Tuesday 18 August 2009

Saturday 15 August 2009

MMhm Huyu Nae...! CCM Maisara


Mdau wa CCM Maisara, sehemu maarufu hapo Zenj!

Thursday 13 August 2009

Maandalizi ya Kongamano la Kitaifa la Wanablogu



Je wewe ni mwanablogu (Blogger) au mdau wa habari na mawasiliano kwa umma kwa kutumia mtandao? Kama jibu ni ndio, tafadhali unaombwa kujiorodhesha kwa ajili ya maandalizi ya Kongamano Maalumu la Kitaifa kwa ajili Wanablogu (Bloggers) na wadau wa habari na mawasiliano wa Tanzania (Tanzanians Bloggers Summit) linalotarajiwa kufanyika Desemba mwaka huu jijini Dar-es-salaam,Tanzania.

Dhumuni la kongamano hili ni Kuelimishana, Kufahamiana, Kuamsha Utambuzi Rasmi Kuhusu Tekinolojia ya Blogu na Mawasiliano ya Umma kwa Kutumia Mitandao, Kusaidia Utambuzi Rasmi juu ya mchango wa blogu nchini Tanzania kama chombo muhimu cha habari na mawasiliano, Kuelimishana jinsi gani blogu zinaweza kutumika katika kuleta maendeleo katika nyanja za kijamii, kisiasa na kiuchumi, kuburudisha, kukuza utamaduni nk.

Wataalamu mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi wataalikwa kutoa mada na mafunzo mbalimbali kuhusiana na tekinolojia ya kublogu, zana nyinginezo za mawasiliano mtandaoni kama vile mitandao jamii(social networking), online forums nk.Kutakuwa na vipindi vya maswali na majibu.
Ili kufanikisha maandalizi ya Kongamano hili la kihistoria, kujiorodhesha kwako ni muhimu sana. Muda wa kujiodhoresha ni kuanzia tarehe 12/8/2009 (Jumatano) mpaka 12/9/2009 (Jumamosi) tu.

Kinachohitajika ili kujiandikisha ni :
Jina Lako, Anuani yako ya barua pepe (E-mail), Mahali Ulipo au unapoishi (Nchi,mji nk),Namba ya Simu (sio lazima) na Anuani au URL(Universal Resource Locator) ya blogu yako (mfano www.kongamano.blogspot.com/wordpress.com/.com/typepad nk). Vyeti vya Ushiriki vitatolewa kulingana na habari utakazoziorodhesha hapa.
Unaweza kujiorodhesha kwa kutuma ombi lako kwa barua pepe kwenda; summit@bongocelebrity.com.
Zingatia tarehe za kujiandikisha.
Ni mwezi mmoja tu! Asante kwa ushirikiano. UMOJA NI NGUVU!

Bandarini Zanzibar

Wednesday 12 August 2009

Usafirishaji wa Mizigo Zenj...








Usafirishaji wa mizigo kwa kutumia Wanyama ulipigwa marufuku kufanyika ndani ya mipaka ya Halmashauri ya Manispaa ya Zanzibar mara baada ya Mapinduzi. Hata hivyo kidogo kidogo magari ya mizigo ya Punda na Ng'ombe yamerudi tena kubeba mizigo ndani ya Manispaa.




Mkokoteni huko Pemba

Tuesday 11 August 2009

Friday 7 August 2009

Wapemba waendeleza ual-qaeda...!


Baada ya Uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995,Visiwa vya Zenj vilishuhudia vituko kibao, ikiwa ni pamoja na mabomu ya baruti na ya petroli yakilipuriwa katika maeneo mbali mbali ya visiwa hivyo. Toka katika maakazi ya watu, ofisi za serikali na hata sehemu nyeti kama za usambazaji wa umeme visiwani humo zilipata makasheshe ya milipuko ya mabomu. Mabomu mengine yaliweza kulipuka huku mengine yakishindwa kulipuka.

Kipindi hicho kilikuwa ni kabla ya ulipuaji wa mpigo(sambamba)wa mabomu kuanza. Ni katika mwaka 1998 ambao ulipuaji wa sambamba uliponza na kukikuhisha kikundi maarufu cha Al-Qaeda, pale walipoweza kulipua kwa wakati mmoja ofisi ya balozi wa Marekani katika majiji ya Dar es Salaam na Nairobi.

Hapo Majuzi nyumba za Masheha huko Pemba ziliweza kulipuliwa kwa staili hiyo na kufanya wengi kufananisha milipuko hiyo kama ile ya kundi la Al-Qaeda. Huu ni muendeelezo wa ulipuaji wa mabomu huko Pemba kwa madai ya kuwa Masheha wanawanyima wakaazi wa huko kuandikishwa kwenye daftali la kudumu la kupiga kura.

Wapemba katika hili wapo mbele, kwa kumbukumbu za haraka haraka, tokea uchaguzi wa mwaka 1995, kumekuwepo na vituko vingi sana huko Pemba, kama vile vya kugeuza visima vya maji kuwa vyoo, kupaka vinyesi katika skuli,ili kuzuia wanafunzi kusoma, kunyang'nya polisi silaha na kuteka kituo cha polisi, kususia shughuli za maziko na arusi, kubagua watu wa kufanya biashara nao, talaka kwa wanandoa kutokana na tofauti za kisaisa na vituko vingine kaza wa kaza.

Pamoja na yote, ili la mabomu ambalo linaendela sasa, linatakiwa kuchukuliwa hatua za haraka la kulidhibiti, kwani litaweza kuleta madhara makubwa sana hapo mbele, na hasa siku ambayo Wapemba hao watakaweza kuwa na mabomu yenye nguvu(haya ya sasa hayana nguvu kubwa)au mabomu ya sumu! Hivyo basi ni vema kwa vyombo vinavyohusika kuwatafuta watu hawa wanaolipua mabomu na kuwafikisha kwenye vyombo husika. Na ni wakati wa kuanza kuitumia sheria ya magaidi iliyotungwa mara baada ya milipuko ya Dar na Nairobi.

7th August 2009

Nyumba za Masheha wawili zalipuliwakwa mpigo

Milipuko miwili tofauti imetokea sambamba nyumbani kwa masheha wawili kisiwani Pemba na kusababisha zaidi ya watu 30 kunusurika kifo.
Akizungumza na Nipashe juu ya matukio hayo yanayofanana na ile milipuko ya kupanga ya kikundi cha kigaidi cha Al- Qaeda kwa kulipuka kwa wakati mmoja, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, Yahya Bugi, alisema matukio hayo ni ya kupanga.
Alisema katika tukio la kwanza, watu wasiojulikana walitega bomu la kutengenezwa kienyeji kwa kutumia baruti (TNT) na kulilipua nyumbani kwa Sheha wa Mihogoni, Salim Said Salim (59).
Kamanda huyo aliliambia Nipashe kwamba nyumbani kwa Sheha Salim kulikuwa na mkusanyiko wa watu waliokuwa wakihudhuria harusi nyumbani kwake saa sita usiku wa kuamkia jana.
Alisema bomu hilo lililipuka wakati Sheha na wageni wake wakiwa wamelala na kusababisha athari kubwa kwenye ukuta wa nyumba yake na mabati sita yaliyoezekwa nyumba hiyo kung’oka.
Kamanda Bugi alisema kwa mujibu wa Sheha Salim, walisikia kishindo kikubwa kikitokea nyuma ya nyumba yao na baada ya kukimbilia katika eneo hilo waliwaona vijana wawili wakikimbilia eneo lenye migomba.



Zaidi: tembelea Nipashe

Thursday 6 August 2009

Pinda amefulia...


Kwa kauli yake juu ya Muungano Waziri Mkuu Mizengo Pinda amefulia na ameonyesha ufahamu mdogo juu ya Muungano huu. Kauli yake ya kuondoa kero za muungano ni kuifuta SMZ haiwezi ikaachwa hivi hivi. Kauli ambayo aliitoa huku akijua kuwa hakuna dalili zozote za sasa za SMT kujaribu kuondoa kero za Muungano achilia mbali jitihada za kuona kuwa Muungano unakwenda vizuri zaidi ya kuburaza upande mmoja wa Muungano. Kauli yake inaweza kuwa sahihi iwapo Muungano huu utakuwa hauna kero yoyote na nchi zote mbili kuridhia kuwa hakuna kero.

Zaidi Pinda anahitaji kupatiwa tuition ya haraka kuhusu Muungano na mambo yote ambayo yahusianayo na Muungano huo. Hii itamuwezesha kujua na kupata ufahamu mkubwa wa Muungano huu kabla ya kujikuta akishitumiwa na kuandamwa na Katiba na kukimbilia kulia.

Wednesday 5 August 2009

Tuesday 4 August 2009

Mwakilishi adai wizi wa watoto umekithiri Zanzibar


WAJUMBE wa Baraza wameishauri Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kufuatilia kwa kina upoteaji wa watoto katika maeneo mbalimbali pamoja na kushughulikia suala la utumiaji wa dawa za kulevya nchini.

Walitoa ushauri huo jana walipokuwa wakichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Kazi Maendeleo ya Vijana, Wanawake na watoto kwa mwaka wa fedha 2009/10 katika kikao cha baraza la wawakilishi kinachoendelea Mjini Unguja.

Mwakilishi kupitia Wanawake (CCM), Raya Suleiman Hamad, alisema kuna haja kwa serikali kuanzisha uchunguzi huo kwani watoto wengi wanapotea ovyo katika mitaa yao, huku wazazi wao wakiwa wanahangaika kuwatafuta bila ya mafanikio.

Alisema kwamba inavyonekana wapo baadhi ya watu wanaoendesha biashara ya kuiba watoto jambo ambalo tayari limeanza kuwatia hofu baadhi ya wazazi nchini.

Mwakilishi huyo alisema kwamba watu wanaoendesha vitendo hivyo hutumia njia za kuwahadaa kwa kuwafuata watoto na kuwapa fedha kisha wanawasihi wawafuate ili wakawanunulie nguo.

Mwakilishi huyo alitoa mfano katika mtaa wa Nyerere kwamba kuna kesi za kupotea watoto wanne na kwamba hadi sasa hawajapatikana pia hawajulikani walipotea katika mazingira gani.

Aliitaka serikali ichukue hatua za kufanya utafiti juu ya suala hilo kwa vile tayari limeanza kuwatisha wananchi na linaweza kusababisha madhara makubwa baadaye

Alisema wakati serikali ikilitafakari hilo, ni vyema hivi sasa kuangaliwa uwezekano katika bandari na Viwanja vya Ndege watu wanaoonekana kubeba watoto wakahojiwa uhalali wao.

Mwakilishi huo pia alizungumzia suala ubakaji wa watoto kuendelea ikiwa pamoja na wagonjwa wa akili na kutaka vyombo vya sheria kutekeleza majukumu yao bila ya upendeleo kwani matendo kama hayo yakiachwa yanaweza kuhatarisha usalama kwa watoto .

Akitoa mifano Mwakilishi huyo alisema iliyowahi kujitokeza kisiwani Pemba baada ya mtoto mmoja kubakwa lakini kesi yake ilipopelekwa Polisi wamekuwa wakishindana na Polisi kwa kuwaeleza wahusika hawana la kufanya na waende wakamkamate mhusika wampeleke kituoni hapo.

Mwakilishi huyo pia alisema ni lazima serikali iandae mkakati maalum wa kukabiliana na tatizo hilo kwani suala la madawa ya kulevya linaonekana kama vile limeshindikana kutokana waletaji na wauzaji wa dawa hizo kuwa wanafahamika lakini hawachukuliwi hatua zozote za kisheria wakati vijana wengi wanazidi kuharibika na utumiaji wa madawa hayo.

Friday 31 July 2009

SMZ:- Serikali Iliyokosa Dira




Ilikuwa ni katika awamu ya mwisho ya Komandoo, ambapo wazenj wengi walipata fursa ya kudhaminiwa na serikali yao ili kuongeza elimu yao na taaluma zao. Lengo lilikuwa ni kusomesha wazenji wengi kadiri uwezo wa serikali ya SMZ inavyoruhusu. Na ni kipindi hikohiko ambapo kulikuwa na wimbi la wakimbizi wa Kizenj kukimbilia hifadhi huko Uingereza. Ni kipindi hikohiko ambapo Komandoo alionekana kuwa ni msaliti baada ya jitihada zake za kubadili katiba kugonga ukuta. Zaidi ni kipindi hicho hicho ambacho wazenj waliona ongezeko kubwa la mapato yao na mabadiliko mengi katika miji yao. Kwa ufupi ni kipindi ambacho wizara ya fedha ilikuwa ni maarufu zaidi katika historia ya SMZ, ikifanya kazi nje ya uwezo wake huku ikivamia kazi za wizara zingine.

Ilikuwa ni mwaka 1996 ambapo SMZ kupitia Wizara ya fedha ilioanza kupeleka wafanyakazi wake na wasio wafanyakazi kwenda kusoma kwa wingi, hata hivyo kozi nyingi zilikuwa zile ambazo zinaweza kufanyika Tanzania Bara. Zenj ilishuhudia masekretari wakipelekwa kusoma UK na Malaysia, wakati kuna chuo cha Uhazili hapo Tabora, kozi za zilikuwa za chini ya mwaka mmoja na wengi hawakurudi tena kupiga chapa na kupokea wageni na sasa wanakula benefit zao huko UK wakijiita Wasomali ama Warundi. Na ni baada ya kuona wakimbizi wa kizenj wakifaidi benefit za UK. Kumbuka kuwa licha ya tofauti za kisiasa zinazo onekana nje ya wazenj, wengi wao wapo pamoja kimashauri na kimaisha kwani kwa namna moja ama nyingine wamehusiana.

Mwaka mmoja baade bila kupima mafanikio ya wanafunzi waliotangulia, SMZ ilikusanya masekreatari na wafanyakazi wengine na wake wasio na kazi na kuwapeleka Malaysia ili kuongeza ujuzi wao. Kwa wale ambao walikuwa hawana ajila katika SMZ walihaidiwa kupewa ajila mara watakapo maliza masomo yao.

Mtiririko mzima wa kwenda huko ulisimamiwa na wizara ya fedha, wala hapakuwa na haja ya kwenda Idara ya Utumishi ili kuweza kupata nafasi ya kwenda huko. Ilikuwa ni kwenda moja kwa moja wizara ya fedha na kueleza adhma yako ya kusoma, wao walitoa mkataba wao na biashara kuishia hapo hapo.

Kama katika mwaka uliotangulia wengi walikuwa ni masektretari, wakifuatiwa kwa karibu na wanafunzi waliopenda kusoma Computer Science, huku wengine wakitaka kusoma Business Management na baadhi kutoka katika idara za uhandisi. Tatizo kubwa lilikuwa hapa kwenye Uhandisi, kwani chuo ambacho SMZ iliingia nao mkataba hawakuwa na fani nyingi za uhandisi zaidi ya umeme! Hivyo kupelekea wafanyakazi toka idara ya Maji, TVZ, Manispaa kulazimika kusomea umeme! Kulikuwa na kundi lingine ambalo lilipenda kusomea Uhasibu na kundi la Sheria, hata hivyo wengi wao walipenda kozi hizo kutokana na ndota zao na walipoanza masomo walijikuta wakishindwa vibaja. Mbaya zaidi Idara ya Utumishi ilikataa kabisa kuwatambua kwa wale wachache waliorudi tena Zenj...

Muda wa kozi unatofutiana, hivyo masekretari walikuwa ndio wa mwanzo kurudi Zenj, katika kipindi chote ambacho walikuwepo hapa Kuala Lumpar na Petaling Jaya, Wanafunzi walishuhudia ziara zisizo na kikomo za viongozi wa ngazi za juu, malipo ya posho zao kwa wakati na kadhalika. Maisha yalikuwa ni mazuri sana na yenye neema nyingi.

Baada ya masekretari kuondoka, ndipo picha halisi ya SMZ kwa wanafunzi wake ilipoonekana. Huduma nyingi muhimu zilipunguwa ama kusimamishwa kabisa. Hii ilijenga chuki na hasira kwa wanafunzi juu ya serikali yao. Mbaya zaidi ni kujua kuwa hata wale ambao wamerudi Zenj wameshindwa kutambuliwa na Idara ya Kazi, hivyo ni sawa kama hawakusoma chochote kile.

Wanafunzi wengi walianza kufikilia kama kuna umuhimu wowote wa kurudi tena Zenj, hawa na pamoja na wale ambao tayali walikuwa wameajiliwa na SMZ. Huku ukumbizi ukizidi kuvuma visiwani humo, wengi waliona ni heri kutorudi tena visiwani huko. Tatizo lilikuwa ni fedha, kwani katika siku za mwisho mwisho SMZ ilikata kutuma fedha, na kutoa ahadi kuwa malipo yatafanyika mara wanafunzi watakaporudi visiwani. Kwao hili halikuwa tatizo kubwa. Na mara baada ya kurudi na kulipwa wengi walikimbilia UK na USA ambapo wapo hadi sasa.

Wanafunzi waliobaki Malaysia waliona joto ya jiwe,kwani walifikia kushindwa hata kulipia pango la nyumba zao na kujikuta wakifukuzwa. Hata hivyo wengi katika waliobaki walikuwa bado na mapenzi makubwa na SMZ hivyo baada ya miaka yao kadhaa walirudi nyumbani na kukutana na kadhia dhidi ya Idara ya Utumishi ambayo ilitaa kuwatambua, mbaya zaidi Komandoo alikuwa atayali amemaliza muda wake. hiki kilikuwa ni kipindi cha Karume ambaye aliamua kwa makusudi kutowatambua wanafunzi hao.

Cha msingi ni kujiuliza ni kwa nini SMZ chini ya Karume ilishindwa kuwatambua wanafunzi ambao waliona bora kurudi nyumbani ili kuendeleza maendeleo ya visiwa hivyo. Ukiangalia kwa kina utaona ni mabo mengi ambayo yalianzishwa na Komandoo yalibezwa na Karume, huku idara ya Utumishi ikilipa kisasi kwa kunyang'anywa kazi yake ya kusomesha wanafunzi wafanyakazi na wizara ya fedha. Mambo mengi yaliamuriwa kutokana na utashishi binafsi pasipo kufuata taratibu za kisheria, kiasi cha kuona kuwa SMZ haina dira yotote katika kumwendeleza mwanachi wake.

Leo hii ukiangalia ni wangapi katika mamia wale ambao walisomeshwa na SMZ, ambao bado wapo hapo visiwani ni kichekesho. Mpaka leo hii SMZ inadaiwa na wanafunzi hao, na Karume ambae mwakani anamaliza muda wake katia pamba masikioni mwake! Hataki kusikia chochote kuhusu madai wa wanafunzi hao! Na sio kama haoni mafanikio ya wale wachache waliobaki ili kuendeleza nchi hiyo bali ni kwa kuwa SMZ yote kwa ujumla haijui inafanya nini.... ipo ipo tu!

Wednesday 29 July 2009

Kadhia hii kwisha yakianza kuchimbwa...?


Vespa inapokuwa inainamishwa upande mmoja ni dalili ya upungufu wa wese, hata hivyo kwa muda sasa kumekuwepo na malumbano marefu juu ya uchimbaji wa mafuta huko Zenj na umiliki wa mafuta hayo... Je iwapo mafuta hayo yatachimbwa chini ya umiliki wa Zenj, kadhia hii kwa maelfu wa wenye vyombo vya moto visiwani humo itakuwa imefikia kikomo?

Tuesday 14 July 2009

Ngoma Africa Band Kupeleka Moto Mwingine Tampere! Finland




The Ngoma Africa Band aka FFU! wanatarajiwa kutumbuiza katika onyesho la
FEST AFRIKA, mjini Tampere, huko Finland siku ya Jumamosi 18-07-2009.

Katika maonyesho hayo pia kutakuwapo na bendi nyingine za mziki na vikundi vingine vingi vya sanaa za maonyesho kikiwemo kikundi maarufu cha The Mpondas Group chenye maskani yake mjini Tampere.bendi ya The Ngoma Africa ilikuwapo Ufini mwanzoni mwa mwezi wa February mwaka 2009 katika misimu wa barafu huko ufini,na kufanikiwa kuwasha moto wake wa mziki.

Wadau wa Scandinavia bendi yenu inakuja kufanya kazi mliyowatuma kufanya nanyo ni mziki moto moto!.

The Ngoma Africa bendi inayotingisha majukwaa kila kukicha bado inaendelea na kufuka majukwaa kama vile moto wa nyikani.

Wasilikize hapa www.myspace.com/thengomaafrica ukiwataka ngoma4u@googlemail.com

Sunday 5 July 2009

Kujinafsi....





Tuesday 30 June 2009

Leo ni siku kubwa kwangu....


Leo ni siku kubwa kwangu, na ni baada ya kumaliza masomo ya Mazingira katika ngazi ya Shahada... Hapa nipo njiani kwenda kuchukua Nondo yangu. Aidha kwangu mimi ni sehemu kubwa ya mafanikio yangu binafsi na jamii mbalimbali ambako nilijitolea wakati wote wa masomo yangu katika kukamilisha miradi yao.

Habari zaidi nitaziandika mara baada ya kukabidhiwa ramsi Nondo hii... Kwa wale ambao wapo Tampere na Helsinki mnakaribishwa kujumuika nami katika siku hii adhimu.

Monday 29 June 2009

Mpemba na kuku

Saturday 20 June 2009

Leo ni Mwaka Kogwa....


Maelfu ya Wazenj leo wanaungana na Wanamakuduchi katika siku ya kuoga mwaka maarufu kama Mwaka Kogwa. Hizi ni sherehe za kimila zinazofanyika kila mwaka katika mwezi huu wa saba.

Kwa habari zaidi tembelea hapa

Saturday 30 May 2009

Ajali ya Mv Fatih



Tunasikitika kuwatangazia ajali mbaya ya meli ya mizigo (Mv. Fathi ya kampuni ya Seagul mali ya Bwana Said Mbuzi) ambayo ilikuwa ikitokea Zanzibar kuja Dar. Inasemekana kuna idadi kubwa ya watu waliopoteza maisha

Source: Jamii Forums



All pictures by Kibunango

Tuesday 26 May 2009

Bia, Konyagi na Sigara


Zenj unaweza kwenda baa na Konyagi yako ulionunua katika duka la ulevi na kuinywa hapo baa pasipo kupata usumbufu toka kwa mwenye baa. Unachotakiwa kufanya ni kuagiza maji au bia na glasi tu!

Friday 22 May 2009

Maili Nne- Zenj


Maili Nne ni kitongoji ambacho kimejengwa bila ya viwanja vyake kupimwa na Idara ya Upimaji. Ni kitongoji ambacho ni mfano katika kupanga nyumba pasipo kuwashirikisha wataalumu ambao wamekuwa na visingizio chungu nzima katika suala la kupima ardhi.

Monday 4 May 2009

Avumae Baharini ni Papa.....


Kwa mara ya kwanza vidagaa baharini vimeanza kujiuliza ni nani mkubwa kati ya Papa na Nyangumi, huku wakiwa wamesahau kuwa avumae bahari ni Papa lakini kubwa lao ni Nyangumi..!

Papa ndie anaye aminika kutamba baharini, kwa mwendo wake wa kasi na mashambulizi ya ghafla tena ya kutisha, kiasi ya kumfanya awe ni maarufu sana baharini.

Hivi karibuni katika vita vya mafahali wawili wa baharini, imeonekana kuwa pamoja na ukubwa wa Nyangumi, Papa bado ni maarufu sana kwa ukubwa katika bahari ya maharamia wa meli hadi kule kwa prez asie tumia ndomu. Hata hivyo wataalumu wa mambo wanasema ni nadra sana kwa vidagaa, vibua, ngisi, pweza, changu,tasi na aina nyingine ya visamaki katika eneo hilo kumwona Nyangumi, hivyo kwao Papa bado ndio samaki/mnyama mkubwa kabisa licha ya kuwepo kwa Nyangumi.

Kama vile haitoshi vidagaa hivyo, ambavyo mara nyingi hukaa mbali na Papa, wameendelea kuhoji ni kwa nini Papa ametumia televisheni ya taifa la wanyama wa baharini,kujinadi kama yeye sio mkubwa kama Nyangumi, wakisahau kuwa Papa hana ubavu kama wa Nyangumi ambae ametumia televisheni yake yenye uwezo wa kuonekana live katika eneo lote avumalo Papa!

Kuna taarifa ambazo sio rasmi kuwa Nyangumi atajaa tena kwenye televisheni yake akipinga madai kuwa yenye ndie mtafunaji wa kwanza wa vidagaa na aina nyingine ya visamaki katika eneo hilo la bahari, huku vidagaa vingine vikifanya mpango wa kwenda kwenye maeneo ambayo Nyangumi amekuwa akivuliwa kwa wingi ili kuweza kujionea samaki hilo lipo la aina gani, na kama inawezekana kuliondoa katika eneo lao la bahari, licha ya madai yake kuwa yupo katika kuwatetea vidagaa na umaarufu wa Papa.


__________________

Sunday 26 April 2009

Muungano unazidi kukua, miaka 45 sio mchezo...


Katika kusherehekea miaka 45 ya Muungano nimejikuta nikikumbuka sana shoki shoki, matunda yenye radha ya aina yake ni maarufu sana hapo Zenj. Anyway lengo ni kusherekea muungano, miaka 45 sio mchezo! Muungano huu ambao ulizaliwa na mambo kumi na moja, sasa una mambo 38 na bado una kero ambazo kuchwa zinapigiwa kelele! Sasa cha kujiuliza muungano huu unakua au unapolomoka. Ukiangalia idadi ya mambo yanayounganisha nchi mbili hizi utaona kama unakua na kama unakuwa unaelekea upande gani? Kuunganisha kila jambo na kuwa na serikali moja?

Hata hivyo dalili zinaonyesha kuwa mengi kati ya hayo 38 yameingizwa kwa upande mmoja kuburuzwa na upande mwingine, ndio maana kumezaliwa neno kero za muungano! Kwa hali ya sasa dalili za kukua kwa muungano huu ni kidogo kuliko kukua kwa kero zake! Nini kifanyike? yarudishwe yale 11 ya mwanzo au haya ya sasa yajadiliwe kwa kina na kuondoa hizo kero. Je ni upande mmoja tu wa muungano ambao unaona kuna kero? na kama ni hivyo upande mwingine wa muungano unajisikia vipi kukaa kimya na kutosikiliza kero za upande mwingine? Ni kiburi ama dharau? Au kuna ajenda ya siri?

Nawatakiwa kila heri watanzania wote katika siku hii muhimu ya kuzaliwa kwa Tanzania.

Saturday 18 April 2009

Kisauni Airport kuongezwa kwa mita 560


Zanzibar International Airport maarufu duniani kama Kisauni Airport inatazamiwa kuongezwa urefu wa njia yake kwa mita 560. Ni katika mradi uliopatiwa fedha na Benki ya Dunia.
Uwanja wa Kisauni umekuwa ukifanyiwa matengenezo mara kwa mara, ili kukidhi ongezeko la matumizi ya uwanja huo na hasa baada ya kukua kwa sekta ya utalii visiwani humo.

Matengenezo haya yatajumuisha ukarabati wa jengo la uwanja pamoja na utiaji wa uzio katika baadhi ya maeneo ya uwanja huo ambayo yapo hatarini kuvamiwa kwa ujenzi wa nyumba za kuishi. Aidha kampuni itakayofanyia matengezeno uwanja huo Sogea Satom ya Ufaransa imenukuliwa ikisema kazi hiyo itachukua muda wa mwaka mmoja na miezi mitatu kukamilika.



Wednesday 15 April 2009

Zenj kuondokana na mafuta ya kwenye Rambo




Japo mtaalamu wa uchunguzi wa kuwepo kwa mafuta katika visiwa vya Zenj alisema mafuta katika visiwa hivyo hayatoshi kwa uchimbaji wa kibiashara, Wawakilishi walimjibu kuwa hata kama ni kidogo kwa ujazo wa kinibu, mafuta hayo ni kwa ajili ya Wazenj na watagawana hivyohivyo! Mbaya zaidi kwa mtaalamu huyo kupendekeza kuwa mafuta hayo yawe chini ya Muungano, jambo ambalo lilizua jambo lingine kwa mahasimu wa siasa visiwani humo kukaa pamoja na kupinga kwa nguvu zote kauli ya mtaalamu huyo aliyejikusanyia vijisenti kadhaa baada ya kukamilisha ripoti yake.

Kadhia ya upitikanaji wa mafuta visiwani humo imekuwa ya muda mrefu licha ya kuwepo kwa vituo vya kutosha kwa ajili ya uuzaji wa mafuta hayo. Watumia vyombo wanajua usumbufu mkubwa wanaoupata wakati bidhaa hiyo adimu inapokosekana visiwani humo.Kiasi cha kufikia kununua mafuta vichochoroni tena yaliyohifadhiwa katika maplastiki na vifuko vya Rambo.Usumbufu huu hauishii kwa wenye vyombo tu bali utambaa na kuenea kwa kila mwananchi wa visiwa hivyo kwa namna moja ama nyingine.

Kauli ya Waziri Mansoor Yusuf Himid katika suala la mafuta aliyoitoa hivi karibuni, inabainisha wazi kuwa serikali ya muungano wa tz(SMT)kupitia shirika lake la TPDC limekuwa likifanya uchunguzi na utafutaji wa mafuta katika visiwa vya Zenj kinyume na makubaliano ya ndoa...Muungano wa Tanganyika na Zenj. TPDC kwa zaidi ya miaka kumi sasa imekuwa ikiingia mikataba na kampuni za uchunguzi wa mafuta katika maeneo ya kujidai ya visiwa hivyo kana kwamba suala la mafuta ni la Muungano. Wawakilishi kwa upande wao walisimamia kidete kuzuia TPDC kunusanusa uwepo wa mafuta katika visiwa hivyo, huku wananchi wa visiwani wakisuburi kwa hamu kujua ubavu wa SMZ dhidi ya SMT.
Waziri Mkuu wa SMT Mizengo Pinda, kwa kuona kuwa kuna tatizo hapo amekubaliana na Waziri Kiongozi wa SMZ Nahodha kuwa mafuta katika Zenj yafanyiwe uchunguzi na wazenj wenyewe na kuweza kuyachimba wao wenyewe hata kama ni kidogo kwa kuweza kujipaka mwilini kwa siku mbili tu. Ingawa kaurusha mpira kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano ili kutoa kauli ya mwisho juu ya mstakabala wa mafuta.

Kinachoshangaza hapo ni kwanini suala hili lipelekwe kwenye Bunge ilhali Bunge hilo haliyawahi kukaa hata siku moja na kusema kuwa mafuta ni suala la muungano? zaidi ya watendaji wa SMT kwa utashi wao binafsi kuliingiza suala hili ndani ya Muungano! Hiki ni kichekesho kikubwa katika kadhia za Muungano huu!

Kinachofurahisha ni jinsi gani SMZ mara hii ilivyoweza kukataa kuburuzwa na SMT. Kuna mambo mengi ambayo SMZ imekuwa ikipelekweshwa mbio na kuna mengi ambayo yamekuwa yakiingizwa kwenye SMT pasipo kuwashirikisha wazenj, ambapo uhambulia taarifa tu kuwa jambo fulani lipo kwanye Muungano!

Ili kulinda na kuendeleza Muungano huu ni vema kwa SMT kuacha tabia yake ya muda mrefu ya kujichukulia uwamuzi pasipo kuwashirikisha wenzao wa SMZ. Ni vema wakakumbuka kuwa Muungano huu ulifikiwa kwa makubaliano ya nchi mbili tena kwa mambo kadhaa na sio sahihi kuongeza mambo mengine bila ridhaa ya upande pili. Hali kadhalika SMT waache kujisahau kuwa wana nafasi sawa na SMZ katika hatima ya muungano huu na hivyo ni vema wakawa na heshima!

Tuesday 7 April 2009

Leo ni siku ya Karume


Watanzania leo wanaungana na ndugu zao wa Zenj katika siku hii muhimu ya kumbukumbu ya A.Karume rais wa kwanza wa Zanzibar na Muasisi wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Wednesday 25 March 2009

Huu Ndio Wakati Muafaka wa Kumiliki gari la Waziri wa SMZ


Mara kadhaa nimewahi kuandika juu ya ubabe wa SMZ dhidi ya Mahkama za Zenj, zaidi ya SMZ hata wananchi wakati mwingine wamekuwa na ubabe dhidi ya maamuzi ya Mahkama za Zenj. Kumekuwepo na hukumu mbalimbali kila siku, ila zinazonipa mashaka ni zile hukumu za kesi za madai. SMZ kama mhimili wa Mahkama imekuwa kwa mara kadhaa ikishitakiwa katika kesi za madai kutoka na ubabe wake wa kushindwa kufuata sheria zake.

Kesi nyingi ambazo SMZ na asasi zake zimekuwa zikijikuta matatani zinatokana na matatizo ya ardhi na madeni yanayotokana na huduma mbalimbali wanazoomba kufanyiwa na hatimae kushindwa kulizipia. Mwaka 2006 niliwahi kuandika jinsi gani Mahakama za Zenj zinapoonja ubabe wa SMZ na wananchi wake kiasi cha mtu kujiuliza iwapo utakuwa na matatizo ambayo yanahitaji haki kutendeka utakimbilia wapi!

Mwaka huo wa 2006 kulikuwa na kesi mbili za muda mrefu ambazo zilipata hukumu yake, lakini zikakutana na ubabe wakati wa utekelezaji wake, kama inavyoelezwa kwa kirefu chini ya bandiko la "Mahakama za Zenj na Matatizo ya Ubabe"

SMZ kwa kujua au kwa makusudi kabisa imekuwa ikipuuza madai mengi ya wananchi wake dhidi ya asasi yake. Nakumbuka kesi nyingi katika hili lakini moja iliyonivutia ni ile ya asasi moja ya SMZ kuibeza amri ya Mahkama kuhusu uvunjaji wa mabanda ya biashara ili kupisha ujenzi wa soko katika eneo la Mwanakwerekwe.

Wengi wa wananchi wamekuwa na madai mbalimbali na wanapokimbilia katika vyombo vya SMZ ili kupata suluhisho, uvunjika moyo jinsi wanavyosumbuliwa na inahitaji moyo wa ziada kwenda Mahakamani ambako ni sawa na kumpa Nyani kesi ya Ngedere. Binafsi nimekuwa nikipigwa tarehe zaidi ya miaka tisa kwa madai ya haki yangu ambayo niliingia mkataba na SMZ.

Hatua ya Mahakama Kuu kupiga mnada magari ya SMZ kwa kushindwa kulipa deni lake la matengenezo ya ikulu ndogo huko Pemba ni ya kuungwa mkono sana. Amri hii iwapo itafanikiwa itakuwa ya kuigwa na kupigiwa mfano. Moja ya mali ambayo inaweza kupigwa mnada ni gari la Mh. Waziri ambae wizara yake inahusika moja kwa moja na kushindwa kufuata taratibu za kuheshimu mikataba. Nategemea jeshi la polisi visiwani humo kusimamia vizuri ushikwaji wa mali hizo za SMZ na hatimae kupigwa mnada. Hii inaweza kuondoa usingizi mzito kwa watendaji wa SMZ kuhusu kuheshimu mikataba wanayoingia.

Tuesday 24 March 2009

Agha Khan na Mji Mkongwe....

Agha Khan Development Network kwa zaidi ya miaka kumi sasa imekuwa ikifanya ukarabati mkubwa katika baadhi ya Majengo ya Mji Mkongwe wa Zanzibar. Na hivi karibuni walikuwa katika hatua za mwisho mwisho za kukamilisha ukarabati wa Forodhani Park.
Leo nitaangalia majengo mawili, nikianzia na Stone Town Culture Centre maarufu kama Old Dispensary ambalo ni mojawapo ya majengo yaliyofanyiwa ukarabati na AKDN baada ya kutupwa na SMZ. Aidha jengo lingine lililolembewa na SMZ ni Extelcom, ambalo leo hii kuingia ndani ya jengo hilo inabidi uwe nazo mfukoni.

Old Dispensary.

Jengo hili ujenzi wake ulikamilika mwaka 1894 chini ya ushauri wa kihandisi toka Uingereza. Michoro na mafundi wa jengo hili ni kutoka India ambako ndipo alipotoka mwenye jengo Bw. Tharia Topan ingawa hakuweza kuona kukamilika kwa ujenzi wa jengo hilo.

Mjane wa Topan aliweza kuendeleza ujenzi na baadae kuliuza. Lengo la Topan lilikuwa kujenga shule na zahanati, ambapo mmiliki wa mwisho wa jengo hilo aliweza kufanya sehemu ya chini ya jengo hilo kuwa zahanati na sehemu ya juu kuwa sehemu ya makaazi yake. Huu ndio ukawa mwanzo wa jina maarufu la Old Dispensary.

Miaka 70 baadae jengo hilo likawa tupu, na kuendelea kuwa tupu huku likiendelea kuchakaa na kuharibika ni hadi pale Agha Khan walipopewa ruhusa ya kulifanyia ukarabati ili kunusuru ufundi mkubwa uliotumika katika ujenzi huo kupotea na hasa nakshi zake za kihindi.


Miaka 100 baadae Agha Khan waliweza kupata kibali cha ukarabati wa jengo hilo, zaidi walipewa mkataba mpya wa kukodishwa jengo hilo na SMZ chini ya muda maalumu. Pichani hapo juu ni old dispensary baada ya kufanyiwa ukarabati mkubwa .


Extelcom
Jengo lingine ambalo lilikuwa chini ya SMZ na kuachwa bila aina yoyote ile ya usimamizi hadi pale walipotokea tena agha khan na kuamua kuligeuza toka ofisi hadi kuwa hoteli ya kitalii. Sasa jengo hili linajulikana kama Serena Inn

Thursday 19 March 2009

Movie...Hobbie iliyokwisha huko Zenj


Jengo hili sasa halitumiki tena kama jumba la Sinema..!

Wednesday 18 March 2009

Amin Salmin Amour, aonja tamu ya siasa

Ni baada ya kushindwa kutamba kwenye kura za awali za kumtafuta mgombea kwa tiketi ya CCM katika jimbo la Magogoni huko Zenj. Amin ambaye ni mtoto wa rais mstaafu wa Zenj Salmin Amour maarufu kama Komandoo, alikuwa ni miongoni wa wagombea 10 wa CCM waliojitokeza kuwania nafasi hiyo.

Umaarufu wa Amin unakwenda nyuma zaidi kipindi cha kwanza cha Komandoo Salmin alipokuwa madarakani,umaarufu wake ulijengeka kwa kuwa mjasirimali zaidi ya siasa na kwa kujaribu kila aina ya biashara za muda mfupi! Hatua yake ya kuingia kwenye siasa kwa wengi ilikuwa ni karata yake muhimu ya kujinyanyua tena baada ya kushindwa kudumu katika sekta ya biashara.

Kwa habari zaidi tembelea hapa

Sunday 8 March 2009

Nani Mjinga Hapa?


Pichani ni mwanamke wa kizenj akiwa katika pilika pilika zake ufukweni, na pembeni kushoto ni mtalii akicheza na maji.

Jaribu kuangalia tofauti ya mavazi kati ya wanawake hawa wawili, halafu jaribu kufikilia hali ya hewa ya Zanzibar, bila kusahau udhaifu wa ngozi za watalii dhidi ya jua kali la ikweta.

Je unafikili kati ya hawa wanawake ni nani mjinga kutokana na aina ya mavazi yake?

Friday 6 March 2009

Maji ya Karume Bai bai, Karibu maji ya Japan



Kwa muda mrefu kisiwa cha Zanzibar kimekuwa kikipata huduma ya maji bure, hatua ambayo ilitokana na mapinduzi ya mwaka 1964. Huduma hiyo muhimu kabisa katika maisha ya kila siku ya binadamu ilibatizwa jina na kuitwa maji ya Karume. Hata hivyo jina hilo halikuja burebure tu! kuna sababu kadhaa ambazo zilisababisha maji hayo yaitwe ya Karume. Moja ya sababu kubwa ilikuwa ni upungufu wa maji na hasa katika halmashauri ya manispaa ya Zanzibar,ambapo wananchi wengi walijikuta wakitafuta maji sehemu mbalimbali za manispaa hiyo. Usumbufu wa upatikanaji wa maji ulisababisha maji hayo kuitwa Maji ya Karume ambayo yalikuwa ni bure lakini shida kupatikana.

Maendeleo yote yaliyotokana na mapinduzi yaligeuka kuwa adha na kero baada ya maji kupungua katika manispaa, Majengo kama ya Mjeru pale Kikwajuni ambayo yalikuwa yakipata maji muda wote yalijikuta yakikosa maji muda mwingi wa mchana na maji yaliweza kutoka usiku tu, na ni usiku wa manane, hivyo kuwafanya wakaazi wake kubadilisha ratiba ya kulala ili waweze kukinga maji. Hali hii ilikuwepo kwa maeneo ya Kilimani, Michenzani na sehemu kadha wa kadha katika manispaa hiyo.

Ukosefu wa maji ya kutosha katika maeneo hayo ambayo yalikuwa na nyumba za ghorofa kulisababisha kubadilika kwa sura za majumba hayo kwa uwekaji wa pump za maji,nyingi katiya hizo kufungwa kienyeji tu na kuendelea kuwa kero kwa wananchi hao. Aidha uchimbaji wa makaro makubwa ya kuhifadhia maji chini ardhi ulishamiri na kupunguza upatikanaji wa maji hayo machache/kidogo kwa wakaazi wengine. Uchimbaji wa visima vile vile ulishamiri kando kando ya manispaa hiyo. Hii yote ilitokana na upungufu mkubwa wa maji ya Karume.

SMZ kwa upande wake walijitahidi kuona kero hiyo inaondoka, lakini mara zote miradi ya maji yenye nia ya kuwa endelevu ilishindwa kuendelea kutokana na SMZ kuendelea kupendelea kuwa na Maji ya Karume.

Wananchi kwa upande wao walikuwa tayali kulipia huduma za maji,hii inaonyeshwa na mifao kadhaa ya baadhi ya wananchi walioamua kutafuta njia za kudumu za upatikanaji wa maji katika maeneo yao. Miradi mingi midogo midogo ya maji iliyowashirikisha wananchi ilifunguliwa na mingi katika hiyo ilitumika kama mifano katika hatua za awali za semina mbalimbali za kubadili msimamo wa serikali na maji yao ya Karume.

Maji ya Karume yalianza kuaagwa rasmi tokea mwaka jana, hata hivyo sio wananchi wote ambao wameweza kupata maji ya Japan licha ya Idara ya maji kuwatumia ankara za maji. Hii kwa upande mmoja inaonyesha kuwa Idara ya Maji bado haijawa makini katika kuona kuwa maji yanalipiwa na yule tu ambae mfereji wake haukauki maji, na sio wale wenye mifereji iliyokauka au ile yenye kupiga filimbi kama maji yanakuja kumbe la..!

Udhaifu huu unathibitishwa na Waziri wa Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi,Bw, Mansour Yussuf Himid katika kauli yake aliyoitoa hivi majuzi wakati wa kusaini awamu ya pili ya maji ya Japan

``Napenda kutoa wito kwa wale wanaopata huduma ya maji kukubali kuchangia na wale wasiopata hawatatozwa fedha hadi hapo watakapoanza kupata maji ya uhakika,``

Tuesday 3 March 2009

Bwejuu Zenj, ina beach nzuri kabisa hapo Afrika Mashariki

Inashikilia rekodi hiyo kwa miaka miwili sasa...
Ni kivutio kikubwa cha watalii katika Zanzibar




Ever wanted to feel like a castaway in a warm, secluded oasis of tranquility and beauty? Conde Nast Traveler has scoured the globe to find the best island beaches.
Following is a list of their top 10 choices:
1. Shipwreck Beach, Zakynthos, Greece -- This is an idyllic, isolated beach scooped out of a vertical wall of white rock.

2. Cumberland Island, Georgia -- With only 300 visitors allowed per day it equates to about 18 tourists per mile of beach.

3. Anse Victorin, Fregate Island, Seychelles -- Almost deserted, the crescent-shaped beach has soft sand, clear, tranquil water and a backdrop of palms and cliffs.
4. Lido, Venice, Italy -- The ultimate seaside resort made famous by author Thomas Mann in Death in Venice.

5. 7-Mile Beach, Negril, Jamaica --The right mix of white sand, tranquil water and enough beach life to keep anyone from getting bored.

6. Gibson Beach, Sagaponack, New York -- With no amenities of any kind, this wild swath of dunes, surf and fabulously wealthy homes is a beach that attracts Manhattan's beautiful people. With minimal parking, cycling is a preferred transport.

7. Cocoa Island, Maldives -- Tiny Cocoa Island is virtually all beach.

8. Bwejuu, Zanzibar, Tanzania -- It's one of the most exotic of Africa's islands and Bwejuu is its wide and blindingly white beach.

9. Kamala Beach, Phuket, Thailand -- The western shores are thick with beaches, and many of those beaches are bustling with commercial activity including food vendors, gift shops, bars and other distractions. Kamala is the antidote. Kamala Bay's main street is a convivial integration of seafood restaurants, shops, and bars that are notably tamer.

10. Waikiki, Oahu, Hawaii -- There's no such thing as boredom in Waikiki. The shops, restaurants and parks of Honolulu are just a block away.

Wednesday 25 February 2009

Wikipedia ya Kiswahili

Watanzania wote wanakaribishwa kuchangia habari za mahali wanapoishi au wanapotoka katika wikipedia ya Kiswahili! (sw.wikipedia.com) Ijulikane ya kwamba wikipedia ni mradi mkubwa wa elimu unaojengwa na wachangiaji wanaojitolea bila malipo yoyote. Kila mtu anakaribishwa kuchangia!

Kwa sasa tumeanzisha makala fupi za kila kata kwenye mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Iringa, Kilimanjaro, Kigoma, Lindi, Mara, Mwanza, Mbeya, Manyara, Morogoro, Mtwara, Pwani na Tanga.

Angalia mfano huu: sw.wikipedia.org/wiki/Mkoa_wa_Mjini_Magharibi_Unguja

Chini kuna sanduku inayoonyesha mikoa yote. Ukiingia katika mkoa fulani unapata majina ya wilaya. Kila safari ukibonyeza kwenye neno lenye rangi ya buluu unapelekwa kwenye makala mpya. Ukifika kwenye wilaya utaona sanduku lenye majina ya kata za eneo hili. Makala mengi yana habari fupi tu kama "ABC ni kata ya wilaya DEF katika Mkoa wa XYZ. Idadi ya wakazi wake ilihesabiwa kuwa xxxxx katika sensa ya 2002". Kila mtu yuko huru kubonyeza kwenye sehemu ya "hariri" juu ya makala na kuongeza habari.

Baada ya kuongeza habari unabonyeza sehemu ya "Hifadhi ukurasa" iliyoko chini.


Taarifa hii imeletwa kwenu kwa hisani kubwa ya Bw. Kipala anayesimamia kamusi hiyo

Tuesday 24 February 2009

Zanzibar Hakuna Sheria za Ujenzi?

Zanzibar kama nchi, mji mkuu wake ni Zanzibar ambao unaundwa na Mji Mkongwe na Ng'ambo, kiutawala upo katika mkoa wa Mjini Magharibi. Mji wa Zanzibar unapata huduma zake kupitia Halmashauri ya Manispaa ya Zanzibar na Mamlaka ya Hifadhi na Uendelezaji wa Mji Mkongwe.

Halmashauri ya Manispaa kama halmashauri zingine duniani imepitia katika mabadiliko mengi ya kiutawala na sheria za kuongoza mji huo na hasa katika suala zima la ardhi na maendeleo yake kwa kushirikiana na idara zingine kama ofisi ya Mkuu wa wilaya, ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Kamisheni ya Ardhi na baadae Idara ya Mipango Miji na Idara ya Ardhi.

Masterplan ya kwanza kabisa ya mji wa Zanzibar ilitolewa mwaka 1923 chini ya sheria ya mji(Town Decree Cap 79). Master plan ilitolewa kutatua matatizo ya ukuaji wa mji kiholela, kupanua wigo wa miundo mbinu na kurahisisha mizunguko katika mji huo ambao ulikuwa na watu 35000 huku asilimia 30 ya watu hao wakiishi Mji Mkongwe na asilimia 70 wakiishi Ng'ambo sehemu iliyokithiri kwa ujenzi holela.

Mwaka 1958 kulifanyika mabadiliko katika Master plan kwa kuingizwa kwa "Town Scheme" chini ya sheria ya mwaka 1955- "Town and Country Planning Decree" ambapo lengo lilikuwa kuandaa rasimu ya usafirishaji/usafiri katika mji mkongwe na kuendeleza maeneo ya wakaazi yaliyopimwa chini ya viwango huko Ng'ambo (semmi planned settlements)

Master plan ya pili "The Town Master Plan -1968" ilifanywa na Wajerumani, ikiwa na lengo la kuboresha zaidi maeneo ya Ng'ambo ambayo yalikuwa yakipanuka kwa kasi, huku umuhimu mkubwa ukiwekwa kwenye upatikanaji wa huduma muhimu kama vile mifereji, taa za kwenye mitaa na misingi ya maji taka.
Mafanikio yake ni pamoja na Majumba ya Mjeru pale Kikwajunina Majumba ya Kilimani.

Master plan kubwa na ya mwisho ilitolewa mwaka 1982 na wataalmu kutoka China. Pamoja na mabo mengine, master plan hiyo iliangalia zaidi kupanuliwa kwa mji wa Zanzibar kwa kupima maeneo mengine mapya ili kuruhusu nafasi kubwa zaidi kwa ya asilimia 68 ya wazenj waliokuwa wamebanana kupatiwa maeneo ya ujenzi huku wengi wakiishi katika maeneo yasiopimwa kisheria, aidha kutoa nafasi kubwa zaidi ya ujenzi kuanzia nyumba za kuishi shule na maeneo ya biashara, ilitizama vilevile kupunguza umwagaji wa maji taka baharini na kuzuia tabia iliyoanza ya kujenga nyumba katika maeneo yenye mafuriko.

Tokea master plan hiyo ya wachina kumekuwepo na nyongeza mbili moja ikiwa ni ya mwaka 1996 The Tourism Zoning Plan ambayo iliingizwa kwenye Master plan kukidhi mahitaji ya mahoteli na maeneo ya kitalii. Ya pili ni pendekezo la kuimarisha na kuanzisha miundo mbinu hasa katika maeneo ya Ng'ambo iliyopendekezwa na Zanzibar Sustainable Programm (ZSP) mwaka 1998.

Kwa nyakati tofauti maendeleo ya ujenzi na udhibiti wake yalikuwa yakisimamiwa na Joint Building Authority (JBA)ambayo ilianzishwa chini ya sheria ya Town and Country Planning Decree (cap 85) ya mwaka 1955, ikiwa na wajumbe watatu toka ambao ni Mkuu wa Afya, Mkuu wa Wilaya na Building Inspector. Kazi zao kubwa ilikuwa ni kutoa vibali vya ujenzi wa aina zote ndani ya mji wa Zanzibar na kudhiti ujenzi ndani ya mji huo kwa mujibu wa sheria ya mji. "Town Decree Cap 79 Subsidiary"

Mwaka 1969 SMZ ilizivunja Halmshauri za Miji na hivyo ukawa mwisho wa awamu ya kwanza ya JBA. Awamu ya pili ya JBA ilianza tena mwaka 1986 baada ya kurejeshwa kwa serikali za mitaa katika ikiwa na wajumbe wengi zaidi huku mkuu wa mkoa akiwa ndie mwenyekiti wake. Wajumbe wengi walitoka baraza la Manispaa, wakifuatiwa na wajumbe toka idara ya Ardhi, idara ya Upimaji na Mhandisi wa ujenzi. Kazi za JBA ziliendelea kufanyika chini ya sheria na taratibu za ujenzi kama zinavyooneshwa katika Cap 79 Subsidiary. Kati ya Mwaka 1969 na 1986 shughuli za ujenzi zilikuwa zikisimamiwa na serikali za majimbo, pasipo kufuata sheria yoyote za ujenzi zaidi ya uzoefu uliopatikana katika Cap 79 ya Town Decree.

Mwaka 1994 Sheria ya uendelezaji na uhifadhi wa Mji Mkongwe ilianza kufanya kazi, hivyo kuitoa JBA kama mdhibiti wa ujenzi katika eneo la Mji Mkongwe. JBA iliendelea kufanya kazi kufuata mipaka ya Master plan ya mwaka 1982 nje ya Mji mkongwe hadi mwaka 1995 ambapo kulitokea tena mgongano wa sheria. Mwaka 1995 ilianzishwa sheria mpya ya halmashauri za Miji Zanzibar, ikichukua sehemu kubwa za sheria za Town decree na kupunguza ukubwa wa Manispaa ya Zanzibar hali kadhalika kuibana zaidi JBA katika utendaji wake.

Kufikia hapa kazi za JBA ziliendelea kufanyika ila ni kwa ubabe tu, kwani chini ya sheria ya mwaka 1995 ya Manispaa ilionekana wazi kuwa JBA haikuwa na nafasi ya utendaji katika manispaa yenyewe na wilaya ya Magharibi. Ikiwa chini ya Mkuu wa Mkoa kama mwenyekiti na Baraza la Manispaa kama katibu, JBA iliendelea kufanya kazi huku ikijua inafanya hivyo kinyume na sheria na taratibu. Udhaifu wa Halmashauri ya wilaya ya Magharibi, nguvu ya kisheria ya Idara ya Ardhi na Idara ya Upimaji iliipa uhai kidogo JBA kutokana na kuwa na wajumbe toka katika Idara hizo.

Mwaka 2000 JBA ilivunjwa rasmi na moja ya sababu kubwa ya uvunjwaji wake ilikuwa ni zoezi la uvunjaji wa nyumba katika mitaa kadhaa ya Mkoa wa Mjini Magharibi iliyofanyika katika mwaka 1996, katika vyanzo vya maji, karibu na njia ya grid ya umeme wa Kidatu na maeneo mengine yaliyovamiwa, ambapo ilionekana zoezi zima limefanyika kisiasa zaidi kuliko kufuata taratibu. Manispaa kwa upande mwingine chini ya sheria ya mwaka 1995 waliona kuwa JBA ni mzigo kwao na walitaka ichukuliwe na asasi nyingine yoyote ya serikali. Kuvunjwa kwa JBA kulitoa nafasi ya kuanzishwa kwa UDCA (Urban Development Control Authority)ambayo ilianzishwa chini ya sheria ya 1955 ya Town and Country Planning decree ambayo ipo chini ya Wizara ya Ardhi na Upimaji. Safari hii Mwenyekiti wake akiwa ni Mkurugenzi wa Manispaa na katibu akiwa ni Town Planner wa Manispaa na wajumbe wengine 10 toka katika asasi zingine zinazohusika na ujenzi. Kwa ufupi UDCA ipo lakini haina nguvu kisheria kutokana na kuwepo kwa sheria ya Halmashauri ya Manispaa ya Mwaka 1995. Aidha sheria iliyotumika na Waziri huyo haina nafasi katika Halmashauri ya Manispaa, kwani Mkurugenzi wa Halmshauri anawajibika kwa Waziri wa Tawala za Mikoa na si venginevyo. UDCA inaendelea kufanya kazi kutokana na mazoea ya kuwepo na kitengo kama hicho katika miaka iliyopita.

Tukio lililotokea hivi karibuni la uvunjaji wa nyumba na misingi ya nyumba katika shehia ya Tomondo lililo fanyika chini ya amri ya Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Mhe. Abdallah Mwinyi, licha ya kuwa ni la kinyama halikufuata utaratibu wowote wa kisheria, zaidi limenikumbusha mojawapo ya sababu ya kumwondoa Mkuu wa Mkoa katika kudhibiti ujenzi visiwani humo. Aidha limenikumbusha kuwa Zanzibar Mjini hakuna sheria ya Ujenzi na kuna asasi nne zote hizo zikidai kuhusika na maendeleo ya ardhi katika mji huo na kufanya kuwepo na vurugu tupu katika kusimamia masuala ya ujenzi katika Mkoa huo wa Mjini Magharibi.

Aidha kuna umuhimu mkubwa kuona kuwa migongano ndani ya Mipaka ya Master plan ya mwaka 1982 inakwisha na kuna umuhimu mkubwa kuona kuwa Idara ya Upimaji, Idara ya Ardhi, Mamlaka ya Hifadhi na Uendelezaji Mji Mkongwe, Halmshauri ya Manispaa ya Zanzibar, Halmashauri ya Magharibi, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Ofisi ya Mkuu wa wilaya ya magharibi pamoja na ofisi ya Mwanasheria mkuu wa serikali wanakaa pamoja na kuamua ni sheria gani ya ujenzi itumike katika eneo la master plan ya mwaka 1982. Kwani kwa sasa hakuna sheria inayotumika zaidi ya wizi mtupu. Yaani inatia aibu kwa wizi huu wa mchana kweupe, huku wanaoumia ni wananchi wasio jua wafuate sheria gani kupata kibali halali cha ujenzi wa nyumba zao.