Wednesday 3 March 2010

Umeme sasa ni Machi 9 - ZECO


IMEDAIWA jana kuwa huduma ya umeme visiwani Zanzibar inatarajiwa kurudi Machi 9 baada ya kukamilika kazi za utengenezaji wa kituo cha kupokea umeme kilichopo Fumba, Mkoa wa Mjini Magharibi

Kaimu Meneja wa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO), Hassan Ali Mbarouk, aliwaambia waandishi wa habari kuwa kutokana na kukamilika kwa matengenezo cha Fumba huduma hiyo itarejea punde na kuwaahidi wananchi wasiwe na wasiwasi huduma hiyo itarejea siku hiyo.

Alisema kazi iliyobakia ni kuunganisha waya za umeme kutoka nchi kavu na baharini na kazi hiyo ya kuunganishwa kwa waya kutoka katika vituo vya Fumba hadi Ras Kiromoni Tanzania Bara itachukua muda wa siku tatu.

Alisema hadi Jumapili ijayo kazi ya matengenezo itakuwa imemalizika na matarajio Machi 8 kutafanyika vipimo vya majaribio na Machi 9 ndiyo huduma hiyo inatarajiwa kuwashwa na kurudi rasmi kwa umeme visiwani humo.

Pia aliweza kuwaambia waandishi wa habari kuwa kuchelewa kwa huduma hiyo kumesababishwa na mafuta yaliyokuwemo ndani ya waya zinazoleta umeme kutokuwa safi na kulazimika kusafishwa kwa muda wa siku tatu.

Wakazi wa visiwani humo wamekosa huduma hiyo ya umeme tangu Desemba mwaka jana, baada ya kutokea hitilafu katika kituo cha kupokea umeme huo kutoka Ras Kiromoni hadi Fumba mjini Unguja.

No comments: