Tuesday 24 February 2009

Zanzibar Hakuna Sheria za Ujenzi?

Zanzibar kama nchi, mji mkuu wake ni Zanzibar ambao unaundwa na Mji Mkongwe na Ng'ambo, kiutawala upo katika mkoa wa Mjini Magharibi. Mji wa Zanzibar unapata huduma zake kupitia Halmashauri ya Manispaa ya Zanzibar na Mamlaka ya Hifadhi na Uendelezaji wa Mji Mkongwe.

Halmashauri ya Manispaa kama halmashauri zingine duniani imepitia katika mabadiliko mengi ya kiutawala na sheria za kuongoza mji huo na hasa katika suala zima la ardhi na maendeleo yake kwa kushirikiana na idara zingine kama ofisi ya Mkuu wa wilaya, ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Kamisheni ya Ardhi na baadae Idara ya Mipango Miji na Idara ya Ardhi.

Masterplan ya kwanza kabisa ya mji wa Zanzibar ilitolewa mwaka 1923 chini ya sheria ya mji(Town Decree Cap 79). Master plan ilitolewa kutatua matatizo ya ukuaji wa mji kiholela, kupanua wigo wa miundo mbinu na kurahisisha mizunguko katika mji huo ambao ulikuwa na watu 35000 huku asilimia 30 ya watu hao wakiishi Mji Mkongwe na asilimia 70 wakiishi Ng'ambo sehemu iliyokithiri kwa ujenzi holela.

Mwaka 1958 kulifanyika mabadiliko katika Master plan kwa kuingizwa kwa "Town Scheme" chini ya sheria ya mwaka 1955- "Town and Country Planning Decree" ambapo lengo lilikuwa kuandaa rasimu ya usafirishaji/usafiri katika mji mkongwe na kuendeleza maeneo ya wakaazi yaliyopimwa chini ya viwango huko Ng'ambo (semmi planned settlements)

Master plan ya pili "The Town Master Plan -1968" ilifanywa na Wajerumani, ikiwa na lengo la kuboresha zaidi maeneo ya Ng'ambo ambayo yalikuwa yakipanuka kwa kasi, huku umuhimu mkubwa ukiwekwa kwenye upatikanaji wa huduma muhimu kama vile mifereji, taa za kwenye mitaa na misingi ya maji taka.
Mafanikio yake ni pamoja na Majumba ya Mjeru pale Kikwajunina Majumba ya Kilimani.

Master plan kubwa na ya mwisho ilitolewa mwaka 1982 na wataalmu kutoka China. Pamoja na mabo mengine, master plan hiyo iliangalia zaidi kupanuliwa kwa mji wa Zanzibar kwa kupima maeneo mengine mapya ili kuruhusu nafasi kubwa zaidi kwa ya asilimia 68 ya wazenj waliokuwa wamebanana kupatiwa maeneo ya ujenzi huku wengi wakiishi katika maeneo yasiopimwa kisheria, aidha kutoa nafasi kubwa zaidi ya ujenzi kuanzia nyumba za kuishi shule na maeneo ya biashara, ilitizama vilevile kupunguza umwagaji wa maji taka baharini na kuzuia tabia iliyoanza ya kujenga nyumba katika maeneo yenye mafuriko.

Tokea master plan hiyo ya wachina kumekuwepo na nyongeza mbili moja ikiwa ni ya mwaka 1996 The Tourism Zoning Plan ambayo iliingizwa kwenye Master plan kukidhi mahitaji ya mahoteli na maeneo ya kitalii. Ya pili ni pendekezo la kuimarisha na kuanzisha miundo mbinu hasa katika maeneo ya Ng'ambo iliyopendekezwa na Zanzibar Sustainable Programm (ZSP) mwaka 1998.

Kwa nyakati tofauti maendeleo ya ujenzi na udhibiti wake yalikuwa yakisimamiwa na Joint Building Authority (JBA)ambayo ilianzishwa chini ya sheria ya Town and Country Planning Decree (cap 85) ya mwaka 1955, ikiwa na wajumbe watatu toka ambao ni Mkuu wa Afya, Mkuu wa Wilaya na Building Inspector. Kazi zao kubwa ilikuwa ni kutoa vibali vya ujenzi wa aina zote ndani ya mji wa Zanzibar na kudhiti ujenzi ndani ya mji huo kwa mujibu wa sheria ya mji. "Town Decree Cap 79 Subsidiary"

Mwaka 1969 SMZ ilizivunja Halmshauri za Miji na hivyo ukawa mwisho wa awamu ya kwanza ya JBA. Awamu ya pili ya JBA ilianza tena mwaka 1986 baada ya kurejeshwa kwa serikali za mitaa katika ikiwa na wajumbe wengi zaidi huku mkuu wa mkoa akiwa ndie mwenyekiti wake. Wajumbe wengi walitoka baraza la Manispaa, wakifuatiwa na wajumbe toka idara ya Ardhi, idara ya Upimaji na Mhandisi wa ujenzi. Kazi za JBA ziliendelea kufanyika chini ya sheria na taratibu za ujenzi kama zinavyooneshwa katika Cap 79 Subsidiary. Kati ya Mwaka 1969 na 1986 shughuli za ujenzi zilikuwa zikisimamiwa na serikali za majimbo, pasipo kufuata sheria yoyote za ujenzi zaidi ya uzoefu uliopatikana katika Cap 79 ya Town Decree.

Mwaka 1994 Sheria ya uendelezaji na uhifadhi wa Mji Mkongwe ilianza kufanya kazi, hivyo kuitoa JBA kama mdhibiti wa ujenzi katika eneo la Mji Mkongwe. JBA iliendelea kufanya kazi kufuata mipaka ya Master plan ya mwaka 1982 nje ya Mji mkongwe hadi mwaka 1995 ambapo kulitokea tena mgongano wa sheria. Mwaka 1995 ilianzishwa sheria mpya ya halmashauri za Miji Zanzibar, ikichukua sehemu kubwa za sheria za Town decree na kupunguza ukubwa wa Manispaa ya Zanzibar hali kadhalika kuibana zaidi JBA katika utendaji wake.

Kufikia hapa kazi za JBA ziliendelea kufanyika ila ni kwa ubabe tu, kwani chini ya sheria ya mwaka 1995 ya Manispaa ilionekana wazi kuwa JBA haikuwa na nafasi ya utendaji katika manispaa yenyewe na wilaya ya Magharibi. Ikiwa chini ya Mkuu wa Mkoa kama mwenyekiti na Baraza la Manispaa kama katibu, JBA iliendelea kufanya kazi huku ikijua inafanya hivyo kinyume na sheria na taratibu. Udhaifu wa Halmashauri ya wilaya ya Magharibi, nguvu ya kisheria ya Idara ya Ardhi na Idara ya Upimaji iliipa uhai kidogo JBA kutokana na kuwa na wajumbe toka katika Idara hizo.

Mwaka 2000 JBA ilivunjwa rasmi na moja ya sababu kubwa ya uvunjwaji wake ilikuwa ni zoezi la uvunjaji wa nyumba katika mitaa kadhaa ya Mkoa wa Mjini Magharibi iliyofanyika katika mwaka 1996, katika vyanzo vya maji, karibu na njia ya grid ya umeme wa Kidatu na maeneo mengine yaliyovamiwa, ambapo ilionekana zoezi zima limefanyika kisiasa zaidi kuliko kufuata taratibu. Manispaa kwa upande mwingine chini ya sheria ya mwaka 1995 waliona kuwa JBA ni mzigo kwao na walitaka ichukuliwe na asasi nyingine yoyote ya serikali. Kuvunjwa kwa JBA kulitoa nafasi ya kuanzishwa kwa UDCA (Urban Development Control Authority)ambayo ilianzishwa chini ya sheria ya 1955 ya Town and Country Planning decree ambayo ipo chini ya Wizara ya Ardhi na Upimaji. Safari hii Mwenyekiti wake akiwa ni Mkurugenzi wa Manispaa na katibu akiwa ni Town Planner wa Manispaa na wajumbe wengine 10 toka katika asasi zingine zinazohusika na ujenzi. Kwa ufupi UDCA ipo lakini haina nguvu kisheria kutokana na kuwepo kwa sheria ya Halmashauri ya Manispaa ya Mwaka 1995. Aidha sheria iliyotumika na Waziri huyo haina nafasi katika Halmashauri ya Manispaa, kwani Mkurugenzi wa Halmshauri anawajibika kwa Waziri wa Tawala za Mikoa na si venginevyo. UDCA inaendelea kufanya kazi kutokana na mazoea ya kuwepo na kitengo kama hicho katika miaka iliyopita.

Tukio lililotokea hivi karibuni la uvunjaji wa nyumba na misingi ya nyumba katika shehia ya Tomondo lililo fanyika chini ya amri ya Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Mhe. Abdallah Mwinyi, licha ya kuwa ni la kinyama halikufuata utaratibu wowote wa kisheria, zaidi limenikumbusha mojawapo ya sababu ya kumwondoa Mkuu wa Mkoa katika kudhibiti ujenzi visiwani humo. Aidha limenikumbusha kuwa Zanzibar Mjini hakuna sheria ya Ujenzi na kuna asasi nne zote hizo zikidai kuhusika na maendeleo ya ardhi katika mji huo na kufanya kuwepo na vurugu tupu katika kusimamia masuala ya ujenzi katika Mkoa huo wa Mjini Magharibi.

Aidha kuna umuhimu mkubwa kuona kuwa migongano ndani ya Mipaka ya Master plan ya mwaka 1982 inakwisha na kuna umuhimu mkubwa kuona kuwa Idara ya Upimaji, Idara ya Ardhi, Mamlaka ya Hifadhi na Uendelezaji Mji Mkongwe, Halmshauri ya Manispaa ya Zanzibar, Halmashauri ya Magharibi, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Ofisi ya Mkuu wa wilaya ya magharibi pamoja na ofisi ya Mwanasheria mkuu wa serikali wanakaa pamoja na kuamua ni sheria gani ya ujenzi itumike katika eneo la master plan ya mwaka 1982. Kwani kwa sasa hakuna sheria inayotumika zaidi ya wizi mtupu. Yaani inatia aibu kwa wizi huu wa mchana kweupe, huku wanaoumia ni wananchi wasio jua wafuate sheria gani kupata kibali halali cha ujenzi wa nyumba zao.

No comments: