kwa Manispaa tano tu barani Afrika ikiwemo Zanzibar, Manispaa zingine zilikuwa ni Bamako (Mali), Maputo (Mozambique), Niamey (Niger) na Lusaka (Zambia). Lengo la mradi huu ambao ulianza mwaka 2001 ilikuwa ni kuziunganisha Manispaa hizo tano katika mtandao mmoja aidha kuwezesha Manispaa hizo kuwa karibu na wananchi wake kwa utoaji wa huduma ya habari kwa njia ya mtandao. Kwa Manispaa ya Zanzibar kupitia mtandao uliofungwa katika Idara zake zote ilikusudiwa kurahisisha ubadirishanaji wa habari za kiutendaji katika idara hizo kwa njia ya umeme(electronically). Zaidi ilikusudiwa kutoa habari juu upatakanaji wa leseni mbalimbali kwa wananchi wake kupitia kwenye tovuti yake, pamoja na wananchi hao kupata nafasi ya kutumia mtandao huo bure katika sehemu maalumu kwa ajili ya kupata habari juu ya sheria ndogo ndogo mpya, muhtasari wa vikao vya kamati za Manispaa na Baraza Kuu, ukusanyaji wa mapato na matumizi yake na kuweza kujionea bajeti ya Manispaa hiyo ndani ya mtandao.
Mradi huu ambao ulikuwa unadhaminiwa na DANIDA/UNESCO, ulikamilika mwaka 2003, ambapo pamoja na Manispaa kupatiwa vitendea kazi vyote na taaluma kwa watendaji wake, wadhamini hao waligharamia na uanzishaji wa tovuti ya manispaa hiyo, ambayo tokea mwaka 2003 hadi leo hii imedumaa. Huu ni wizi mtupu.
Mradi huu ulikuwa wa thamani ya dola za kimarekani elfu arobaini haukuweza kuendelea kama ilivyokusudiwa kwa sababu zisizo na msingi zaidi ya kuendeleza tabia za ukiritimba ndani ya vyombo vya utoaji wa huduma ambapo ni wizi mtupu.
Madiwani ambao kwa namna moja ama nyingine ndio wanao wawakilisha wananchi wao katika Manispaa, ilitegemewa wawe mstali wa mbele kuona huduma hii muhimu iliyokuwa inaweza kuwapunguzia bughuza za waombaji wa fomu kugonga milango ya nyumba zao alfajili, kuwabana wahusika kuikamilisha tovuti hiyo ili kuwezesha wananchi kujaza fomu online walikaa kimya na kufumbia macho kudumaa kwa mradi huu ili waweze kuendelea kuwazungusha wananchi wao juu ya upatikanaji wa fomu mablimbali... Huu ni wizi mtupu!
Mkurugenzi wa Manispaa ama kwa kutojua ama kushindwa kwenda na mabadiliko katika utoaji wa huduma nae alishindwa kuendeleza mradi huu. Kwa nafasi yake angeweza kuhakikisha kuwa kila Idara inapeleka taarifa zake za mapato katika tovuti hiyo na kila idara inaweka fomu za maombi katika tovuti hiyo na hivyo kupunguza ama kuondoa foleni zisizo na ulazima wowote katika Ofisi ya manipaa hiyo. Hata hivyo kwa miaka saba sasa amekaa kimya tokea alipoweka ada za kupaki magari mwaka 2003... Wizi mtupu!
Mstaki Meya ambae huwa anaalikwa kwenye matukio muhimu yote yanayofanyika katika Manispaa yake nae ameshindwa kumbana afisa uhusiano kuona kuwa Matukio muhimu yote yanawekwa katika tovuti hiyo, hii ingekuwa ni njia mojawapo ya kuelekea kuweka hata matangazo ya matukio kwa njia ya kulipia hivyo kuifanya tovuti hiyo kuingiza mapato. Nae kama wengine ameamua kukaa kimya... Ni wizi mtupu!
Tovuti ya Baraza la Manispaa ilifanyiwa marekebisho kwa mara ya mwisho mwaka 2003, na hata yale ambayo yamo katika tovuti hiyo yanatia kichefuchefu. Yaliyoandikwa humo yana uhusiano mdogo kabisa na shughuli za Manispaa hiyo huu ni wizi mtupu. Hata design na layout ya tovuti hiyo ni vichekesho vitupu... Yaaaani ni Wizi mtupu!
No comments:
Post a Comment